UWT yatoa vifaa vya Sh20 milioni hospitali Dodoma, Kunambi ahimiza umoja, mshikamano

Dodoma. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Suzan Kunambi, amesema chama hicho kimejengwa juu ya misingi ya umoja na mshikamano, hali iliyosaidia kudumisha amani na utulivu nchini.

Amesema hiyo ni tunu adhimu na msingi wa maendeleo ya Taifa, na kutokana na hilo, amewataka wananchi kutokubali kuchochewa kutumia tofauti za kiitikadi, kisiasa, kidini au kikabila kuvuruga amani iliyopo nchini.

Kunambi ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Februari 3, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Nguji, Kata ya Ng’hong’onha, Jijini Dodoma.

Katika maadhimisho hayo, jumuiya hiyo imetoa msaada wa vifaa vya matibabu vyenye thamani ya Sh20 milioni kwa wodi ya wazazi na watoto wajiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Amesema CCM ni chama kilichojengwa juu ya misingi ya uzalendo, umoja, mshikamano na maendeleo ya watu tangu kuanzishwa kwake, na kimeendelea kuwa mhimili mkuu wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, amesema chama hicho kimekuwa chachu ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa ahadi zake zilizomo katika ilani za uchaguzi.

Kunambi amebainisha kuwa CCM kimekuwa kinara katika kuhimiza usawa wa kijinsia na kutoa fursa kwa wanawake kushiriki katika vyombo vya uamuzi.

Pia, amesema kupitia UWT, wanawake wamepata jukwaa la kujiimarisha kisiasa, kiuchumi na kijamii, huku jukumu kubwa la jumuiya hiyo likiwa ni kuhamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wakati wa chaguzi.

“Leo tunajivunia kuona wanawake wakishika nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa. Mfano mzuri ni uchaguzi mkuu uliopita ambapo idadi ya wabunge wanawake wa majimbo imeongezeka kutoka 26 hadi 36,” amesema Kunambi.

Kaimu kwenyekiti wa Bodi ya wakurugezi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma Mchenya John akimkabidhi tuzo ya kutambua mchango wa Jumuiya ya UWT kwenye sekta ya afya katibu mkuu wa Jumuiya hiyo Suzan Kunambi baada ya kupokea msaada wa vifaa vya matibabu.

Amesema maadhimisho hayo si ya kusherehekea pekee, bali ni fursa ya kutafakari wajibu wa wanawake kama nguzo ya familia na Taifa.

Amesisitiza kuwa wanawake wana nafasi kubwa ya kuimarisha maadili, kulea kizazi chenye uzalendo na kulinda amani ya nchi, huku akiwataka kusimama imara kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, ubaguzi na unyanyasaji, pamoja na kuhamasisha elimu kwa watoto wa kike na wa kiume.

Katika kuenzi fikra za waasisi wa CCM, Kunambi amesema maadhimisho ya miaka 49 yamebeba kaulimbiu: “Tumechagua umoja na amani kwa maendeleo ya Taifa letu,” akisisitiza kuwa kauli hiyo inabeba wajibu wa Watanzania kuilinda na kuiendeleza amani na utulivu ili Taifa lipate maendeleo endelevu.

Aidha, amewakata wanawake kukemea vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na watu wanaotamani kuona Taifa linasambaratika.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mchenya John, amesema vifaa hivyo vimewasili kwa wakati muafaka kutokana na hospitali hiyo kukabiliwa na ongezeko la watoto wanaozaliwa kabla ya muda na wenye uzito mdogo, huku idadi ya vitanda ikiwa ndogo kiasi cha kuwalaza watoto wawili katika kitanda kimoja.

Amesema mashine ya kuwapa joto watoto wajiti iliyotolewa na UWT ni msaada mkubwa, kwa kuwa hospitali ilikuwa na mashine moja isiyotosheleza mahitaji. Hivyo, amesema msaada huo utachangia kuokoa maisha ya Watanzania wenye hali ya chini.

Kwa upande wake, muuguzi mfawidhi wa hospitali hiyo, Stanley Mahundo, ameikabidhi UWT cheti na tuzo ya kutambua mchango wake katika kuimarisha huduma za afya, huku akiiomba iendelee kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji.