Haya ndiyo maisha mapya ya kidijitali kwa wanavyuo

Dar es Salaam. Vyuo vikuu vya leo si vile vya jana. Ukitembea katika viunga vya vyuo nchini, utaona wazi mabadiliko makubwa ya maisha ya mwanafunzi wa kizazi cha sasa, maarufu kama Generation Z (Gen Z).

Simu janja imekuwa sehemu isiyotenganishwa na maisha ya mwanafunzi wa leo. Karibu wote masikioni wana ‘earphones’ au ‘earpods’, macho yakikodolea skrini, na vidole vikigusa skrini kwa kasi kufuatilia mitandao ya kijamii, ikiwemo ‘challenges’ zinazovuma kwenye TikTok na Instagram.

Kwa Gen Z, simu si kifaa cha mawasiliano tena, bali ni nyenzo ya maisha. Ndani ya madarasa, hutumika kupiga picha za slides, kutafuta ufafanuzi wa dhana mbalimbali kupitia akili unde (AI), au kushiriki mijadala ya kitaaluma kwa kutumia majukwaa ya mtandaoni kama Google Classroom.

Kujifunza kwa Gen Z hakuishii tena ndani ya vitabu vya maktaba pekee, bali kunafanyika papo hapo, kwa kasi na kwa mtindo unaochanganya elimu na burudani. Kwao, simu ni mwendelezo wa fikra za ubongo, kizazi kilichokulia kwenye intaneti hakiwezi kuitenga teknolojia na maisha ya kila siku.

Mbali na darasani, maisha ya wanavyuo wa Gen Z yamejaa challenges za mitandaoni. Kuanzia kucheza, kuigiza, kuimba hadi kampeni za kijamii au pranks zinazovuma kwa muda mfupi, vyuo vimegeuka kuwa majukwaa ya uundaji wa maudhui ya kidijitali.

Katika baadhi ya matukio, hata madarasa yamekuwa sehemu za kurekodia maudhui, ikiwa ni njia ya kujitambulisha, kujenga jina mtandaoni na wakati mwingine kupata kipato kupitia content creation.

Si jambo la kushangaza tena kumuona mwanachuo akitengeneza video inayoonesha changamoto za maisha ya chuo anapokuwa hana fedha, kisha baadaye akarekodi video nyingine akionesha furaha baada ya kupata pesa maudhui yanayopata mvuto mkubwa mitandaoni.

Hali hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa na maisha ya wanafunzi wa vizazi vilivyotangulia, ambavyo vilijikita zaidi katika kusoma vitabu maktabani na kuiona elimu ya chuo kikuu kama ngazi ya kupata ajira rasmi.

Kwa Gen Z, mtazamo huo umebadilika. Chuo si tu maandalizi ya ajira ya kudumu, bali ni jukwaa la fursa nyingi, ikiwemo ujasiriamali wa kidijitali, kazi za mtandaoni na hata kujenga umaarufu kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kuhitimu masomo.

Kwa vyovyote vile, jambo moja ni wazi: Gen Z hawasomi kwa mtindo wa zamani. Maisha yao ya chuo ni kielelezo cha dunia inayobadilika kwa kasi, ambapo elimu, teknolojia na utamaduni vinaingiliana kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati akipokea tuzo kwa mchango wake katika kukuza lugha ya Kiswahili iliyotolewa na Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili (Chalufakita), mhadhiri na aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala, amesema vijana wa sasa ni tofauti na wale wa zamani.

Amesema tofauti hiyo inaonekana hata katika utayari na umakini wa wanafunzi darasani, akieleza kuwa baadhi yao hujihusisha na simu hata wakati wa masomo.

“Mwanafunzi anaweza kuwa darasani akiwa na simu pajani, anachati. Ukimuuliza swali, anasema hajasikia,” amesema Profesa Mukandala.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Rachel Lucas, amesema kushiriki challenges na kutengeneza maudhui ni sehemu ya maisha ya sasa kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia.

“Teknolojia imebadilika. Siku hizi kila kitu ni mtandaoni. Madhara sijaona moja kwa moja, inategemea na maudhui unayofanya, kama yanafaa kwa jamii au yanatoa funzo. Wengine hufanya kwa ajili ya kujifurahisha tu,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano, amesema kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia imeongeza matumizi ya mitandao ya kijamii na mifumo mingine ya kidijitali duniani kote.

Amesema licha ya changamoto zinazojitokeza, mitandao ya kijamii inaleta fursa nyingi kwa vijana, ikiwemo kujifunza, kujenga ujuzi na kunufaika kiuchumi.

“Kikubwa ni mtumiaji kujitambua, kuzingatia mipaka na kutumia mitandao kwa namna inayojenga, kielimu na kiuchumi,” amesema.

Naye Sebastian Mathew, aliyemaliza chuo miaka ya 2010, amesema mabadiliko hayo yanatokana na teknolojia iliyobadili mfumo mzima wa maisha.

“Zamani hatukuwa na TikTok wala X, hivyo hatukuwa na mazingira ya kufanya haya. Lakini sasa wanavyuo kutengeneza maudhui na kuyaweka mtandaoni ni jambo la kawaida, kwa sababu ni sehemu ya maisha ya sasa,” amesema.