MBONGO anayekipiga Port Fouad inayoshiriki Ligi daraja la pili Misri Oscar Evalisto amesema dakika 50 alizocheza akiwa na chama hilo jipya zimempa taswira ya namna gani anapaswa kuwania namba.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Fouad hivi karibuni akitokea Makadi FC inayoshiriki ligi daraja la tatu nchini humo na msimu mmoja alioitumikia timu hiyo alifunga mabao matano na asisti nne.
Akizungumza na Mwanaspoti, Evalisto amesema dakika 50 alizocheza amefunga bao moja na asiti moja kwenye mechi mbili jambo ambalo anatamani kuwa na muendelezo.
“Nimecheza mechi mbili na nimeshafunga bao moja mechi yangu ya kwanza nilicheza dakika 20, ya pili nilicheza dakika 30 kila mechi kwangu ni nafasi ya kupambana zaidi na kuonyesha uwezo wangu,” amesema Evalisto na kuongeza;
“Ushindani hapa ni mkubwa sana kwa maana timu hii ina wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa. Baadhi yao wamecheza hadi katika timu ya taifa naamini katika uwezo wangu na ni suala la muda tu nitakuwa mchezaji muhimu katika hii timu.”
“Malengo yangu ni kujihakikishia kwanza kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza (first eleven) baada ya hapo mengine yatafuata kikubwa juhudi na kuheshimu maelekezo ya kocha.”