Na FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Baada ya mafuriko makubwa ya mwaka 2024 kukata mawasiliano na kuhatarisha maisha ya wananchi wa Kata ya Ngerengere, hali iliyosababisha adha kubwa ya usafiri na kudhoofisha shughuli za kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia wakala wa barabara mijini na vijijini TARURA mkoa wa Morogoro ililazimika kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto hiyo ya muda mrefu.
Serikali ilitenga jumla ya shilingi 200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la upinde wa mawe katika barabara ya Ngerengere – Sinyaulime lenye urefu wa mita 30 na midomo miwili ya kupitisha maji, sambamba na uchongaji wa barabara yenye urefu wa kilometa moja, mradi uliolenga kurejesha mawasiliano ya uhakika na usalama wa usafiri kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza na Michuzi Blog kwenye ziara ya kamati ya siasa Mkoa wa Morogoro iliyokuwa ikikagua miradi ya barabra ndani ya Halmashauri hiyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Sinyaulime Shabani Ramadhani amesema kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na adha ya usafiri na usafirishaji, hususani nyakati za mvua, baada ya daraja hilo kusombwa na maji na kukatiza mawasiliano, kuhatarisha maisha ya wananchi na kudhoofisha shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Morogoro katika maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho, mkandarasi M/S Yesaca Civil and Building Works Company Limited anaendelea na kazi bila kuwasilisha madai ya malipo hadi sasa, huku thamani ya mradi ikifikia shilingi 199,668,112.
Mradi huo wa dharura unasimamiwa na TARURA Wilaya ya Morogoro hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 80, huku unatarajiwa kukamilika Aprili 8, 2026, baada ya ratiba ya awali kuathiriwa na changamoto za mvua.
Kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa kuta za daraja, uchongaji wa barabara, uwekaji wa kifusi, ujenzi wa kinga za daraja (gabions), uwekaji wa guard rail pamoja na kuvunja daraja la zamani, hatua zinazolenga kuhakikisha daraja linakuwa imara, salama na la kudumu.
Aidha baada ya kutembela na kukagua kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Morogoro imelidhika na utekelezaji wa mradi huo na kuipongeza TARURA kwa usimamizi mzuri, ikisisitiza kuwa barabara ni kiungo muhimu katika kukuza uchumi na ustawi wa jamii.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Joseph Masunga, amesema kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa maeneo hayo, hususani katika kusafirisha mazao ya kilimo na kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Ndyamukama amesema wakala huo umejipanga kuhakikisha maeneo yote korofi nyakati za mvua yanaboreshwa ili kurahisisha huduma kwa wananchi, kulingana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Nae Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Nuru Ngereja ameitaka TARURA na TANROADS kukamilisha miradi yote inakamika kwa wakati ili kukidhi hitaji la watanzania huku ikisisitiza kutoa kazi kwa wakandalasi wanaotekeleza miradi kwa wakati.
Wadau wa maendeleo wameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo ni ushahidi wa utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Awamu ya Sita na Ilani ya CCM kwa vitendo, hasa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha miundombinu ya vijijini.

