Dalili kama mtoto wako ana tatizo la afya ya akili

Wataalamu wa afya ya akili wanasema wazazi wanapaswa kuwa waangalifu zaidi katika kubaini dalili za matatizo ya afya ya akili kwa watoto wao, wakibainisha kuwa changamoto hizo huanza mapema.

Hata hivyo, wanasema mara nyingi dalili hizo huchukuliwa kimakosa, kwamba mtoto ni mkaidi au ana tabia mbaya.

Nilipata kuzungumza na mwanasaikolojia wa watoto aliyeniambia watoto huonyesha ishara za awali kupitia mabadiliko ya tabia na hisia, ambayo yakipuuzwa, huweza kuathiri makuzi yao ya nyumbani ma hata ya kielimu.

Mtaalamu huyo aliniambia mzazi anapomuona mtoto wake aliyekuwa mchangamfu anajitenga, anakosa hamu ya kucheza au kuanza kuwa mkimya kupita kiasi kwa muda mrefu, hilo si jambo la kawaida, mzazi unapaswa kuchunguza.

Kwa mujibu wa machapisho niliyowahi kuyasoma kuhusiana na magonjwa ya akili, dalili nyingine kwa mtoto ni ile ya kuwa na huzuni ya kudumu, hasira zisizo na sababu, hofu kupita kiasi au wasiwasi mkubwa hata awapo katika mazingira salama.

Ndiyo maana katika nyakati hizi, watoto wengi hushindwa kueleza wanachopitia kwa maneno, hivyo hisia zao hujitokeza kwa kulia mara kwa mara, kuogopa kwenda shule au kujilaumu.

Wataalamu hao pia wanataja mabadiliko ya usingizi na ulaji kama ishara muhimu kwamba, mtoto anaweza kushindwa kulala, kuota ndoto mbaya mara kwa mara, kulala kupita kiasi au kupoteza hamu ya kula.Hali hizi mara nyingi huambatana na uchovu na kushuka kwa umakini darasani.

Kwa upande wake, mshauri nasaha na mtaalamu wa malezi ambaye nilipata pia kuzungumza naye, Rehema Salum, anasema hata kushuka kwa ufaulu wa mtoto shuleni na ongezeko la malalamiko ya walimu kuhusu tabia yake mbaya, ni dalili ambazo wazazi hawapaswi kuzichukulia juu juu.

Mfano mzazi akipigiwa simu mara kwa mara kutoka shuleni kuhusu mwenendo wa mtoto, ni vyema akaanza kujiuliza kuna nini nyuma ya tabia hizo, badala ya kumwadhibu bila kumuelewa.

Kwa sababu baadhi ya watoto huanza kulalamika mara kwa mara maumivu ya tumbo au kichwa bila sababu ya kitabibu. Kwa mujibu wa wataalamu, hali hiyo mara nyingi huhusishwa na msongo wa mawazo au hofu iliyojificha.

Kuhusu hatua za kuchukua, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa mawasiliano ya wazi kati ya mzazi na mtoto.

Mzazi anashauriwa kuzungumza na mtoto kwa upole, kuepuka vitisho au lawama na kumpa uhakika kuwa yuko salama pale anapoeleza anachohisi.

Mtoto anapohisi kusikilizwa na kueleweka, huanza kufunguka polepole. Hapo ndipo mzazi unaweza kuelewa kiini cha tatizo lake, badala ya kumpuuza.

Ukifanya hivyo, itakusaidia kuchukua hatua nyingine muhimu ya kutafuta msaada wa kitaalamu mapema.

Kumuona mtaalamu wa afya ya akili si ishara ya kushindwa kulea, bali ni hatua ya kinga inayoweza kumsaidia mtoto wako kurejea katika hali yake ya kawaida mapema.

Wataalamu pia wanashauri wazazi kuunda mazingira chanya nyumbani kwa kuweka ratiba nzuri ya mtoto kulala, kula chakula na ya muda wa kucheza na kupumzika.

Kwa ujumla, wazazi wanapaswa kutambua kwamba uangalizi wa karibu wa mzazi ni nguzo muhimu katika kulinda afya ya akili ya mtoto.

Kwa sababu dalili zikibainika mapema na hatua stahiki kuchukuliwa, mtoto anayo nafasi kubwa ya kukua akiwa na utulivu wa kihisia na uwezo mzuri wa kujifunza na kuishi kwa kujiamini.