IMEKUWA ni kawaida kwa baadhi ya wachezaji wazawa wa kikapu nchini kutojiamini katika mechi wanazocheza kutokana na aina ya ushindani wanaokutana nao kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani.
Makocha wakongwe wa kikapu wamezungumzia sababu zinazochangia hilo kutokea wakidai licha ya hofu kuwa jambo la kawaida, lakini ina sababu zingine nje ya ukweli ubora wanaoweza kuwa wanakutana nao kutoka kwa wapinzani wao.
Hofu hiyo inaweza kuondoka endapo makocha watawaelimisha wachezaji hao kuhusu athari zinazoweza kujitokeza baada ya kucheza kwa kutojiamini, ikiwamo kupoteza mechi au kupata majeraha yasiyotarajiwa.
Kamishna wa makocha wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Nchini (TBF), Robert Manyerere, anasema ili mchezaji aweze kujiamini ni lazima awe na uzoefu wa mchezo, na bila hivyo inakuwa vigumu kujiamini hasa anapowaona wapinzani wake wakicheza kwa kasi na kuonana ipasavyo.
Amesema kwa lugha ya kitaalamu ni lazima mchezaji awe katika hatua ya juu ya kujifunza akiwa na uwezo wa kutambua jambo na umahiri nalo.
“Unajua wachezaji wazawa wengi hawajifunzi kwa hatua. Lakini, changamoto hii siyo, bali ni ya upande wa makocha zaidi ambao nao pengine hawafahamu hatua na namna za kujifunza, hivyo kuchangia kuruka hatua na kukosa kujiamini,” amesema Manyerere.
Kocha wa JKT, Alfred Ngalalija aliwataka makocha wenzake kutumia muda mwingi kuwajenga wachezaji katika mazingira ya kujiamini huku wakijikita katika ubora, uelewa mpana wa mchezo na hasa kisaikolojia.
Amesema makocha wengi hupenda wachezaji waliofundishwa vizuri na wenye uwezo mkubwa, suala ambalo kwa chipukizi lina shida iwapo hawatakutana na wakufunzi bora.
Akizungumzia suala la upotevu wa mpira kwa urahisi, Manyerere amesema inatokana na ukosefu wa umahiri katika umiliki na kuuhifadhi na ili mchezaji asipoteze anatakiwa kufanya mazoezi mengi ya kumjenga katika umiliki.
“Kwa mfano kudunda mara kwa mara na kucheza mpira kila wakati pamoja na kucheza mchezo wa mmoja kwa mmoja (1 v 1),” amesema Manyerere na kusisitiza kwamba wachezaji kupumzishwa hutokana na uamuzi wa kocha wa timu husika kulingana na mbinu, mikakati na namna anavyousoma mchezo.
