Fumbo wanawake kuvutiwa na wenye ‘vitambi’

Tofauti na ilivyozoeleka kuwa wanawake wanapenda wanaume wenye miil yenye misuli maarufu ‘six-pack’, baadhi ya kazi za kitafiti zinaonesha siku hizi wanawake hawahangaiki na wanaume wa aina hiyo.

Badala yake, macho yao yanakwenda kwa yule mwanaume wa kawaida mwenye kitambi kidogo, mwili wa kati na chakula chake huwezi amini ni ugali!

Huyu si mwanaume anayejianika Instagram, wala si bingwa wa kwenda vituo vya mazoezi. Ni mwanaume wa mtaani, wa kazini, wa vijiweni na cha kushangaza, wanawake wengi wanamuona huyu kuwa na mvuto zaidi.

Ukikaa vijiweni, utaona jamaa mwenye tumbo kubwa kidogo ndiye mwenye mwanamke mzuri, si yule aliyekaza mwili kama jiwe. Wengine watasema ni bahati, lakini ukweli ni kwamba kuna sababu.

Mabadiliko haya ya mtazamo yamezua mjadala mpana, yakivunja dhana kwamba mvuto wa mwanaume hupimwa kwa misuli pekee.

Utafiti uliofanywa mwaka 2017 na Planet Fitness nchini Marekani uligundua kuwa wanawake wengi walioulizwa waliwaona wanaume wenye vitambi, kuwa wanajiamini na kujikubali walivyo, hali ambayo inakuwa ishara ya mvuto wa kihisia na kimaendeleo.

Zaidi ya hayo, takriban nusu ya wanawake walisema kuwa wanaume wenye kitambi kwa mbali ni kama ‘six-pack’ mpya, huku kinamama wengi wakisema kuwa wangefurahia kuwa na mume mwenye mwili wa aina hiyo.

Utafiti mwingine wa mtandao wa Dating.com wa mwaka 2021 ulionyesha kuwa karibu asilimia 75 ya watu wasio kwenye uhusiano walipendelea mwanaume mwenye mwili wa kawaida kuliko yule aliyekaza sana misuli.

Matokeo haya yanathibitisha kuwa mvuto wa mwanaume hauzingatii tu mwili wa nje, bali pia unahusiana na sifa zinazodhaniwa kuambatana na mwili huo.

Wataalamu wa saikolojia ya jamii wanasema kuwa wanaume wenye miili iliyokakamaa sana mara nyingi huonekana kuwa na ushindani mkubwa, wanapenda kuonekana, na wana msukumo wa kuthibitisha uanaume wao.

Mtazamo huo mara nyingine huwapunguzia mvuto kwa wanawake wanaotafuta uhusiano wa kudumu, kwa sababu wanaona wanaume hao wanaweza kuwa wakali, wenye tabia zisizo thabiti, au hatari kwa uhusiano wa muda mrefu.

Kwa upande mwingine, mwanaume mwenye kitambi kidogo huonekana kama mtu mtulivu, mkomavu kihisia, mwenye maadili mema, anayejali na mwenye uwezo wa kulea familia.

Mtazamo huu unachangia kwa kiasi kikubwa mvuto wa mwanaume wa aina hiyo, hususani pale wanawake wanapokuwa wanatafuta wenza wa kudumu na si wa muda mfupi.

Mtaalamu na Profesa wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Bucknell nchini Marekani, Joel Wade anasema tafiti zinaonyesha kuwa wanaume wenye mvuto mkubwa sana wa kimwili mara nyingi huwa na sifa ambazo wanawake huziona kuwa hazifai kwa uhusiano wa muda mrefu.

“Kwa mfano, wanaume wenye mvuto wa hali ya juu wana uwezekano mkubwa wa kutokuwa waaminifu. Bila shaka, watu wenye mvuto mkubwa hupata fursa nyingi zaidi za kufanya usaliti,”anasema katika tovuti ya Psychology Today

Anaongeza: “Hata hivyo pia inahusiana na kiwango cha homoni ya testosterone (inayozalishwa kwa wingi kwenye korodani) aliyonayo mwanaume, kwani testosterone huongeza hamu ya ngono. Wanaume wenye kiwango cha juu cha testosterone huwa na uwezekano mkubwa wa kusaliti.”

Anasema wanawake wanaweza kuvutiwa zaidi na mwanaume wanayemdhania kuwa na kiwango cha chini cha testosterone na wengi wenye kiwango kidogo ni wenye vitambi, kwa sababu huonekana kuwa mtulivu zaidi, mpole, na mwenye sifa za kuwa mwenza mzuri na baba bora.

Ingawa mwanaume mwenye six-pack na mwili wa kujichora anaweza kuvutia kwa macho, utafiti mwingi unaonyesha kuwa wanawake mara nyingi hupendelea mwanaume anayeshikilia sifa zinazofaa kwa uhusiano wa kudumu.

Mtaalamu wa uhusiano, Adela Martini anasema kwa wanawake, mwanaume mwenye kitambi hutoa hisia ya usalama, utulivu, na uwiano wa kihisia, hali inayoongeza mvuto wake kwenye uhusiano wa muda mrefu.

Anasema pia, baadhi ya wanawake hupendelea mwanaume mwenye nyama nyama kulinganisha na mwenye misuli sana.

 “Kuna wanawake wanapenda hata wakikumbatia waume zao wasiumizwe na mifupa bali wakutane na nyama,”anasema.

Anasema mwili wa kawaida au wenye kitambi cha wastani unatoa faraja kwa wanawake zaidi kuliko miili iliyochongwa sana.

 Wanawake wengi wanajihisi huru pale mwanaume anapokuwa wa kawaida, asiye na presha ya kujionyesha au kuonesha uanaume wake kila mara na unaotoa ishara ya kuwa tayari kwa uhusiano wa kudumu, ikimaanisha kwamba mwanaume huyo anaweza kuwa mume na baba bora.

“Ni kweli kuna baadhi yetu huvutiwa na wanaume wenye vitambi lakini vya wastani sio tumbo kubwa sana. Hii ni kwakuwa inahakikisha kuwa huo ndiyo mwonekano wake halisi,”anasema Siwema Rajabu mkazi wa jijini Mwanza.

Anasema mwanaume wa aina hiyo hana mambo mengi hasa yanayomuweka ‘ bize’ kuhangaikia mu

mwonekano wake bali atakuwa anashugulika na masuala ya familia yake na kuhakikisha inastawi.

“Ukikuta mwanamke anachagua kuwa mimi nataka mwanaume mwenye umbo la kuvutia asiye na kitambi basi jua huyo siyo mume wake, huyo ni mwanaume wa maonesho si wa kujenga naye familia,”anaongeza.

Kauli ya Siwema inaungwa mkono na Anitha Jerome anayesema ni hatari sana mwanamke kuvutiwa na mwanaume mwenye mvuto wa mwili, kwakuwa mabadiliko yanaweza kutokea muda wowote ndani ya uhusiano.

“Sawa umevutiwa na six pack na umeanzisha naye uhusiano…siku akiacha kwenda huko gym anapojenga misuli yake kutokana na utafutaji akarudi kwenye umbo la mwili lisiloeleweka utamuacha? Jibu hapana! Kwahiyo binafsi navutiwa na mwanaume mwenye mwili wake halisi…kwanza wenye vitambi hawana mambo mengi,”anasema.

Akizungumzia kuhusu wanawake kupenda wanaume wenye vitambi, Samwel Gerlad anasema hawezi kubishana na utafiti na kuwa anavyoamini siku zote wanawake hupenda na kutamani vitu visivyo na uhalisia.

“Kama wangekuwa wanapenda vitambi mbona wanachanganywa na wanaume wanaoshinda gym? Labda uniambie kuwa wanaume wenye vitambi hawana mambo mengi hivyo baadhi ya wanawake wanaona bora waanzishe nao uhusiano tena wa kudumu, yaani mume na mke…tofauti na hawa wenye matumbo flati na vifua vikubwa kwani ni ndoto ya kinadada wengi,”anasema.

Anaongeza: Mwanamke akikwambia bora kitu fulani kuliko hiki anza kuchunguza kwanini kasema hivyo kwakuwa wanapenda vitu visivyo na uhalisia, ndio maana si kitu cha ajabu mwanamke kukwambia sina kabisa nguo wakati kabati lake limejaa nguo.”

Anaeleza kuwa kutojiamini kwao ndiko kunafanya wakimbilie wanaume ambao kwa upeo wao wanadhani hawavutii wengi. Wanasahau kuna wenzao wenye akili kama zao kuwa wanaume wa aina hiyo hawavutii hivyo wanajikuta wanachokikwepa (kusalitiwa) wanakutana nacho.

Hata hivyo, wataalamu wanakumbusha kuwa si kila mwanaume mwenye kitambi huwa mvuto kwa wote, afya bado ni jambo muhimu.

Kitambi kikubwa kupita kiasi kinaweza kuashiria changamoto za kiafya, hivyo mvuto wa kimapenzi haupaswi kuamuliwa pekee kwa mwonekano wa nje.