Mzee Hood afariki dunia, wadau wamzungumzia

Morogoro. Mfanyabiashara maarufu aliyekuwa mmiliki wa Kampuni ya Usafirishaji ya Mabasi Hood ya mkoani Morogoro, Mohamed Hood Said (90)) amefariki dunia jana Februari 2, 2026 akiwa nyumbani kwake Mtaa wa Mlapakoro, Kata ya Mji kuu Manispaa ya Morogoro.

Akitoa taarifa za kifo cha mfanyabiashara huyo mtoto wa marehemu Faiz Abdallah Salumu amesema baba yake mkubwa amefariki dunia jana saa 12 jioni.

“Huyo marehemu mzee Hood mimi ni baba yangu mkubwa, na mpaka anafariki alikuwa mzee sana, hivyo hakuugua bali alifariki kifo cha kawaida tu, akiwa nyumbani kwake,” amesema Salim.

Amesema taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu na wanatarajia kumzika leo saa saba mchana katika makaburi ya Kola yaliyopo Manispaa ya Morogoro.

Mweka hazina wa Chamacha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) Issa Nkya amesema mzee Hood alikuwa mwalimu aliyewafundisha wafanyabiashara wengi hasa namna ya kuendesha biashara ya usafirishaji.

“Nimepata taarifa hizi jana usiku nikiwa jijini Arusha, ilinibidi nisafiri usiku ili niweze kufika Dodoma na muda (saa tatu asubuhi) najiandaa kwenda Morogoro kushiriki mazishi ya mzee wetu,” amesema Nkya ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Happy Nation.

Amesema kabla hajaanza kuingia kwenye biashara hiyo, mzee Hood alimwita na kumfundisha misingi ya uendeshaji wa biashara ya usafirishaji na kumueleza miiko ya biashara hiyo.

“Mzee Hood alikuwa anaijua vyema biashara ya usafirishaji na ndio maana alidumu kwa muda mrefu katika biashara hiyo, na hata alipoacha aliweza kuendesha biashara zake nyingine huku akiwa mshauri na mwalimu mzuri wa wafanyabiashara wengine waliochipukia kwenye biashara hii niwamo mimi,” amesema Nkya.

Amesema mchango wake katika sekta ya usafirishaji na uchumi wa Taifa kwa jumla ni mkubwa.

“Ushindani wa kibiashara uliopo sasa hata kipindi ambacho mzee Hood anafanya biashara ya usafirishaji ulikuwepo, zilikuwepo kampuni nyingi lakini Hood bado alilishika soko na alikuwa kinara katika suala la usafirishaji,” amesema Nkya.

Amesema wakati wa uhai wake mzee Hood alimfanya kama mtoto wake, hivyo alikuwa akimueleza mambo mengi yanayohusu biashara, chama na hata masuala ya kifamilia.

Akieleza mchango wa Hood aliyehudumu nafasi ya uenyekiti wa Taboa kwa zaidi ya miaka 11, amesema aliweza kutoa mchango wake wa mawazo na busara kwa uongozi mpya.

Amesema kwa kuwa chama kimepoteza wanachama wawili ambao ni mzee Hood na mzee Nasor Hamdan ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya NBS, viongozi wa Taboa wamelazimika kugawana majukumu.

Amesema wapo viongozi wamekwenda Tabora kushiriki mazishi ya mzee Hamdan na kutoa rambirambi lakini yeye na baadhi ya wanachama wanaelekea mkoani Morogoro kwenda kushiriki mazishi ya mzee Hood.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye amesema atamkumbuka Hood kwa mambo mengi mema lakini machache ni pamoja na utii katika kufuatia sheria za usafirishaji.

Amesema Hood,  hakuwahi kumpendelea dereva wake yeyote aliyeleta uzembe na kuvunja sheria za usalama barabarani.

Andengenye amesema mara zote Hood alikuwa tayari kutoa ushirikiano polisi na hakuwahi kutumia vibaya nafasi na umaarufu wake kukandamiza wala kuchongea askari wa usalama barabarani badala yake akitumia njia sahihi za kuwasilisha malalamiko yake pale ambako askari amekosea.

“Ipo tabia ya baadhi ya wasafirishaji ya kuwatumia askari barabarani kukandamiza wasafirishaji wenzao ili wao wafanye biashara, hili mzee Hood hakuwahi kulifanya, mara zote alipenda wafanyabiashara wachanga wakue na wale aliokuwa akishindana nao kibiashara aliweza kwenda nao sawa,” amesema Andengenye.

Amesema mzee Hood hakuwahi kuwa na ugomvi na Jeshi la Polisi,  bali alijitoa kuhakikisha jeshi linatekeleza wajibu wake, na hata alipokuwa juu kibiashara hakuwabeza wala kuwafanyia fujo wasafirishaji wenzake.

“Mbali na kufanya naye kazi, mimi kwangu nilimuona na kumchukulia kama baba na rafiki, tulikuwa tikizungumza mengi yanayohusu namna ya kuboresha sekta ya usafirishaji na usalama barabarani,”amesema.

Andengenye amesema akiwa mwenyekiti wa Taboa, mzee Hood hakuwa kushinikiza migomo ya mabasi bali alipenda mijadala na utatuzi wa changamoto zilizokuwepo kwa wakati huo kwa njia ya mazungumzo.