Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, leo Februari 1, 2026 amezindua rasmi mashindano makubwa ya usomaji wa Qurani ya mabara yote yanayofanyika nchini Tanzania kila mwaka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Abdulla amewashukuru viongozi wa kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kulinda amani ya nchi, akisema ndiyo msingi mkubwa wa mafanikio ya mashindano hayo.
Amesema Tanzania kuendelea kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa kipindi cha miaka 26 mfululizo ni matokeo ya utulivu na mshikamano uliopo, hali inayoiwezesha nchi kuaminika kimataifa katika masuala ya dini na amani.
Aidha, amewataka wakazi wa Dar es Salaam, Zanzibar na mikoa mingine nchini kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, ili kuwaunga mkono vijana kutoka mabara mbalimbali wanaoshindana katika kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mashindano hayo yanayoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdeen Kishki, amesema mashindano yatafanyika Machi 1, 2026 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Mwinyi.
Sheikh Kishki amesema mshindi wa kwanza wa mwaka huu atapata zawadi ya shilingi milioni 30, fedha zinazodhaminiwa na mdhamini mkuu wa mashindano hayo, PBZ Bank Ikhlas.
Ametaja baadhi ya nchi zitakazoshiriki kuwa ni Canada, Mexico, Barbados, Guyana, Sweden, Ujerumani, Uingereza, New Zealand, Australia, Indonesia na Kazakhstan, huku Bara la Afrika likiwakilishwa na nchi mbalimbali ikiwemo Zambia, Uganda, Kenya na Reunion.
Akizungumza kwa nyakati tofauti, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar na Mjumbe wa Hay’atul Ulamaa Tanzania, Sheikh Twaha Suleiman Bane, wameipongeza Al-Hikma Foundation, wakisisitiza kuwa mashindano hayo ni fursa muhimu kwa jamii kurejea katika maadili, uadilifu na mwongozo wa Qurani.
.webp)