KOCHA wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema baada ya kumaliza vibaya mzunguko wa kwanza, mipango na mkakati wa timu hiyo kwa sasa ni kufanya vizuri mechi zilizobakia.
Hadi sasa Ceasiaa imekusanya pointi nane pekee kwenye mechi 10 ilizocheza ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi, ikishinda mechi mbili sare mbili na kupoteza sita.
Akizungumza na Mwanaspoti Chobanka amesema baada ya kupoteza pointi 23 za mzunguko wa kwanza mkakati wao kwa sasa ni kuzirudisha mzunguko wa pili.
Aliongeza wanaamini makosa waliyofanya kwenye mechi 10 hawatayarudia raundi zinazofuata na ujio wa wachezaji watatu wa kigeni unaongeza ushindani kikosini hapo.
“Ni kweli hali yetu sio nzuri tuko nafasi ya 10 kama tutaendelea kucheza hivi basi huenda tukafanya vibaya na hilo siyo lengo letu, tunaamini makosa tuliyofanya hayatajirudia tumejifunza,” amesema Chobanka na kuongeza;
“Hivyo mechi zilizosalia angalau tushinde mechi sita za nyumbani halafu zingine tutajua tunafanyaje ugenini ili tuweze kuepukana na changamoto ya kushuka.”