Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM) Clayton Chipando maarufu Babalevo amesema vijana wa Tanzania wanataka fedha, hawataki konakona.
Babalevo amesema hayo bungeni leo Jumanne Februari 3, 2026 wakati akichangia mapendekezo ya mpango wa Serikali uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Mbunge huyo amesema masharti mengi yanawekwa na taasisi za ukopeshaji kiasi cha kuwafanya vijana washindwe kupata mikopo kama ambavyo Serikali inataka.
Ametolea mfano wa fedha zilizotolewa kwa ajili ya kuwakopesha wasanii akisema zilikuja na masharti na aliyabaini alipokwenda kutafuta mkopo wa Sh100 milioni akajikuta anadaiwa vitu vingi kama dhamana.
Msanii huyo ambaye mchango wake ulikuwa ukipigiwa makofi mara zote, amesisitiza namna ambavyo vijana wanaweza kusaidiwa kwa kupunguza mlolongo wa masharti kwa taasisi zenye dhamana ya mikopo kwa vijana.
“Hawa vijana wetu wanamaliza vyuo kisha wanakuwa na vyeti, tunawaambia wajiajiri na wakienda kutafuta mitaji ya mikopo wanaambiwa wawe na dhamana ya nyumba ama magari watatapa wapi hizo dhamana, mwisho wake wanaishi na ujuzi wao bila kazi,” amesema.
“Hata hivyo, Sh2 bilioni ambazo Makonda (Paul Makonda-Waziri wa Habari) msipokuwa makini mtakuta zinachukuliwa na wasanii na watu wenye mitaji ambao watakuwa na dhamana lakini wenye vipaji wataachwa,” amesema.
Katika kusisitiza hilo, Babalevo amesema: “Vijana wengi wanataka pesa, hawataki konakona na ndiyo maana vijana wengi wana- beti, wanaiua Simba baada ya mechi unachukua hela yako unaendelea na maisha mengine.”
Mbunge huyo ameahidi kuwashukia baadhi ya mawaziri ambao amesema kwao atakuwa kiherehere kwa kuwa yeye ndiye mbunge ambaye hategemei kuteuliwa kuwa waziri.
Babalevo ametaja sababu zinazosababisha asiwe na nafasi ya kuteuliwa kwenye nafasi ya waziri ni kwa sababu ya elimu yake ndogo ingawa hakuitaja elimu aliyonayo na udogo wake ambao mara kadhaa amekuwa akisema.
Ameishauri Serikali kuangalia kodi ambazo wakati mwingine hazina tija akitolea mfano aliponunua nguo za vijana wake huko Dubai kwamba aliposhuka Tanzania alidaiwa fedha kwa nguo za watoto wake watano.
Katika hatua nyingine ameomba Serikali kutazama zao la michikichi na migebuke (samaki wa kuokwa) kwamba vikiwekwa mazingira mazuri inaweza kuwasaidia wananchi wa jimbo lake kujikwamua kiuchumi.
Kingine amemwomba Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kesho atakapoanza kushuka mji wa Kigoma aangalie chini ataona vumbi jingi kwa kuwa huo ndiyo mji ambao hauna barabara na kumtaka Waziri wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe kumjengea barabara.
“…nashukuru sana Rais Samia mawaziri ambao amewaleta sasa hivi, ni mawaziri shupavu ni mawaziri wa kutosha na mimi ndiye mbunge pekee ambaye sitegemea kuteuliwa kuwa waziri kwa sababu ya elimu niliyonayo kwa hiyo nawategemea sana, sina wivu na ninyi lakini mawaziri sitawaacha,” amesema Babalevo.
Katika mchango wake, Babalevo amesema ubunge ni ajira yake ya mwisho na ameahidi kuwatumikia wananchi wa Kigoma Mjini kwa uwezo wake wote, akitumia elimu na uzoefu alionao ili kuleta maendeleo chanya katika jimbo hilo.
Amesema kwanza anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuweka hai hadi kufikia hatua hiyo, akieleza safari ya kampeni haikuwa rahisi kutokana na changamoto na hekaheka nyingi.
