Tanga. Sakata la kuondoa huduma za upakiaji na ushushaji wa abiria wa mabasi ya mikoani katikati ya Jiji la Tanga limechukua sura mpya baada ya Baraza la Madiwani kumuomba Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, kutumia mamlaka yake kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.
Awali, Halmashauri ya Jiji la Tanga ilielekeza wamiliki wa mabasi ya mikoani kuacha kupakia na kushusha abiria katikati ya jiji na badala yake kutumia Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange, ambacho Serikali imewekeza miundombinu ya kisasa kwa ajili ya huduma hiyo.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mabasi yote ya mikoani yanashusha na kupakia abiria wanaoingia na kutoka nje ya Mkoa wa Tanga katika kituo hicho, ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji.
Meya wa Jiji la Tanga, Alhaji Mustapher Selebosi, amesema utekelezaji wa agizo hilo umekuwa ukisuasua licha ya maandalizi yote kufanyika.
“DC, tunaomba hili likamilike mara moja. Mahitaji ya msingi yote yamefanyiwa kazi na hata tumeongeza zaidi. Nimpongeze mkurugenzi na timu yake ya menejimenti kwa kutenga fedha za kuboresha huduma, hususan kwa wafanyabiashara wadogo waliowekewa miundombinu bora na ya uhakika,” amesema Selebosi.
Ameongeza kuwa halmashauri imetenga maeneo maalumu kwa mama lishe na jitihada zinaendelea kutafuta fedha za kuwaandalia mazingira yanayolingana na hadhi ya kituo hicho.
“Nikuombe sana mheshimiwa DC, kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa, usimamie suala hili ili ifikapo Januari 30, shughuli hii iwe imetekelezwa kikamilifu,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Khalid Hamza, amewataka madiwani kuungana kwa maslahi mapana ya jiji.
“Kama kuna jambo litakaloipa heshima jiji letu ni kusimamia kwa pamoja kuondolewa kwa mabasi katikati ya mji. Kutakuwa na kelele na maneno mengi, lakini kwa kuwa huu ni mpango wa Serikali, wadau wanapaswa kutii,” amesema Hamza.
Diwani wa viti maalumu, Anjelika Nyangasa, amesema mpango huo ni wa maendeleo na hauna budi kuungwa mkono licha ya malalamiko ya awali.
“Kituo cha Kange kimepooza kwa muda mrefu. Dar es Salaam watu walilalamika kuondoka Mnazi Mmoja kwenda Ubungo na baadaye Mbezi, lakini walihamia. Huwezi kupinga mabadiliko yenye lengo la maendeleo,” amesema Nyangasa.
Diwani wa Kata ya Mnyanjani, Thobias Haule, amesema kuchelewa kutekeleza mpango huo kunapoteza dhumuni la uwekezaji uliofanyika.
“Kituo kimejengwa kwa lengo la kutoa huduma na kuwa chanzo cha mapato. Hilo halitafikiwa kama mabasi yataendelea kufanya kazi katikati ya jiji na kusababisha msongamano,” amesema Haule.
Akizungumzia mpango huo, dereva wa daladala aliyefanya kazi Kange kwa zaidi ya miaka 10, Rashid Mtoi, amesema,“Hatua hii itaongeza mapato ya halmashauri. Ahadi ya kuhamisha mabasi imekuwa ikitolewa kwa muda mrefu bila utekelezaji, sasa ngoja tuone.”
Mkazi wa Wilaya ya Pangani, Zaituni Msangi, amesema utekelezaji wa agizo hilo utasaidia kulifufua jengo la kitega uchumi lililopo kituoni hapo.
“Mji utapangwa vizuri zaidi, mapato yataongezeka na hata kipato cha mtu mmoja mmoja kitaimarika,” amesema Msangi.
Dereva wa gari la abiria linalofanya safari kati ya Tanga na Lushoto, Laurent Jambo, amesema mpango huo ni mzuri, lakini changamoto ipo kwenye utekelezaji.
“Hoja ni nzuri, lakini tatizo limekuwa ni uwajibikaji mdogo katika kusimamia utekelezaji wake,” amesema Jambo.
Mkazi wa Korogwe, Matiasi Mdoe, amesema Serikali iliwekeza fedha nyingi katika kituo hicho, lakini hakijatumika ipasavyo.
“Nimefurahi kusikia maelekezo ya kuhamisha vituo vyote kuja hapa, kwa sababu maandalizi na uwekezaji tayari umefanyika,” amesema Mdoe.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, amesema, “Mabasi yamekuwa yakiingia katikati ya jiji na kusababisha msongamano. Vikao vimeshafanyika na makubaliano yamefikiwa ya kuhamishia huduma Kange.”
Amesema kampuni zilizo na stendi zinazokidhi vigezo zinaweza kufikiriwa, lakini waliokosa vigezo utekelezaji utafanyika mara moja.
“Tunawataka wafanyabiashara na wamiliki wa mabasi kuhamia maeneo sahihi kabla ya Januari 30 ili mabasi yote yatumie Kituo cha Kange,” amesema Kolimba.
