Profesa Mbarawa asisitiza ukaguzi njia za reli, usalama wa abiria

Dodoma. Serikali imeuagiza uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kusimamisha safari za treni kwa muda pale wanapojenga mashaka ya miundombinu.

Wito huo umetolewa leo Jumapili Februari Mosi, 2026 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 tangu aingie madarakani.

Profesa Mbarawa alikuwa akijibu swali kuhusu kauli ya Serikali jinsi ilivyojipanga kupambana na changamoto za kusimama kwa safari za treni wakati wa mvua kama ilivyotokea hivi karibuni.

Waziri amesema miundombinu ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) imebuniwa kwa teknolojia ya hali ya juu lakini suala la kusimama kwa usafiri lipo mataifa yote.

“Tena nawaagiza wenzetu wa TRC, hakikisheni mnaangalia usalama wa abiria kwanza, wakati wote mkiona kuna mashaka muhimu, mkakague kwanza maeneo yenye mashaka na hapo safari zitabidi kusimama kwanza,” amesema Profesa Mbarawa.

Akizungumzia sababu za msongamano wa watu na mfumo wa ukataji wa tiketi wakati wa safari kwamba umetokana na mapokeo chanya ya wananchi, jambo ambalo linaifanya Serikali ione namna ya kuboresha ikiwemo kuongeza idadi ya mabehewa.

Wakati huo huo,  Tume ya Mipango ipo hatua za mwisho kukamilisha mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji na tathmini (National Project Management Information System -NPMIS).

Mfumo huo unalenga kupeleka mageuzi ya ufuatiliaji unaozingatia zaidi matokeo ya kazi na uwajibikaji ambao utaanza kutumika sambamba na utekelezaji wa Dira 20250 ifikapo Juni 2026.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Fred Msemwa alipokuwa akitoa  taarifa kwa niaba ya Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Dira 2050 ambapo Serikali kupitia NPC ameendelea na maandalizi ya nyenzo kuu tatu.

Nyenzo hizo ni kukamilisha maandalizi ya mpango elekezi wa muda mrefu, kukamilisha kuandika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/27 na kukamilisha mpango wa nne wa maendeleo wa miaka mitano.

Kesho Jumatatu Februari 2, 2026 Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo atawasilisha mipango hiyo bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na baadaye Bunge litafanya uamuzi.