Maxime asisitiza jambo, Josiah apiga mkwara

WAKATI leo Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ukitarajiwa kuchezwa mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Mbeya City na Dodoma Jiji, makocha wa timu hizo kila mmoja ameibuka kwa staili yake akizitaka pointi tatu.

Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mecky Maxime amesisitiza jambo kwa mastaa wake baada ya kubaini kuna tatizo la kuruhusu mabao katika kila mchezo, hali ambayo ameifanyia kazi huku akiwataka mastaa wake kupambana kupata pointi tatu.

Amesema anachofurahia ni jinsi timu ilivyoimarika na kuweza kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini umakini wa kufunga umekuwa changamoto akieleza kuwa anaamini leo hali itakuwa tofauti.

“Tumekuwa tunaruhusu mabao, lakini nimeliona na kulifanyia kazi, nimewaambia suala la matokeo ya nyuma yasikae akilini bali tupambane upya na bahati nzuri wameimarika kwa kutengeneza nafasi suala ni kufunga,” amesema kocha huyo.

MBE 01


Kwa upande wa Dodoma Jiji, kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah amesema hawaingii kazini wakimtegemea mchezaji mmoja, Wiliam Edgar bali wapo wengine wenye uwezo wa kumaliza mchezo.

Kwa hivi karibuni, Edgar amekuwa na kiwango bora akifunga mabao katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Yanga walipolala 3-1 na wakiilaza JKT Tanzania bao 1-0.

Timu hiyo ambayo haikuwa na mwanzo mzuri msimu huu katika Ligi Kuu Bara, kwa sasa imeonekana kuwa imara ambapo katika mechi tano zilizopita, imepoteza moja dhidi ya Yanga, ikishinda mbili sawa na sare.

MBE 02


Josiah amesema wakati wakiikabili Mbeya City, watakuwa makini kutokana na hali waliyonayo wapinzani, lakini matokeo mazuri ya Dodoma Jiji inawapa nguvu na matumaini ya kufanya kweli.

Amesema Edgar amekuwa bora, lakini si mchezaji ambaye wanamtegemea kila kitu badala yake wanategemea matokeo ya timu kwa ujumla na kwamba wapo wachezaji wenye uwezo wa kuamua mechi iwapo nyota huyo atabanwa.

“Wakimbana Edgar, kuna Beno Ngasa, George Makang’a, Dickson Ambundo, Idd Kipagwile, Elias Maguli, Yassin Mgaza na Anuari Jabir, wote hawa wanaweza kufanya kazi eneo la mbele,” amesema Josiah.

MBE 03


Kocha huyo wa zamani wa Biashara United, Tunduru Korosho na Tanzania Prisons, ameongeza kwamba, mkakati wao ni kumaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo akieleza kuwa anaendelea kuisuka zaidi timu.

Kwa upande wake winga wa Dodoma Jiji, Beno Ngassa, amesema baada ya kusota mechi za mwanzoni bila kupata matokeo mazuri, kwa sasa ari na morali vimeamka upya kufuatia kile walichovuna kwa mechi za karibuni.

Amesema kiwango alichonacho kwa sasa si juhudi zake binafsi bali ushirikiano na wenzake kikosini na maelekezo ya benchi la ufundi akieleza kuwa matarajio yao ni kuona wanaendelea kufanya vizuri.

“Tunacheza kama timu na hatukuwa na mwanzo mzuri lakini tunashukuru kwa sasa tumebadilika na tunahitaji kulinda tulichonacho, si juhudi binafsi bali ni maelekezo ya kocha na ushirikiano kikosini,” amesema Ngasa.

MBE 04


Wakati huohuo, kipa wa Mbeya City, Soud Dondola, amesema mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji ni kufa au kupona, akieleza kuwa pointi walizopoteza zinatosha na sasa kazi inaanza upya.

Mbeya City imekuwa na matokeo mabovu tangu kuanza msimu huu wa Ligi Kuu, ambapo kwa sasa ipo nafasi ya 14 kwa pointi tisa baada ya michezo 12 na leo Jumanne itakuwa nyumbani Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kuikaribisha Dodoma Jiji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dondola amesema wamepitia kipindi kigumu ambacho kwao wanaona kama sehemu ya kujifunza, akieleza kuwa pointi walizopoteza zinatosha na sasa ni wakati wao kuanza rasmi kazi.

Amesema makosa yaliyoonekana kwa muda wote, benchi la ufundi limeona akieleza kuwa wataiheshimu Dodoma Jiji lakini pointi tatu ni lazima ili kurejesha matumaini kwa mashabiki na wao binafsi uwanjani.

“Tumeachana na yaliyotokea nyuma, tunaenda kuanza upya, hata maji baharini huchafuka, kisaikolojia tuko fiti na kocha amesahihisha makosa na tumekubaliana na kujifunza kwa kilichojitokeza ila sasa inatosha na kesho ni kufa au kupona,” amesema Dondola.