GGML yatajwa chachu ukuaji sekta ya madini

Dar es Salaam. Serikali imeitaja Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kuwa miongoni mwa zilizotoa mchango katika kukuza sekta ya madini nchini kwa kipindi cha miaka 25.

Imeeleza mchango wa kampuni hiyo, umejikita katika ulipaji kodi, utoaji wa ajira, uchimbaji madini unaowajibika na ushiriki wake katika maendeleo ya jamii.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, wakati akizungumza katika hafla ya   kuadhimisha miaka 25 ya GGML iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Amesema historia ya GGML tangu kuanza shughuli zake mwaka 2000 inaonesha wazi kuwa uchimbaji madini unaotekelezwa kwa uwajibikaji unaweza kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Taifa na maendeleo ya wananchi.

“GGML ni mfano hai unaothibitisha kuwa sekta ya madini inaweza kuleta matokeo chanya endapo itatekelezwa kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wawekezaji na jamii,” amesema.

Ameeleza kupitia ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali, uanzishaji wa ajira kwa maelfu ya Watanzania na utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), GGML imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya madini na uchumi kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa (kulia) akioneshwa picha zilizopo ukutani (Wall Museum) zilizokuwa zikimuonesha historia ya Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) kutoka kwa Makamu wa Rais wa kampuni mama ya GGML, AngoGold Ashanti, anayehusika na Uendelevu na Mahusiano barani Afrika, Simon Shayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 25 ya mgodi huo hapa nchini iliyofanyika jijini Dar es Salaam.



Ameongeza kadiri Serikali inavyoendelea kufanya mageuzi katika sekta ya madini, ushirikiano na wawekezaji wanaozingatia misingi ya maendeleo endelevu kama GGML ni muhimu katika kufanikisha malengo ya taifa.

Hafla hiyo, iliwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali, wakuu wa taasisi mbalimbali, wanadiplomasia, viongozi wa sekta binafsi na wadau wa sekta ya madini. Miongoni mwa taasisi zilizohudhuria ni Stanbic Bank, PUMA Energy, Mwananchi Communications Limited na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Sekta ya madini iliwakilishwa na Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania (TCM) kikiongozwa na Katibu Mtendaji wake, Mhandisi Raymond Rweyemamu, pamoja na makandarasi wa migodi na wanachama wa jumuiya ya kidiplomasia.

Maadhimisho hayo yalipambwa na jukwaa maalumu la simulizi lililopewa jina la Stori za Dhahabu, linalokusanya na kuhifadhi uzoefu wa wafanyakazi, makandarasi na wanufaika wa miradi ya jamii iliyotekelezwa na GGML kwa kipindi cha miaka 25.

Katika hafla hiyo, GGML pia ilizindua filamu ya ‘Stori za Dhahabu’ na kitabu cha kumbukumbu kinachoeleza safari ya mgodi huo tangu kuanzishwa kwake hadi sasa.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa GGML na sasa Makamu wa Rais wa Biashara Afrika wa AngloGold Ashanti, Terry Strong amesema GGML ni miongoni mwa migodi inayofanya vizuri zaidi ndani ya kampuni hiyo barani Afrika.