SUPASTAA wa zamani wa timu DB Lioness, Orlyne Londo aliyetimkia Bravehearts ya Malawi inayoshiriki Ligi ya Kikapu nchini humo amewataja Jesca Lenga wa DB Troncatti, Jesca Ngisaise (JKT Stars) na Irene Gerwin (DB Troncatti) kuwa ndio nyota watatu waliouteka mchezo huo katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kwa Wanawake (WBDL).
Orlyne ameyasema hayo wakati akipiga stori na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, kuwa wachezaji hao wanapokuwa uwanjani hujituma vilivyo katika kuzipigania timu zao kusaka ushindi, huku akiutaja ushindani uliopo katika mashindano hayo.
Mchezaji huyo aliyekuwa staa wa DB Lioness iliyobeba ubingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam msimu uliopita kwa Wanawake (WBDL), amesema pamoja na ubora wa watatu hao, pia ligi hiyo ina ushindani mkubwa kutokana na aina ya wadhamini waliopo wanaotoa motisha nzuri kwa wachezaji.
“Kwa kweli ushindani huo umetokana na udhamini unaowapa motisha wachezaji, hali iliyofanya wachezaji wajitume katika mechi,” amesema Orlyne akilinganisha na mashindano mengine ya kikapu nchini na baadhi ya nchi jirani.
Aliwashauri viongozi wa mikoa mbalimbali kutafuta wadhamini hatua itakayosaidia wachezaji wasikimbilie kusajiliwa katika timu za mkoani Dar es Salaam.
Akizungumzia maandalizi ya mashindano hayo mwaka huu, mchezaji huyo anayecheza namba moja (point guard), amesema amekuwa akifanya mazoezi mara tatu kwa siku ambapo asubuhi hufanya mazoezi ya kukimbia eneo la viwanjani.
“Mchana nafanya mazoezi ya kufunga na jioni tunafanya mazoezi ya pamoja na timu,” amesema Orlyne.
Mchezaji huyo aliyeacha gumzo katika ligi hiyo kabla ya kutimkia Malawi, jina lake lilitawala vinywani mwa mashabiki wa mchezo huo kutokana na uwezo wake wa kukaa na mpira kwa muda mrefu bila kupokonywa na wachezaji wa timu pinzani kwa urahisi.
Sifa nyingine aliyonayo ni uwezo wa kutoa asisti kwa wafungaji pamoja na kupunguza makali ya timu inayoshambulia kwa kutulia na mpira na kubadili mbinu za uchezeshaji na ni kama walivyo mastaa wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), akiwamo Stephen Curry wa Golden State Warriors na Devin Booker wa Phoenix Suns.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa kikapu nchini, Saidi Mussa, amesema kwa sasa kiwango cha uchezaji wa Orlyne kimebadilika tofauti na miaka ya nyuma na kwamba anacheza kwa utulivu, hana haraka akiwa na mpira na pia awapo uwanjani amekuwa akitumia akili zaidi katika kutoa pasi kwa wenzake.
