Serikali yatoa msimamo riba ya asilimia 7 kwa wafanyakazi

Dodoma. Serikali imesema haina mpango wa kuamuru taasisi za fedha kupunguza riba za mikopo kwa wafanyakazi hadi kufikia asilimia 7 au 8, ikieleza kuwa viwango vya riba nchini huamuliwa na misingi ya soko huria kulingana na sera za uchumi zinazotekelezwa.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo, Jumanne Februari 3, 2026, na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, wakati akijibu swali la mbunge wa Kigamboni, Haran Nyakisa Sanga, aliyetaka kujua ni lini wafanyakazi wa Tanzania watanufaika na mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 7 au 8.

Akijibu swali hilo, naibu waziri amesema riba za mikopo zinazotolewa na taasisi za fedha kwa wateja mbalimbali, ikiwemo wafanyakazi, huamuliwa na nguvu ya soko (market-determined) na si kwa maelekezo ya Serikali.

Amesisitiza kwamba kuzielekeza benki au taasisi za fedha kuweka kiwango maalumu cha riba, kama asilimia 7, kutakuwa kinyume na mwelekeo wa sera ya uchumi wa soko huria inayotumika nchini.

Hata hivyo, amesema sera hiyo haizuii taasisi za fedha kuamua kwa hiari kutoa mikopo kwa wafanyakazi kwa riba ya asilimia 7 au pungufu, endapo zitaona kuna mazingira yanayoruhusu kufanya hivyo.

Aidha, amebainisha kwamba mkopaji yeyote, ikiwemo mfanyakazi, ana fursa ya kufanya mazungumzo na benki husika na kukubaliana kiwango cha riba kitakachotumika kulingana na makubaliano yao.

Naibu waziri amesema wafanyakazi kupitia waajiri wao wanaweza kuwasiliana na benki au taasisi za fedha na kujadiliana kuhusu riba nafuu kwa mikopo yao, hatua ambayo inaweza kusaidia kupunguza gharama za mikopo bila kuvunja misingi ya soko.

Ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kuunda mazingira wezeshi kwa watumishi wa umma kupitia mfuko maalumu wa Wizara ya Fedha, lengo likiwa ni kuwezesha utoaji wa mikopo kwa masharti nafuu yenye riba ya asilimia 4 ili kuimarisha uchumi wa wafanyakazi.

Amesema hadi sasa jumla ya Sh74 bilioni zimekopeshwa kwa wafanyakazi kupitia taasisi zao, hatua ambayo itasaidia kuboresha maisha yao, kuunda matumaini mapya na kuongeza uwezo wa kifedha wa kaya za watumishi hao.

Amesema mfumo huo unalenga kutoa suluhisho la kifedha lenye tija kwa watumishi, huku akisisitiza utekelezaji unaendelea kwa umakini kuhakikisha riba nafuu inafikiwa na mikopo inatolewa kwa usawa.

Majibu hayo yameweka wazi msimamo wa Serikali wa kuendelea kulinda sera ya soko huria, huku ikihamasisha mazungumzo ya hiari kati ya wafanyakazi, waajiri na taasisi za fedha ili kupata mikopo yenye masharti nafuu zaidi.

Katika hatua nyingine, Serikali imefafanua sababu zinazowalazimu wakulima kununua mbegu za mahindi kila msimu wa kilimo badala ya kutumia mbegu wanazovuna mashambani, ikieleza hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha uzalishaji wenye tija na ubora unaokusudiwa.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amesema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Urambo, Magreth Sitta, aliyetaka kujua kwa nini mkulima analazimika kununua mbegu za mahindi kila mwaka badala ya kutumia mbegu alizovuna.

cAkijibu swali hilo, Silinde amesema mbegu zinazouzwa katika maduka ya pembejeo zimepitia majaribio ya kisayansi katika maabara mbalimbali ili kuthibitisha ubora wake, ikiwemo kiwango cha juu cha uzalishaji, uhimilivu dhidi ya magonjwa pamoja na uwezo wa kustahimili ukame.

Amesema mkulima anapotumia mbegu alizovuna kama mbegu kwa mara ya pili au zaidi, sifa za awali za mbegu husika hupungua au kupotea kabisa, hali inayosababisha kushuka kwa uzalishaji na tija shambani.

Silinde amesema asilimia kubwa ya mbegu zinazotumiwa na wakulima nchini ni mbegu za chotara, ambazo hutengenezwa kwa kutumia aina mbili au zaidi za mbegu wazazi kutoka jamii moja.

Amesema kutokana na muundo wake wa kisayansi, mbegu hizo haziwezi kuhifadhi sifa zake bora endapo zitatumika tena kama mbegu, jambo linalochangia kupungua kwa mavuno na kuathiri kipato cha mkulima.

Amewahimiza wakulima kuendelea kutumia mbegu bora zilizoidhinishwa ili kuongeza uzalishaji, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Katika swali la nyongeza, mbunge wa Urambo alitaka kujua mkakati wa Serikali katika kupunguza gharama za kilimo cha mahindi, hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini, kuweza kumudu gharama ya uzalishaji na hatua zinazochukuliwa kulinda mazao dhidi ya wadudu waharibifu.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo amesema kuwa Serikali ina mpango wa kupunguza gharama za kilimo kwa wakulima kupitia ruzuku ya pembejeo za kilimo, ikiwemo mbegu, viuatilifu na mbolea.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha mchakato wa kilimo unakuwa endelevu na bei za mazao zinapungua, jambo litakalowezesha wakulima kupata faida kubwa zaidi na kuongeza tija ya kilimo cha mahindi.

Kuhusu wadudu waharibifu, amesema Serikali inendelea na tathmini ya kina ya changamoto zinazotokana na wadudu, ili kuimarisha mikakati ya udhibiti wa wadudu bila kuathiri uzalishaji.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa ruzuku na usimamizi wa wadudu unaendelea kwa hatua zilizopangwa kitaalamu, kuhakikisha kila hatua inachangia kuongeza tija na kulinda maslahi ya mkulima.