Uhaba wa miundombinu, wataalamu vikwazo mapambano dhidi ya saratani

Unguja. Licha ya jitihada zinazofanyika na maendeleo yanayopatikana, imeelezwa kuwa Afrika bado inakabiliwa na changamoto kubwa katika usimamizi wa saratani, hasa uhaba wa rasilimali watu na ukosefu wa miundombinu ya kutosha.

Hayo yamebainika leo Februari 2, 2026 katika mkutano wa nusu mwaka wa uratibu wa kikanda wa mradi wa RAF6060-Kuimarisha uwezo wa nchi wanachama katika utambuzi na matibabu ya saratani, Unguja, Zanzibar ukiwa na washiriki zaidi ya 90 kutoka mataifa 33 ya Afrika.

Ofisa wa Usimamizi wa Programu kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Amal Elrefaei amesema jitihada zinafanyika lakini bado saratani bado ni tishio Afrika.

“Bado kuna safari ndefu, changamoto kubwa katika usimamizi wa saratani hasa katika uhaba wa rasimali za kibinadamu na ukosefu wa miundombinu,” amesema.

Hata hivyo, amesema ili kukabiliana na changamoto hizi kwa njia ya kina, IAEA imeongeza jitihada zake za kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia barani Afrika kupitia ujenzi wa uwezo endelevu na maendeleo ya rasilimali za kibinadamu.

“Hii inajumuisha usaidizi kwa ajili ya kuanzishwa kwa programu za uzamili, mitaala iliyoimarishwa, na moduli za e-learning katika radiolojia, fizikia ya matibabu, dawa za nyuklia, matibabu ya mionzi, lishe na sayansi na teknolojia ya nyuklia,” amesema.

Pia, amesema hatua muhimu zimechukuliwa katika kukuza mitandao ya kitaalamu na ushirikiano.

Amesema mkutano huu unatoa fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa uzoefu wa wengine, kwa lengo la kutambua hatua za kina na zinazoweza kutekelezwa ambazo zinaweza kuimarisha ufanisi wa programu na kusababisha maboresho ya kweli katika matokeo ya saratani katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Amal, saratani ni moja ya visababishi vikuu vya vifo barani Afrika akitaja Ripoti ya Globocan Cancer Observatory ya mwaka 2022 iliripoti kuwa watu 763,000 walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na saratani na wagonjwa mpya wa saratani 1.18 milioni waliripotiwa barani Afrika.

Amesema Ripoti ya Kamisheni ya Lancet Oncology iliyochapishwa Mei 2022, inaonyesha kuwa vifo vya saratani barani Afrika vinatarajiwa kuongezeka mara mbili na kufikia vifo 1.4 milioni kila mwaka ifikapo 2040.

Daktari bingwa wa mionzi ya nuklia hospitali ya Kanda Bugando na msimamizi wa mradi huo Tanzania, Dk Benard Gombanila amesema mradi huo wa miaka minne wa kikanda ya Afrika unaoshirikisha nchi zote wanachama wa nguvu za kiatomiki duniani ambao ulianza mwaka 2024 na unatarajia kufikia kikomo mwaka 2027.

“Lengo kuu ni kusogeza huduma za matibabu ya saratani kuanzia uchunguzi mpaka matibabu kwa nchi za Afrika ambazo inaonekana sehemu kubwa bado zina changamoto sio tu kwa mashine kwa ajili ya matibabu lakini rasimali watu.

Amesema mradi huu umegusa watu kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu na vifaa vimepatikana kupitia mradi huo.

Amesema saratani nchini vinaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na nchi bado hazina uwezo wa kugundua na kutibu kwani kuna upungufu mkubwa wa mashine za uchunguzi na matibabu na wataalamu.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, takwimu za mwaka 2022 za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha Tanzania ina watu wenye saratani 45,000 kwa mwaka na vifo vinavyokaribia 22,000 kwa mwaka kutoka na saratani na vinakadiriwa vitaongezeka mara mbili ndani ya miaka 20 ijayo.

“Kama nchi tuna jukumu kuhakikisha tunaweka mifumo ambayo itasaidia kubaini magonjwa na kutibu ili wapone,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mngereza Miraji Mzee amesema saratani si tena ugonjwa wa siku zijazo bali ni changamoto ya sasa na inayokua ya afya ya umma Zanzibar na barani Afrika.

“Magonjwa yasiyokuambukiza, hasa saratani, yanaweka shinikizo kubwa kwenye mifumo yetu ya afya, yanahitaji utambuzi wa mapema, hatua sahihi, mbinu za matibabu salama, na rasilimali za kibinadamu,” amesema.

Amesema Zanzibar imechukua uamuzi ya kimkakati ya kisiasa na uwekezaji ili kuweka huduma za saratani kama kipaumbele cha kitaifa.

Hatua hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfumo wa Kitaifa wa Kudhibiti Saratani ulioendana na mazoezi bora ya kimataifa.

Pia, ujumuishaji wa huduma za saratani katika ngazi za msingi, sekondari, na za juu za huduma, kuimarisha upigaji picha wa uchunguzi, patholojia na dawa za maabara na kujenga uwezo katika matibabu ya mionzi, dawa za nyuklia, na uuguzi wa onkolojia,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Mionzi Tume ya Nguvu za Atomiki, Dk Emanuel Ngaile amesema kwa Tanzania, mradi huu unakamilisha vipaumbele vya kitaifa katika sekta ya afya na kuchangia juhudi zinazoendelea za kuboresha upatikanaji wa huduma za utambuzi na matibabu ya saratani bora.

Pia, amesema unatoa fursa kwa Tanzania Bara na Zanzibar kuimarisha uwezo wa kitaasisi na kuunganisha huduma za dawa za nyuklia na matibabu ya mionzi ndani ya mifumo ya afya ya kitaifa.

Akifungua mkutano huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kuongezeka kwa matukio ya saratani, pamoja na kikomo cha upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu katika maeneo mengi barani Afrika, kunahitaji kuimarishwa kwa uwezo, ushirikiano wa kikanda na matumizi bora ya sayansi na teknolojia.

Amesema kuna jukumu kubwa kuhakikisha mradi wa RAF6060 unafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.