Pingamizi lakwamisha kesi watuhumiwa walioandamana kufanya uhaini

Arusha. Mabishano ya kisheria yameibuka katika kesi ya kukusanyika na kuandamana kwa lengo la kufanya uhaini, inayowakabili washtakiwa watano baada ya upande wa utetezi kuwasilisha pingamizi, kupinga Jamhuri kuomba kuingiza vielelezo kwenye mfumo.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha maombi kwamba, miongoni mwa vielelezo walivyotaja wakati wa kusoma maelezo ya awali (PH) katika kesi hiyo, havijaingizwa kwenye mfumo.

Leo Februari 3, 2026, shauri hilo la jinai namba 38539/2025 linalosikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Jeniffer Edward wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, lilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi upande wa Jamhuri.

Washtakiwa hao waliOkamatwa Oktoba 29, 2025 katika tukio la vurugu zilizotokea eneo la Mianzini ni Abubakar Issa, Daniel Mbwambo, Hassan Ibrahim, Masoud Idd, Israel Mollel.

Kabla ya kesi kuendelea Wakili wa Serikali, Witness Mosoli aliwasilisha ombi hilo.

“Tumebaini kwamba miongoni mwa vielelezo tulivyotaja kwenye PH havijawa filed (havijawasilishwa) kwenye mfumo licha ya kutajwa, hivyo tunaomba Mahakama yako tuzi-file nyaraka au vielelezo hivyo kwenye mfumo na nakala tutawapa upande wa pili kama sheria inavyoelekeza,” amesema Mosoli.

Kufuatia maombi hayo, upande wa utetezi uliokuwa ukiwakilishwa na wakili wanne, wakiongozwa na Ally Mhyela waliweka pingamizi kufuatia maombi hayo.

 “Wakili hakutoa sababu yoyote ya msingi kuhusiana na ombi lao la kutaka kuongeza vielelezo hii haina maana isipokuwa ku pre- empt mwenendo, kwamba kukiwa na gap (pengo) wanaomba kujazia,” amesema Mhyela  na kuongeza:

“Kwa mantiki hiyo, tunaomba wasiruhusiwe kuongeza vielelezo wanachotaka kuongeza mahakamani kwani mahakamani siyo mahali pa kuviziana, ni mahali pa kujiandaa, walikuwa na muda wa kujiandaa na kesi yao. PH walisoma wao wenyewe, hawajaja na sababu ya msingi, hivyo wasiruhusiwe kwani wakiruhusiwa itawanyima haki washtakiwa.”

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Jamhuri Mosoli aliomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hilo na kuruhusu vielelezo hivyo vipokelewe kwani siyo kitu kigeni, walishavitaja wakati wa PH.

“Tumesikia hoja za upande wa utetezi akisema Jamhuri hatujatoa sababu yoyote kuhusiana na lengo la kuongeza vielelezo hivuo na kwamba tumeona gap kwa hiyo tunajipanga.

“Hii siyo kweli wakati tunaleta ombi nilisema vielelezo ambavyo tumepanga kuvi-file tulishavitaja wakati wa PH na nikasema sababu ni kwamba havikupandishwa kwenye mfumo, siyo kitu kigeni kama ilivyowasilishwa na utetezi,” amefafanua.

Wakili huyo ameeleza kuwa upande wa utetezi kusema wanajaribu kurekebisha siyo kweli, na kuwa hawajaieleza Mahakama ni kwa namna gani kuongezwa kwa vielelezo hivyo kutawaathiri washtakiwa, huku akiiomba Mahakama kutupilia mbali pingamizi na kukubali ombi lao.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 11,2026 Mahakama hiyo itakapotoa uamuzi mdogo,siku ambayo pia washtakiwa hao wanaokabiliwa na kesi ya uhaini watakaposomewa PH katika kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.