MSHAMBULIAJI wa Kitanzania anayekipiga IFC Malaysia, Said Khamis ‘Said Jr’ amesema amebakiza mabao saba kufikisha malengo aliyojiwekea msimu huu.
Chama la Mtanzania huyo liko nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi na pointi 15, imecheza mechi 14 ikishinda nne, sare tatu na kupoteza mechi saba.
Akizungumza na Mwanaspoti Said Jr amesema malengo yake msimu huu ni kuweka kambani mabao 20 na hadi sasa anayo 13.
Said Jr aliongeza kuwa anataka kuwa mfano bora kwa wachezaji vijana wa Kitanzania wanaocheza soka nje ya nchi kuwa ni inawezekana kufikia malengo.
“Malengo yangu ni kufunga mabao 20 msimu huu na hadi sasa nimeshafunga 13 bado saba tu, naamini nitafikia lengo langu na kwa timu angalau tumalize nafasi ya nne kwa sababu ndio lengo letu,” amesema Said Jr.
Zimesalia raundi 12 kumalizika kwa ligi hiyo na kama Said Jr ataendelea kufunga huenda akafikisha idadi hiyo.
Huu ni msimu wa kwanza kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Mbao FC na kabla aliwahi kukipiga Hatta Club ya Ligi Daraja la kwanza ya Dubai na Bani Yas za Falme za Kiarabu.
Said Jr alikuwa nje ya uwanja kwa takribani nusu msimu na alijiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Malaysia marufu Liga Super Malaysia akitokea FK Jedinstvo UB ya Serbia aliyoitumikia kwa msimu mmoja wa 2023/24.