Simba ni rasmi kuwa haina nafasi tena kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kushindwa kulinda mabao 2-0 na kumaliza kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Esperance de Tunis kwenye mchezo wa hatua ya makundi uliopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, leo.
Bado Simba imeendelea kuburuza mkia kwenye kundi ikiwa na pointi moja baada ya mechi nne, Stade Mallien inaongoza na pointi nane, Esperance wanashika nafasi ya pili na pointi sita, huku Pedro akiwa na pointi tano na kila timu imebakiza michezo miwili.
Kocha wa Simba, Steve Barker, aliingia uwanjani akiwa amefanya mabadiliko matatu kwenye kikosi cha kwanza ikilinganishwa na kilichoanza mchezo uliopita dhidi ya Waarabu hao wa Tunisia ambao Simba ililala kwa bao 1-0.
Barker aliwaanzisha wachezaji wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 30, akiwemo Libasse Guaye, Anicet Oura na Clatous Chama.
Katika safu ya ushambuliaji, Barker alimpa jukumu Kibu Denis kuongoza mashambulizi badala ya Jonathan Sowah, tofauti na ilivyokuwa Tunisia ambapo alishambulia akitokea pembeni.
Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu katika dakika 30 za mwanzo, Esperance ikionekana kujaribu kuhimili presha ya Simba kwa kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza.
Hata hivyo, kuanzia dakika 15 za mwisho za kipindi cha kwanza, Simba iliongeza kasi ya mashambulizi na kuanza kuitawala Esperance hasa kupitia maeneo ya pembeni, ambapo Oura na Guaye walikuwa tishio
Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 39, pale Shomary Kapombe alipoiandikia Simba bao la kwanza kwa kichwa baada ya purukushani langoni mwa wapinzani wao.
Dakika sita baadaye, Simba iliongeza bao la pili kupitia Yusuph Kagoma, aliyemalizia kwa kichwa cha chinichini baada ya kazi nzuri ya Chama. Bao hilo liliifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.
Tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza, Esperance ilirejea na nguvu huku ikijaribu kutafuta nafasi za kusawazisha.
Miamba hiyo ilipata bao la kwanza katika dakika ya 64 kupitia Aboubacar Diakité kufuatia presha kubwa ya mashambulizi.
Dakika ya 74, Barker alifanya mabadiliko matatu kwa mpigo kwa kuwatoa Kibu, Guaye na Kante huku wakiingia Seleman Mwalimu, Morice Abraham na Ellie Mpanzu.
Licha ya mabadiliko hayo, Esperance iliendelea kucheza kwa utulivu huku icheza kwa kustuka kwa kutupa mipira nyuma ya ukuta wa Simba kutokana na kasi ya washambuliaji wao.
Hesabu hizo zilijipa dakika ya 79 kupitia Boualia ambaye aliwahadaa mabeki wa Simba na kuachia mkwaju ambao ulimshinda Kassali na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Hata hivyo dakika ya 90, wageni hao walikosa mkwaju wa penalti baada ya Hamza Jellas kupiga mkwaju mkali uliopaa juu ya lango.
Tofauti na ilivyokuwa katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Simba ilionekana kupoteza muundo wake katika kujilinda baada ya Esparance kuamua kufunguka kufuatia kuwa nyuma kwa mabao 2-0.
Wakati ambao Simba ilikuwa ikijaribu kuimaliza mechi kwa kusaka bao la tatu, timu ilionekana kuwa wazi eneo la nyuma kitu ambacho kwa Esperance ilikuwa faida.
Licha ya uwepo wa Kagoma na Kante huku nyuma kukiwa na De Reuck na Nangu bado haikuwa imara na kuacha Esperance kuwa huru karibu na eneo lao.
Katika dakika 45 za kipindi cha pili, Esparance ilifika mara nyingi kwa Simba na kupiga mashuti sita huku matatu yakilenga lango, Simba ilipiga moja tu.
Hata hivyo, Esperance ilikuwa na nafasi ya kumaliza mechi katika dakika za lala salama lakini walipoteza mkwaju wa penalti na kufanya mechi hiyo imalizike kwa sare ya mabao 2-2.
Simba SC: Kassali; Kante, Kapombe (C), Oura, Kagoma; De Reuck, Chama, Gueye; Nangu, Kibabage, Kibu. (Akiba: Abel, Duchu, Sowah, Toure, Naby, Morice, Mwalimu, Loemba, Mpanzu.)
Esperance Sportive de Tunis: Ben Said; Keita, Laifi, Jelassi, B. Hmida (C), Konaté, Onuche, Tka; Yan Sasse, Diakité, Diarra. (Akiba: Mechiche, Guemichi, Florent, Msakni, Rafa, Kouceila, Jebali, Jabri.)