Mbunge wa zamani Munde afariki dunia, kuzikwa kesho

Tabora. Mbunge wa zamani wa wa viti maalumu (CCM), mkoa wa Tabora, Munde Tambwe amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam  alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mwili wa Munde ambaye amewahi Halmashauri Kuu (NEC) unasafirishwa leo kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoa wa Tabora ambako maziko yatafanyika kesho Jumatano, Februari 4, 2026 katika Manispaa ya Tabora baada ya swala ya adhuhuri.

Munde amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu mkoa wa Tabora kwa misimu mitatu mfululizo.

Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu Munde Tambwe

Jaha Kaducha, mmoja wa wanafamilia ya Munde amesema, “Tumeondokewa na mtu muhimu kwenye familia. Munde ni zaidi ya kiongozi, mzazi na mlezi, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha yake.”

Mkazi wa Tabora, Mwajuma Abasi, amesema Munde alikuwa kiongozi imara, mwenye mapenzi mema kwa watu wa Tabora, kwani mara kadhaa akiwa bungeni alikuwa akichangia hoja zinazogusa maisha ya wana Tabora moja kwa moja.

Maandalizi bado yanaendelea nyumbani kwa aliyekuwa mbunge mstaafu viti maalum mkoa wa Tabora Munde Tambwe.

“Kwa Tabora sijui tutaweka wapi haya machozi, ila ni Mungu tu ameamua kuchukua mja wake.  Tunamshukuru. Munde alitugusa hasa wanawake, akatuwezesha kupata mikopo na hata gesi tulipika vizuri,” amesema.

Kwa upande wake, Maria Kambilo amesema maisha ya mwanasiasa huyo yalikuwa zawadi kwa watu wa Tabora kutokana na utendaji kazi wake bora uliotukuka.

“Wananchi waliona na walifaidika naye kupitia mapambano yake dhidi ya matatizo ya wananchi wake.

“Alikuwa na mapenzi kwa watu wa Tabora, yaani alikuwa anapenda nyumbani na hata aende wapi, anajua yeye ni mzaliwa na mkazi wa Tabora, na hata akiona fursa lazima anawahi Tabora. Anakula na wa nyumbani,” amesema.