Mwigulu: Serikali kushirikiana na sekta binafsi kukuza utalii

Arusha. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza mipango na mikakati ya kuimarisha sekta ya utalii, ikiwemo kuboresha mazingira ya uwekezaji ili sekta hiyo ichangie kikamilifu maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya utalii inanufaisha wadau wote, kuanzia watoa huduma, wawekezaji hadi jamii zinazozunguka maeneo ya utalii, huku ikiongeza ushiriki wa wananchi kama nguzo muhimu ya kupunguza migogoro, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za asili na kuhakikisha maendeleo jumuishi.

Dk Mwigulu ameyasema hayo usiku wa Januari 31, 2026, jijini Arusha, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Kitaifa za Uhifadhi na Utalii, maarufu,Serengeti Awards.

Akizungumza katika hafla hiyo, amesema Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya maliasili na utalii kwa kushirikiana na sekta binafsi, hususan katika kuboresha miundombinu muhimu ikiwemo ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege, kuanzishwa kwa njia mpya za ndege pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa.

Amesema hatua hizo zimefungua fursa mpya za utalii katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Morogoro, na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, sekta ya utalii inachangia asilimia 21 ya pato la Taifa, ambapo asilimia 17 inatokana na shughuli za utalii na asilimia nne kutoka sekta za misitu na ufugaji nyuki. Ameongeza kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2023, idadi ya watalii wa kimataifa ilifikia zaidi ya milioni 2.09, sawa na ongezeko la asilimia 9.02 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

“Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa na ustawi wa jamii. Hii ni pamoja na kuwezesha uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuimarisha utalii na kuongeza ajira, kipato pamoja na fursa za kiuchumi kwa wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mikakati itakayohakikisha sekta hiyo inanufaisha wadau wote, jambo litakalosaidia kulinda maliasili, kukuza utalii na kuhakikisha fursa za kiuchumi zinagawanywa kwa haki na tija.

Aidha, ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na wadau kuwekeza katika ubunifu, kuboresha ubora wa huduma na matumizi ya teknolojia ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la utalii. Kwa sasa, sekta hiyo inatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa zaidi ya watu milioni tatu.

Akizungumzia Tuzo za Serengeti, Dk Mwigulu amesema tangu zilipozinduliwa Desemba 2024, zaidi ya tuzo 56 zimekuwa za ushindani, hali inayoonesha mchango mkubwa wa sekta binafsi katika uhifadhi wa maliasili, uendelezaji wa utalii wa kitaifa na kimataifa pamoja na uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa utalii.

“Sekta ya utalii hutoa fursa nyingi za uwekezaji kuanzia hoteli, usafiri, uwakilishi wa utalii hadi uendelezaji wa vivutio vya asili. Fursa hizi zinachangia moja kwa moja kuongeza pato la Taifa na kukuza biashara ndani na nje ya nchi,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema mafanikio ya sekta ya utalii yanatokana na mchango wa Serikali katika kutafuta rasilimali fedha zilizosaidia shughuli za uhifadhi, kuboresha miundombinu ya utalii na kutangaza vivutio vilivyopo nchini.

Amesema filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo, huku mwaka 2025 Tanzania, kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, ikifanikiwa kushinda tuzo 18 za kimataifa.

Dk Kijaji amesema wadau wa sekta binafsi wamekuwa miongoni mwa walioshinda tuzo hizo, hali inayoendelea kuthibitisha kuwa Tanzania inajiimarisha kama kitovu cha utalii chenye hadhi ya kimataifa.

“Haya yote yamewezekana kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi. Serikali itaendelea kuipa sekta binafsi kipaumbele na kuwapa nafasi wadau kuchangia katika ujenzi wa uchumi endelevu wa Taifa,” amesema.

Ameongeza kuwa kupitia tuzo za Serengeti, Wizara imelenga kuhamasisha ubora, uwajibikaji na ushiriki mpana wa wadau katika kulinda rasilimali za asili, huku tuzo hizo zikiendelea kutolewa kila mwaka kwa lengo la kuhimiza ubunifu, ushindani chanya na viwango vya juu vya huduma katika sekta za uhifadhi na utalii.

Katika hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo maalumu ya Visionary Leadership kwa mchango wake mkubwa katika kukuza utalii na uhifadhi wa maliasili, hususani kupitia filamu za ‘The Royal Tour’ na ‘Amazing Tanzania’.