Waziri Sangu awataka PSSSF kujiandaa Dira 2050, kuwasikiliza wafanyakazi

Kibaha. Watumishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wametakiwa kujipanga kuanza safari ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kuanzia Julai mwaka huu.

Sambamba na hilo, mfuko huo umepongezwa kwa kuvuka lengo la makusanyo ya michango kutoka lengo la kukusanya Sh1.1 trilioni hadi kufikia Sh1.2 trilioni katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025.

Hayo yamebainishwa jana, Jumamosi Januari 31, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi na Mahusiano, Deus Sangu, wakati akizindua Baraza la Tatu la Wafanyakazi la PSSSF katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, mjini Kibaha mkoani Pwani.

“Jambo kubwa lililoelekezwa kwenye Dira 2050 ni kukuza uchumi na kuzalisha ajira. Tuhakikishe fedha tunazowekeza zinaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na pili ziwe ni miradi inayoweza kuzalisha ajira kwa vijana,” amesema.

Amesema jukumu la wafanyakazi ni kuwa wazalendo, kujituma na kutanguliza masilahi ya taifa mbele.

Amesisitiza menejimenti ya mfuko kuwapa nafasi wafanyakazi kueleza changamoto zao kwa uwazi ili kuimarisha utendaji kazi na kupata suluhu ya changamoto wanazokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).



“Kwa upande wa wafanyakazi, nipende kuwakumbusha kuwa Serikali inakemea uzembe, vitendo vya rushwa na majungu mahala pa kazi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, amesema baraza hilo limeundwa ili kupanua wigo wa ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi yanayohusu utumishi wao na kwa lengo la kuleta ufanisi mahala pa kazi.

Baraza hilo limeundwa kwa kuijumuisha menejimenti ya mfuko, wawakilishi wa wafanyakazi kutoka kila kanda, kurugenzi na vitengo, wajumbe kutoka Chama cha Wafanyakazi cha TUICO chenye wanachama wengi (378) na wajumbe kutoka Chama cha Wafanyakazi cha TALGWU chenye wanachama wachache (48) ndani ya mfuko.

“Moja ya mambo yaliyojadiliwa jana katika kikao cha baraza hili ni taarifa ya utendaji kwa nusu mwaka Julai hadi Desemba 2025, ambapo mambo yaliyofanyika vyema ni kukusanya michango ya Sh1,272.74 bilioni, ambayo ni utekelezaji wa asilimia 110 ikilinganishwa na malengo ya Sh1,154.01 bilioni.

“Ulipaji wa mafao ni kiasi cha Sh883.26 bilioni, ambayo ni asilimia 99.36 ikilinganishwa na malengo ya kulipa Sh888.96 bilioni, na uwekezaji uliofanywa ni Sh965.37 bilioni, ambao ni asilimia 113 ikilinganishwa na malengo ya kuwekeza Sh854.51 bilioni. Pia Mfuko ulipata hati safi ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2023/24,” amesema.

Amesema mfuko ulisajili wanachama wapya 21,792, ambao ni asilimia 78 ikilinganishwa na malengo ya kusajili wanachama 27,812, hali iliyotokana na idadi ya walioajiriwa kwenye sekta ya umma kwa kipindi hicho.

Amesema baraza hilo ni la tatu tangu kuanzishwa kwa mfuko Agosti 2018, ambapo baraza la pili lililomaliza muda wake limefanya kazi kwa mafanikio makubwa.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wakimshangilia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu (hayupo pichani) alipoingia ukumbini katika tukio la uzinduzi wa Baraza hilo juzi, kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani.



Pamoja na mambo mengine, baraza hilo lilijadili na kushauri upitishwaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2022/23, 2023/24, 2024/25 na 2025/26, mipango yote ikiwa inalenga kutekeleza malengo na majukumu yaliyoelezwa kwenye Mpango Mkakati wa Mfuko wa miaka mitano (2022/23–2026/27) ulioboreshwa ili kuendana na Dira ya Taifa.