Arusha. Mahakama Kuu, imeiamuru kampuni ya Lodhia Steel Industries Ltd na dereva wake, Abdalah Mbugu, kuilipa kampuni ya Leopard Tours Limited, fidia ya Sh270 milioni kutokana na madhara ya ajali iliyosababishwa na Mbugu.
Awali katika madai yake kupitia shauri hilo la madai namba 28359 la mwaka 2023, lililofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kampuni hiyo iliomba ilipwe fidia maalum na fidia ya jumla ya zaidi ya Sh1.7 bilioni kutokana na athari za ajali hiyo.
Katika hukumu yake aliyoitoa Januari 30,2026, Jaji Frank Mahimbali alisema mwajiri anawajibika kisheria (vicariously liable) kwa matendo ya mwajiriwa yaliyofanywa wakati wa ajira, hivyo wote wawili wanawajibika kulipa fidia hiyo.
Leopard Tours Limited walifungua kesi hiyo dhidi ya kampuni ya Lodhia Steel Industries Limited kama mdaiwa wa kwanza, Mbugu au Abdalah Mohamed Kituru kama mdaiwa wa pili na mdaiwa wa tatu, kampuni ya Bima ya Meticulous General.
Kulingana na hati ya madai, Juni 16,2023 eneo la Kambi ya Mkaa, Kikatiti katika barabara Kuu ya Moshi-Arusha, gari la Lodhia Steel Industries likiendeshwa kwa uzembe na mwajiriwa wao, liligongana uso kwa uso na gari la Leopard Tours.
Kutokana na ajali hiyo, kampuni ya Leopard Tours ikaiomba mahakama iwaamuru wadaiwa, kuilipa fidia kutokana na madhara waliyoyapata wakati gari lao Toyota Landcruiser lilipogongana na lori Mitsubish Fuso.
Hivyo kampuni ya Leopard Tours wakaomba walipwe fidia maalum na fidia ya jumla inayofikia Sh1.75 bilioni, riba ya fedha hizo pamoja na gharama za kesi hiyo ambapo mdaiwa wa kwanza na wa pili walikataa kuwajibika kulipa fidia hiyo.
Mdaiwa wa tatu, kampuni ya bima ilipinga fidia chini ya mkataba wa bima.
Kwa makubaliano ya mdai na wadaiwa, walikubaliana hoja za kuamuliwa na mahakama ambazo ni pamoja na kama Mbugu alikuwa ni mzembe hadi kusababisha ajali na pili kama pia alikuwa ni dereva wa kampuni ya Lodhia.
Hoja nyingine ya ilikuwa ni kama mdai katika shauri hilo alipata hasara kutokana na ajali hiyo, kama kulikuwa na mkataba wa bima kati ya mdai na mdaiwa wa tatu ni kwa kiasi gani kampuni ya bima inapaswa kuifidia kampuni ya Lodhia.
Katika shauri hilo, kampuni ya Leopard Tours iliwakilishwa kortini na wakili Patricia Erick wakati mdaiwa wa kwanza na wa pili waliwakilishwa kortini na wakili Nafikile Mwamboma, na mdaiwa wa tatu akiwakilishwa na wakili Philip Mushi.
Jaji alisema mashahidi wa upande wa wadaiwa katika shauri hilo walijaribu kushambulia uhusiano wa mwajiri na mwajiriwa hisia za hasara wakati mdai ana ushahidi thabiti wa uzembe, majeraha, na uharibifu wa kifedha wa haraka.
“Kwa kuangalia madai ya nafuu zinazoombwa inaonyesha kuwa mdai alipata hasara maalumu na hasara ya jumla zilizoorodheshwa katika hati yake ya madai. Kanuni zinazoongoza utoaji wa fidia ya uharibifu si ngeni, ” alisema Jaji.
Jaji Mahimbali alisema baada ya kuupitia kwa makini ushahidi na misingi ya kisheria, alisema kuhusu kama dereva Mbugu alikuwa mzembe, shahidi wa kwanza ambaye ni dereva wa gari la kampuni ya Leopard Tours alieleza kwa kina.
Dereva huyo alitoa ushuhuda wa kuona namna mdaiwa wa pili wakati akiendesha lori la mdaiwa wa kwanza, alipuuza alama za barabarani na kuendeshwa kwa uzembe na kusababisha lori alilokuwa akiendesha kugongana naye uso kwa uso.
“Mdaiwa wa pili aliyekuwa shahidi wa kwanza kwa mdaiwa alikana kuendesha kwa uzembe, akilaumu mafundi wanaotengeneza barabara lakini akakiri kutiwa hatiani katika kesi ya trafiki. Kukataa kwake kunapingana na kesi hiyo,”alisema.
Mahusiano ya mwajiri, mwajiriwa
Kuhusu hoja ya mahusiano ya ajira kati ya mdaiwa wa pili (Mbugu) na mwajiri wake (kampuni ya Lodhia), shahidi wa pili wa mdai ambaye ni Ofisa Rasilimali Watu (HR) wa Leopard Tours alitoa vielelezo vinavyoonyesha mahusiano hayo.
Miongoni mwa nyaraka alizozitoa mahakamani kama kielelezo ni pamoja na michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na katika mahojiano ya dodoso, mdaiwa wa pili alikiri kuwa ni kweli ni mwajiriwa wa kampuni ya Lodhia.
Jaji alisema shahidi wa pili wa wadaiwa ambaye HR wa kampuni ya Lodhia alijikanganya mwenyewe katika ushahidi wake, kuna wakati anakubali kumwidhinisha na kuna wakati anakataa uwepo wa mkataba baina yao.
“Kwa kuzingatia mizania ya ushahidi, ninaona mdaiwa wa pili alikuwa mwajiriwa wa mdaiwa wa kwanza na alikuwa akitenda kazi ndani ya wigo wa ajira yake. Hivyo, dhana ya wajibu wa mwajiri inafanya uwajibikaji uhamishiwe kwake,”alisema Jaji.
Fidia ya madhara ya uharibifu
Kuhusu hoja ya uharibifu, Jaji Mahimbali alisema shahidi namba tatu wa mdai ambaye ni Meneja wa Fedha, alitoa vielelezo ambavyo ni bili za matibabu, Ankara za hoteli, gharama za kuvua gari na makadirio ya gharama za kutengeneza gari.
“Nyaraka hizi zinaeleza kikamilifu jinsi mdai anavyothibitisha uharibifu au hasara, faida iliyopotea na biashara, pamoja na gharama za papo hapo,”alisema Jaji na kuongeza kuwa hoja ya wageni kusitisha safari iliegemea katika makadirio.
“Makadirio hayo hayakufanyiwa ukaguzi au rekodi za benki. Madai ya aina hiyo yanaweza kuwa ya juu au yakawa ni hisia (speculative). Nyaraka zinathibitisha madhara halisi lakini naona faida iliyotarajiwa imeongezewa chumvi.”
“Hivyo ninaona ni kweli mdai alipata hasara lakini zile zinazoweza kuthibitishwa,”alisema.
Kuhusu iwapo kulikuwa na mkataba wa bima kati ya mdaiwa wa kwanza na mdaiwa wa tatu, Jaji alisema imethibitika ulikuwepo mkataba huo.
“Kuhusu ni kiasi gani mdaiwa wa tatu anabeba mzigo katika madai haya, Jaji alisema bima ilikuwa inahusu madhara ya mwili na mali ambayo yamesababishwa na madereva walioidhinishwa na shahidi wa pili wa mdaiwa alikiri hilo,”alisema.
“Hivyo basi, bima inawajibika kufidia mdaiwa wa kwanza kwa majeraha ya mwili kwa abiria na uharibifu wa mali kwa gari la mdai katika shauri hili,”alieleza Jaji.
Hata hivyo Jaji alisema, Sera hii haijumuishi hasara za pembeni kama vile kusitishwa kwa biashara na uharibifu wa sifa kwa hivyo, anaona kuwa bima inawajibika tu ndani ya wigo wa uharibifu wa kimwili na wa mali.
Ni fidia kiasi gani ilipwe
Jaji katika uamuzi wake, hukumu yake imetolewa kwa niaba ya mdai dhidi ya mdaiwa wa kwanza na wa pili kwa pamoja na kila mmoja peke yake hivyo mdai wanapewa tuzo ya kurejeshewa bili za matibabu zinazofikia Sh2 milioni.
Pia anapewa tuzo ya kulipwa gharama za malazi Sh1.68 milioni, tuzo ya kurejesha pesa kwa Kobo Safaris Sh6.6 milioni, gharama za kuvuta gari Sh400,000, utengenezaji wa gari Sh164 milioni na gharama nyingine.
Mbali na tuzo hiyo, mahakama imewaamuru wadaiwa kulipa Sh50 milioni za uharibifu wa sifa na usumbufu, hasara iliyotokana na gari kusimama kwa miezi sita Sh25 milioni, gharama za kesi na kampuni ya bima kulipa madhara ya kimwili.
Fidia yote hiyo inafikia Sh270.4 milioni bila kujumlisha gharama za kesi.