ALIYEKUWA kocha wa Alliance Girls, Sultan Juma amesema ameondoka kikosini hapo kwa heshima akiiacha timu hiyo ikiwa nafasi nzuri ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Juma alikuwa kikosini hapo tangu mwishoni mwa msimu uliopita akiisaidia kubaki ligi kuu na kumaliza nafasi ya nane kwenye msimamo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Juma amesema amefanya uamuzi huo baada ya maelewano ya pande zote mbili kati yake na Alliance ambayo bado ilikuwa inahitaji huduma yake.
Aliongeza sababu iliyomfanya asiendelee kuitumikia timu hiyo ni pamoja na masilahi kwani alihitaji ofa ambayo Alliance hawakukubaliana nayo.
KOCHA
“Nimeondoka na rekodi nzuri kwanza nimeiacha timu ikiwa nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, kwa hiyo sio kwamba nimeachana nao kwa ubaya hapana, mkataba wangu ulipoisha tukakaa kuzungumza juu ya pesa ambayo nilikuwa naitaka wakasema hawana,” amesema Juma na kuongeza;
“Kwa hiyo tutakubaliana mimi naondoka. Tunafanya kazi ili tupate masilahi walau kidogo, soka la wanawake bado linahitaji kushikwa mkono sababu timu hazina fedha za kutosha.”
Alliance Girls kwa sasa wapo katika mchakato wa mwisho kumpata mrithi wa kocha huyo kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo.