Mahakama yaamuru Waziri wa zamani na wenzake kulipa fidia ya Sh3.18 bilioni

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, Manispaa ya Kinondoni na Naomi Raymond Kwayu wameamriwa na Mahakama kulipa fidia ya Sh3.18 bilioni kwa kubomoa nyumba ya makazi kinyume cha sheria.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi jijini Dar es Salaam, pia imewaamuru wadaiwa hao kulipa fidia ya madhara ya jumla ya Sh40 milioni pamoja na gharama zote za kesi.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi ya ardhi namba 000032646 ya mwaka 2024, shauri hilo linatokana na tukio la Februari 29, 2024, Silaa akiwa Waziri wa Ardhi wakati huo, alifika katika eneo husika na kusimamia ubomoaji wa nyumba hiyo.

Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Januari 21, 2026 na Jaji Sharmila Sarwatt aliyebatilisha uamuzi wa Waziri Silaa wa kubomoa ghorofa, unatokana na mgogoro wa umiliki wa kiwanja kilichopo kitalu namba 484 (2196), Block H, Mbezi Medium Density, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa  akisimamia ubomoaji wa nyumba ya makazi Februari 29, 2024. Picha na Maktaba

Jaji Sarwatt alitoa hukumu hiyo kutokana na kesi  iliyofunguliwa katika Mahakama hiyo na mfanyabiashara Johnsen Mahururu dhidi  ya Waziri Silaa na wenzake watano.

Hata hivyo, akitoa ufafanuzi wa hukumu hiyo, wakili wa Mahururu, Barnabas Luguwa alisema anayewajibika kulipa fidia hiyo ni Silaa.

“Sisi mbali na kuishtaki Serikali lakini  pia tulimshtaki Silaa kwa jina lake,” alisema Wakili Luguwa.

Hata hivyo, wadaiwa walioorodheshwa kwenye uso wa hukumu wapo saba  na jina la Silaa halimo, lakini ndani ya hukumu Mahakama imetaja idadi ya wadaiwa kuwa ni wanane na kwamba mdaiwa wa nane pia aliwakilishwa na mawakili wa Serikali, lakini hajatajwa jina lake wala cheo au wadhifa wake.

Kwa upande wake Silaa hakupokea simu kadhaa alizopigiwa na gazeti hili ikiwamo kutokujibu ujumbe mfupi wa maandishi aliotumiwa.

Mahururu kwenye madai yake aliomba Mahakama hiyo itamke kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa kiwanja na itoe amri ya zuio kwa Naomi kuingia katika kiwanja hicho na kufanya shughuli zozote.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu (Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Kamishna wa Ardhi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Naomi Raymond Kwayu anayejulikana pia kama Fainess Dawson Kiwia aliyemilikishwa kiwanja hicho, pamoja na Juma Rajab Kapungu.

Jaji Sarwatt katika uamuzi wake amewataka Silaa, Manispaa ya Kinondoni na Naomi (anayetambulika pia kama Fainess Dawson Kiwia), aliyemilikishwa kiwanja hicho na Waziri Silaa kumlipa Mahururu Sh3.18 bilioni ikiwa fidia ya thamani ya nyumba ya makazi iliyobomolewa na Sh40 milioni kama fidia ya madhara ya jumla pamoja na gharama za kesi.

Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, katika hukumu yake imekubaliana na madai ya Mahururu hasa ya msingi ambapo imetamka kuwa ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho.

Pia, Jaji Sarwatt ametamka kuwa utoaji wa hati ya umiliki ya kiwanja hicho kwa Naomi ni batili, huku akimuamuru Msajili wa Hati kurekebisha usajili wa kiwanja hicho kisajiliwe kwa jina la Mahururu.

Vilevile Jaji Sarwatt ametoa amri ya zuio la kudumu kwa Naomi na mtu yeyote anayeweza kufanya kazi kwa maelekeo yake kuingia, kuvamia au kuingilia kwa namna yoyote ile umiliki na matumizi ya kiwanja hicho.

Katika hatua nyingine Jaji Sarwatt amekataa madai mengine ya Mahururu yakiwamo ya fidia ya Sh16.2 bilioni ikiwa ni thamani ya mali zilizoharibiwa au kupotea kutoka kwenye jengo la makazi na jengo la hoteli wakati wa ubomoaji.

Katika hukumu hiyo Jaji Sarwatt amesema kuwa, kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Mahakama imebaini kuwa, kiwanja hicho kilitolewa kwa watu wawili Wood Pecker Limited na Naomi.

Hata hivyo, amesema inaonesha wa kwanza kupewa alikuwa ni Kampuni ya Wood Machi 6, 1987 na Naomi Julai 12, 1987 na kwamba kwa mujibu wa  kanuni ya kipaumbele mtu aliyepata ugawaji wa ardhi hiyo kwanza kwa wakati ndiye anayepaswa kuzingatiwa kwanza.

Hivyo basi, ni wazi kuwa Wood Pecker Limited ilipewa barua ya toleo mapema kuliko mshtakiwa wa sita. Kwa msingi huo, Wood Pecker Limited ilikuwa na masilahi bora na ya juu zaidi katika ardhi hiyo kuliko mshtakiwa wa sita.

Kuhusu uhalali wa ubomoaji ingawa Mahururu  alidai kuwa aliomba na kupata vibali vya kujenga nyumba ya makazi na hoteli, lakini hakuna ushahidi uliotolewa kuthibitisha madai hayo kuhusiana na ujenzi wa hoteli.

Ushahidi unaonesha wazi kuwa kibali pekee kilichotolewa katika kiwanja husika na ambacho kilipokewa na Mahakama kama kielelezo ni cha ujenzi wa nyumba ya makazi ya ghorofa mbili.

“Kwa kuwa kulikuwa na kibali halali cha kujenga nyumba ya makazi, basi ubomoaji wa nyumba ya makazi ulikuwa kinyume cha sheria,” amesema Jaji Sarwatt.

Kuhusu hoteli, amesema kuwa alishindwa kuthibitisha kuwa alikuwa na kibali halali kutoka kwa mamlaka husika kinachomruhusu kujenga hoteli kwenye kiwanja hicho kinyume na Kanuni ya 139(1) ya Kanuni za Mamlaka za Serikali za Mitaa (Udhibiti wa Maendeleo ya Miji), 2008.

Amesema hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa, notisi ilitolewa kabla ya ubomoaji huo.

Hata hivyo, amesema japo ilibomolewa bila notisi, lakini ilijengwa kinyume cha sheria.

Awali, Mahururu aliiomba Mahakama itamke kuwa kitendo cha kutoa hati ya umiliki kwa Naomi ni kinyume cha sheria, kwa kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa kiwanja  hicho kisheria. Aliomba Msajili wa Hati  aamriwe kubatilisha hati ya umiliki iliyo katika jina la Fainess Dawson Kiwia na kukisajili  kwa jina lake, Mahururu.

Vilevile aliomba Mahakama iwaamuru mdaiwa wa kwanza mpaka wa sita kwa pamoja na kila mmoja binafsi kumlipa fidia ya  Sh16.2 bilioni,  ikiwa ni thamani ya mali zilizoharibiwa au kupotea kutoka kwenye jengo la makazi na jengo la hoteli wakati wa ubomoaji.

Mahururu pia aliomba Mahakama iwaamuru wadaiwa wa kwanza mpaka wa sita  kwa pamoja na kila mmoja binafsi kumlipa fidia ya  Sh3.18 bilioni, ikiwa ni thamani ya nyumba ya makazi na ya hoteli walizozibomoa.

Aliomba pia Mahakama iwaamuru wadaiwa hao wamlipe Sh4  milioni  kila siku kama hasara ya  biashara kuanzia Septemba mosi, 2024 hadi malipo yatakapokamilika na Sh300,000 kwa siku ikiwa ni gharama za malazi ya hoteli kuanzia Machi mosi, 2024 hadi malipo yatakapokamilika.

Mbali na fidia hizo pia,  aliomba amri ya kulipwa riba ya kibiashara kuanzia Februari 2024 hadi malipo yatakapokamilika, riba kwa kiwango cha Mahakama kwa jumla ya fidia watakayoamuriwa kumlipa,  tarehe ya hukumu hadi malipo yatakapokamilika.

Siku hiyo  Silaa  aliyekuwa Waziri wa Ardhi wa wakati huo,  Naomi/Fainess,  maofisa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni na Kamishna wa Ardhi wa Dar es Salaam, walidaiwa kuvamia ardhi  na kubomoa nyumba ya makazi ya familia ya Mahururu pamoja na jengo la hoteli lililokuwa likijengwa.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa  akisimamia ubomoaji wa nyumba ya makazi Februari 29, 2024. Picha na Maktaba

Silaa aliamuru na kusimamia ubomoaji nyumba hiyo  kwa madai kuwa Mahururu hakuwa mmiliki halali wa kiwanja hicho, bali alikuwa mvamizi kufuatia malalamiko ya Naomi/Fainess aliyedai kuwa ndiye alikuwa mmiliki halali.

Hata hivyo, siku hiyo ubomoaji huo haukufanikiwa badala yake waliondoka na kurudi mahali hapo Machi mosi, 2024, kwa kutumia tingatinga ubomoaji wa nyumba hizo ulikamilika.

Kisha Silaa alimtangaza Naomi kuwa ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho na baadaye hati ya umiliki ikasajiliwa kwa jina lake Fainess Dawson Kiwia.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo Mahururu aliwakilishwa na wakili Barnaba Luguwa  huku Katibu Mkuu, Waziri, Kamishna wa Ardhi Manispaa ya Kinondoni na AG  waliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Pauline Mdendemi na Jeremia Odinga.

Naomi kwa upande wake aliwakilishwa na wakili Gordian Mugusi huku  Kapungu akiwakilishwa na wakili Paul Elias.