Mgombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Peramiho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Lazaro Komba Bunungu, amechukua rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika jimbo hilo lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Dkt. Bunungu amesema amejiandaa kikamilifu kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Peramiho endapo atapewa ridhaa hiyo na wananchi.
Ameeleza kuwa dhamira yake ni kushirikiana na wananchi katika kuwaletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia sera na mwelekeo wa Chama Cha Mapinduzi.
Aidha, amewashukuru wananchi wa Peramiho kwa sapoti na ushirikiano wao, huku akiwataka kuendelea kudumisha mshikamano na umoja wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Vilevile, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi Taifa kwa imani waliyoonesha kwake kwa kumpa ridhaa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mdogo Peramiho
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Songea Vijijini, Juma Nambaila, amewashukuru viongozi wa CCM kutoka kata zote 16 za jimbo hilo kwa mshikamano wao, akisema hali hiyo ni ishara ya ushindi wa chama hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Februari.
Naye Mwenyekiti wa CCM Songea Vijijini, Thomas Masolwa, amempongeza Dkt. Bunungu kwa kuchukua fomu hiyo, akisema CCM imemuamini kuwa msimamizi wa masuala ya maji, umeme na barabara, pamoja na kuwa sauti ya wananchi wa Peramiho.











