Shule hizi bado hazijapoa matokeo kidato cha nne

Mwanza. Licha ya Serikali kusitisha utaratibu wa kutangaza shule bora kitaifa, matokeo ya kidato cha nne 2025 yanaonyesha kuwa baadhi ya shule zilizowahi kutamba kimatokeo,  bado zinaendelea kufanya vizuri kwa kiwango cha juu, zikirekodi ufaulu wa asilimia 100 kwa watahiniwa wake wote kupata  daraja la kwanza.

Uchambuzi wa matokeo ya shule tano ambazo kwa muda mrefu zilikuwa hazikosi katika orodha ya vinara kitaifa, unaonyesha kuwa zimepata ufaulu wa asilimia 100 wa daraja la kwanza.

Uchambuzi huo ni kwa mujibu wa mapitio ya matokeo yaliyotangazwa Jumamosi ya wiki iliyopuita  na kuwekwa kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Baadhi ya shule hizo ni Mzumbe (Morogoro), Kemebos  (Kagera), St. Francis Girls’  (Mbeya), Canossa (Dar es Salaam) na Ahmes (Pwani).

Kwa mujibu wa tovuti hiyo; www.necta.go.tz, shule ya Mzumbe ilikuwa na watahiniwa 94 huku wote wakipata daraja la kwanza, sambamba na shule nyingine zilizopata daraja hilo kwa wanafunzi wake wote.

St Francis ilikuwa na watahiniwa 91, Kemebos (67), Ahmes (78) na Canossa (101).

Necta ilitangaza rasmi kusitisha utaratibu wa kupanga na kutangaza shule na wanafunzi 10 bora kitaifa Januari 29, 2023 wakati ikitangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne wa mwaka 2022.

Aliyekuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi alisema baraza lilibaini kuwa hakuna tija ya kuendelea na utaratibu huo, akieleza kuwa kumtaja mwanafunzi mmoja au shule moja kati ya wengi haikuwa msingi sahihi kwani mazingira ya shule yanatofautiana.

“Ina tija gani kumtaja mmoja kati ya shule nyingi na tena bahati mbaya unamlinganisha mtu na mwingine ambaye hawakusoma kwenye mazingira yanayofanana?” alihoji Amasi na kuongeza:

“Kutangaza shule ya kwanza huenda tunaifanyia biashara, kwa hiyo ni jambo ambalo halina tija tumeona tuondokane nalo.’’

Awali, Necta ilianza mabadiliko haya kwa matokeo ya darasa la saba, ikieleza kuwa imeondokana na mazoea yaliyokuwa hayana mchango chanya kwa mfumo wa elimu.

Lengo likiwa kuunda mazingira yenye usawa, kupunguza presha kwa wanafunzi na walimu, na kuhakikisha kwamba ushindani haupo kwa sababu ya utajiri wa shule au rasilimali.

Wanachosema wadau wa elimu

Mhitimu wa  Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (Saut), Msafiri Msekwa anasema matokeo ya shule zilizokuwa 10 bora mara kwa mara yanaonesha wazi kuwa ubora hauko kwa bahati,  bali kwa ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya mwanafunzi mmoja mmoja.

Anasema matokeo hayo pia yanaonesha nidhamu ya muda mrefu ya kitaaluma, walimu wenye uzoefu na motisha pamoja na utamaduni wa ushindani wa ndani unaojengwa na shule hizo.

“Shule hizi zinaonyesha kwamba misingi thabiti ya kitaaluma haiwezi kufutwa kwa sera…shule zinazoweka nidhamu na uwajibikaji wa walimu na wanafunzi zinaendelea kutoa matokeo bora,”anasema na kuongeza:

“Matokeo ya kidato cha nne 2025 yanaonyesha kuwa hata bila kutangazwa rasmi, ubora wa elimu hauwezi kufichwa….shule zilizowahi kutamba zinaendelea kuzungumza kupitia takwimu, si matangazo”.

Mchambuzi na mdau wa elimu, Christina Nyangindu anasema uamuzi wa Serikali uliua kabisa ari ya ushindani wa kitaaluma miongoni mwa walimu na wanafunzi, hali iliyosababisha kushuka kwa viwango vya uwajibikaji katika baadhi ya shule.

“Badala ya Serikali kurekebisha vigezo na kuondoa upungufu uliokuwapo katika mfumo huo, ilichagua njia rahisi ya kufuta mfumo mzima, jambo ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu nchini,” anasema Nyangindu.

Anasema mfumo wa kutangaza shule bora ulikuwa kichocheo cha bidii, nidhamu na ubunifu kwa walimu huku pia ukiwawezesha wazazi na wadau wengine kupata taarifa sahihi kuhusu hali halisi ya utoaji wa elimu.

Nyangindu anaongeza kuwa kurejeshwa kwa mfumo huo kwa vigezo vilivyoboreshwa, kutasaidia kuimarisha ushindani wa haki, kuongeza uwazi na kuchochea maboresho ya kweli katika sekta ya elimu, hususan kwa shule za Serikali zinazofanya kazi katika mazingira magumu.

Naye mhadhiri wa Saut kampasi ya Malimbe Mwanza, Mary Kalumbete anasema uamuzi wa kusitisha utaratibu wa kutangaza shule bora, ni wa kisera usiozingatia athari za muda mrefu kwa maendeleo ya elimu nchini.

“Serikali inaonekana kukwepa lawama zinazotokana na kushuka kwa viwango vya elimu kwa kuficha uhalisia wa matokeo, badala ya kukabiliana na changamoto zilizopo kwa uwazi na ujasiri wa kisera,” anasema.

Anaongeza: “Uwazi katika matokeo ya elimu ni nguzo muhimu ya uwajibikaji, kwani huwafanya walimu, wasimamizi wa shule na Serikali yenyewe kuwajibika ipasavyo kwa jamii.’’

Mdau wa elimu na mmiliki wa kituo cha elimu Ngwanza, mkoani Simiyu, Dk Jerry Nyabululu anasema uamuzi wa Serikali ni mfano wa sera inayolinda udhaifu badala ya kukuza ubora katika sekta ya elimu.

“Kwa kuchanganya dhana ya usawa na kufuta kabisa ushindani wa kielimu, Serikali imetuma ujumbe usio sahihi kwa walimu na wanafunzi wanaojituma, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya elimu kwa ujumla,” anasema.

“Usawa haupaswi kumaanisha kufuta viwango au kuficha matokeo, bali kutoa fursa sawa kwa shule zote huku zile zinazofanya vizuri zikitambuliwa na kuigwa,”anaongeza.

Kwa upande mwingine, mwalimu mstaafu Bakari Heri anasema, Serikali ilikuwa sahihi kufuta utaratibu huo akieleza kuwa matokeo yalitumika kama matangazo ya kibiashara.

‘’Kwanza ilikuwa sawa na kutangaza biashara za watu lakini pia ilikuwa ni aina mojawapo ya kuifanya elimu yetu kuonekana kuwa ipo kibiashara zaidi. Lakini kwa upande mwingine, Serikali ilishabaini kuwa elimu sio ufaulu wa mitihani pekee,’’ anasema.

Mwalimu Heri anaungwa mkono na Pendo Msita anayesema: ‘’ Nadhani Serikali ilishaona madhara yake kwani sasa tungekuwa na elimu inayojali mitihani na hivyo wahusika wangekuwa wakitumia kila mbinu hata zile chafu ili kupata ufaulu mzuri.’’