:::::::
Na OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OWM- TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekutana na uwakilishi wa Benki ya NMB na kujadili namna wanavyoweza kufanya maboresho katika mchakato wa kutoa fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi kupitia taasisi hiyo ya kifedha.
Prof. Shemdoe amekutana na ujumbe huo leo Februari 03, 2026 ofisini kwake jijini Dodoma, ikiwa ni mwendelezo wa Serikali kutafuta namna bora ya kurahisisha utolewaji wa mikopo hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha makundi yote lengwa ya Wanawake, Vijana na wenye Ulemavu yananufaika na mikopo hiyo.
Msisitizo wa Prof. Shemdoe kwa ujumbe huo ulioongozwa na Mkuu wa Biashara ya Serikali wa Benki ya NMB, Bi. Vicky Bishubo umekuwa ni kuhakikisha vikundi vya wanufaika vyenye sifa stahiki vinapata mikopo hiyo kwa wakati.
Sanjali na hilo, Prof. Shemdoe ameipongeza na kuishukuru Benki ya NMB kwa kuiunga mkono Serikali katika uboreshaji wa miundombinu ya afya msingi na elimu msingi pamoja na kurahisisha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa walengwa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya walengwa kutakiwa kuweka dhamana ili kupata mikopo ya asilimia 10, Bi. Bishubo amesema kuwa, hoja hiyo si ya kweli kwani mikopo hiyo ni nafuu na inatolewa bila dhamana yoyote, hivyo amewataka walengwa kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo.
Katika hatua nyingine, uwakilishi huo wa Benki ya NMB umekutana na Naibu Waziri OWM- TAMISEMI, anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, pamoja na Naibu Waziri, OWM – TAMISEMI, anayeshughulikia Afya, Mhe. Dkt. Jafal Seif kama sehemu ya Kuimarisha mahusiano baina ya Benki hiyo na OWM- TAMISEMI.




