Kinachoibeba Bandari Tanzania First League

MTENDAJI Mkuu wa klabu ya Bandari Tanzania, Ismail Chempele amesema maandalizi makubwa waliyofanya mwanzo wa msimu yakijumuisha usajili bora wa kikosi, benchi la ufundi, bajeti nzuri na mazingira salama ya kambi, ndiyo siri ya ubora walionao kwenye michuano ya First League.

Timu hiyo ambayo iko Kundi A la First League, imemaliza mzunguko wa kwanza kwa kucheza mechi saba ikiwa kileleni, ikikusanya pointi 17, huku ikiwa haijapoteza mechi.

Bandari ambayo ni msimu wake wa kwanza kushiriki First League baada ya kupanda daraja, imeshinda mechi tano na sare mbili, huku ikifunga mabao 12 na kuruhusu matatu.

Katika kundi A lenye Cosmopolitan, Nyumbu, Moro Kids, Magnet FC, Pan African, Green Warriors na Dar City, Cosmopolitan inashika nafasi ya pili na pointi 13, huku Nyumbu ikiwa na pointi 12 nafasi ya tatu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chempele alikiri ligi hiyo ni ngumu kwani imesheheni timu kubwa zenye uzoefu ambazo zimewahi kucheza hadi Ligi Kuu, lakini kutokana na maandalizi ya kutosha waliyoyafanya mwanzo yamewasaidia kuwa hapo walipo.

“Siri ni maandalizi na kutambua kile tunachokiendea, mpira ni burudani yenye gharama, hivyo unatakiwa kuwa na nidhamu na kuziheshimu zile njia unazopita kwenye mpira mafanikio utayaona,” amesema Chempele na kuongeza;

“Sisi kama uongozi na timu tumeweka bajeti yetu nzuri, tumetengeneza wachezaji wetu vizuri, tumefanya usajili mzuri, benchi la ufundi tumeliweka vizuri, mazingira ya timu inapokaa na namna wanavyoishi.”

Amesema ili kufikia malengo wanayoyakusudia ya kupanda daraja kwenda Ligi ya Championship, wameamua kufuata taratibu za uendeshaji wa soka la kisasa na kuiishi misingi ya timu ya kisasa bila ubabaishaji.

“Ligi ni ngumu, timu zimejiandaa lakini kwa kujiandaa kwetu kama timu na mipango yetu imetupelekea kuwa hapo. Tulijua tunakwenda kucheza ligi yenye wazoefu wengi na sisi ni wageni timu yetu ni changa, kwa ufupi mwanga umeoneka kutokana na namna tulivyojiandaa,” amesema.

Kiongozi huyo amesema licha ya kiwango hicho bora katika mzunguko wa kwanza, wameiboresha timu yao kwa kuongeza wachezaji saba kupitia usajili wa dirisha dogo baada ya mapendekezo ya benchi la ufundi.

Bosi huyo aliwashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kuiunga mkono, huku akiahidi kwamba sapoti wanayoendelea kupata basi mambo mazuri na mengi yanakuja na watafanikiwa kwa pamoja kufikia malengo.

Bandari baada ya kuichapa Dar City mabao 4-0 na kumaliza mzunguko wa kwanza wa First League, kocha mkuu wa timu hiyo, Omega Seme, amewapa mapumziko ya siku nane wachezaji wa kikosi hicho.