Serikali kuboresha bandari za Kibirizi, Ujiji

Dodoma. Serikali imesema imeanza utekelezaji wa hatua za kurejesha bandari za Kibirizi na Ujiji mkoani Kigoma zilizokumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika, hali iliyosababisha kudorora kwa shughuli za usafirishaji na biashara.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumanne, Februari 3, 2026, na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (ACT-Wazalendo), Kiza Mayeye, aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali kurejesha bandari hizo ambazo ni muhimu kwa uchumi wa Kigoma na nchi jirani.

Naibu Waziri huyo amesema Serikali, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ilifanya tathmini ya kina ya madhara yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi katika Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, ambapo bandari kadhaa zilibainika kuathiriwa, zikiwemo Ujiji na Kibirizi.

Amesema kufuatia tathmini hiyo, TPA imeanza kazi za ukarabati pamoja na kuweka miundombinu mbadala ili kurejesha ufanisi wa bandari hizo.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 2026, hatua itakayorejesha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi kupitia Ziwa Tanganyika.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa Serikali kukamilisha miradi ya kuunganisha uchumi wa Kigoma na nchi jirani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na namna taifa litakavyonufaika kwa kuhusisha sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari hizo.

Akijibu swali hilo, Kihenzile amesema Serikali imetenga Sh2.3 bilioni kwa ajili ya kuwezesha miradi ya bandari kuwa na tija, ikiwemo ujenzi wa soko na kufungua bandari ili kuchochea biashara na uwekezaji wa sekta binafsi.

Amesema hatua hizo zinalenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa biashara kati ya Kigoma na DRC, kuongeza mapato ya Serikali na kuwanufaisha wananchi kupitia ajira na fursa za kiuchumi.