Mahakama yaamuru Waziri wa zamani kulipa fidia ya Sh3.18 bilioni

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, imemuamuru aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, Manispaa ya Kinondoni na Naomi Raymond Kwayu kulipa fidia ya Sh3.18 bilioni kwa kubomoa nyumba ya makazi kinyume cha sheria.

Pia, Mahakama hiyo imewaamuru wadaiwa hao kulipa fidia ya madhara ya Sh40 milioni pamoja na gharama zote za kesi.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi ya ardhi namba 000032646 ya mwaka 2024, shauri hilo linatokana na tukio la Februari 29, 2024, Silaa, akiwa Waziri wa Ardhi wakati huo, alifika katika eneo husika na kusimamia ubomoaji wa nyumba hiyo.

Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Januari 21, 2026, na Jaji Sharmila Sarwatt, aliyebatilisha uamuzi wa Waziri Silaa wa kubomoa ghorofa, unatokana na mgogoro wa umiliki wa kiwanja kilichopo kitalu namba 484 (2196), Block H, Mbezi Medium Density, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Jaji Sarwatt alitoa hukumu hiyo kutokana na kesi iliyofunguliwa katika Mahakama hiyo na mfanyabiashara Johnsen Leonard Mahururu dhidi  ya Waziri Silaa na wenzake.

Mahururu kwenye madai yake aliomba Mahakama hiyo itamke kuwa, yeye ndiye mmiliki halali wa kiwanja na itoe amri ya zuio kwa Naomi kuingia katika kiwanja hicho na kufanya shughuli zozote.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Kamishna wa Ardhi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Naomi Raymond Kwayu anayejulikana pia kama Fainess Dawson Kiwia, aliyemilikishwa kiwanja hicho, pamoja na Juma Rajab Kapungu.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa  akisimamia ubomoaji wa nyumba ya makazi Februari 29, 2024. Picha na Maktaba

Pia, Mahururu aliomba Mahakama itamke kuwa kitendo cha kutoa hati ya umiliki kwa Naomi ni kinyume cha sheria, kwa kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa kiwanja  hicho kisheria; hivyo Msajili wa Hati  aamriwe kubatilisha hati ya umiliki iliyo katika jina la Fainess Dawson Kiwia na kukisajili  kwa jina lake, Mahururu.

Awali, aliiomba Mahakama iwaamuru mdaiwa wa kwanza mpaka wa sita kwa pamoja na kila mmoja binafsi kumlipa fidia ya Sh16.2 bilioni, ikiwa ni thamani ya mali zilizoharibiwa au kupotea kutoka kwenye jengo la makazi na jengo la hoteli wakati wa ubomoaji. Hata hivyo kwenye uamuzi wa Mahakama imeamriwa alipwe Sh3.18 bilioni.

Mahururu pia aliomba Mahakama iwaamuru wadaiwa wa kwanza mpaka wa sita  kwa pamoja na kila mmoja binafsi kumlipa fidia ya  Sh3.18 bilioni, ikiwa ni thamani ya nyumba ya makazi na ya hoteli walizozibomoa.

Aliomba pia Mahakama iwaamuru wadaiwa hao wamlipe Sh4  milioni  kwa kila siku kama hasara ya  biashara kuanzia Septemba mosi, 2024 hadi malipo yatakapokamilika na Sh300,000 kwa siku ikiwa ni gharama za malazi ya hoteli kuanzia Machi Mosi, 2024 hadi malipo yatakapokamilika.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa  akisimamia ubomoaji wa nyumba ya makazi Februari 29, 2024. Picha na Maktaba

Mbali na fidia hizo pia aliomba amri ya kulipwa riba ya kibiashara kuanzia Februari 2024 hadi malipo yatakapokamilika, riba kwa kiwango cha Mahakama kwa jumla ya fidia watakayoamuriwa kumlipa,  tarehe ya hukumu hadi malipo yatakapokamilika.