Vikwazo matibabu ya kisukari nchini vyatajwa

Unguja. Wakati wagonjwa wa kisukari wakiongezeka, usambazaji usiothabiti wa dawa ya insulini hususani maeneo ya vijijini, gharama kubwa na uwezo mdogo wa familia nyingi kumudu matibabu, vimetajwa kuwa vikwazo katika kupambana na ugonjwa wa kisukari.

Pia, utegemezi mkubwa wa insulini kutoka mataifa ya Ulaya, upungufu wa wataalamu na uelewa mdogo wa jamii kuhusu dalili za kisukari vinaendelea kuziumbua nchi za Afrika.

Takwimu za Mfuko wa Taifa wa Taarifa za Afya (DHIS2) zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano, idadi ya watu wanaoishi na kisukari imeongezeka kutoka watu 680,445 mwaka 2021 nchini Tanzania hadi watu 863,741 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 27.

Hayo yamebainishwa leo Februari 3, 2026 katika mkutano wa kimataifa wa kushughulikia changamoto na vikwazo vya upatikanaji na usambazaji wa dawa ya Insulini (ACCISS) Unguja, Zanzibar.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua mkutano huo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema tatizo hilo linahitaji juhudi za kikanda ili kuhakikisha mahitaji hayo yanatimizwa kupitia mifumo thabiti iliyoratibiwa na huduma za afya.

“Ni wazi kuwa ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ni uthibitisho kwamba, changamoto ya ugonjwa wa kisukari sio ya sekta moja wala nchi moja pekee, bali ni changamoto ya afya duniani kote inayoathiri mamilioni ya watu wa rika mbalimbali,” amesema Dk Mwinyi.

Amebainisha kuwa, licha ya ufanisi wa dawa hiyo, bado kuna changamoto kubwa ikiwamo kukosekana kwa usawa duniani katika upatikanaji wa dawa hizo bora na zenye unafuu.

Dk Mwinyi amebainisha kuwa nchi nyingi duniani hasa zenye kipato cha kati zinakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya watu wenye uhitaji wa dawa hiyo.

Hata hivyo, amesema Serikali ina wajibu kuunda mazingira wezeshi kupitia sera madhubuti, ufadhili endelevu na ushirikiano unaohakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

“Ni lazima tuwekeze katika kinga, uchunguzi wa mapema na huduma endelevu sambamba na kuunga mkono tafiti za uzalishaji wa ndani wa dawa muhimu ikiwamo insulini,” amesema.

Dk Mwinyi amesema zaidi ya Watanzania milioni 2.9 wanaishi na kisukari, kati ya hao zaidi ya watu 10,000 wanahitaji insulini ili kuendelea kuishi na kuboresha maisha yao.

Aidha, amesema kwa sasa Tanzania bara na Zanzibar zina zaidi ya kliniki 170 zenye jumla ya watoto 7,607 wanaoishi na maradhi ya kisukari aina ya kwanza kati ya hao 7,134 ni Tanzania bara na 473 ni wa Zanzibar.

Washiriki wa mkutano wa Kimataifa wa kushughulikia changamoto na vikwazo vya upatikanaji na usambazaji wa dawa ya Insulini kwa ugonjwa wa kisukari kutoka mataifa 15 ya Afrika na Ulaya wakifuatilia hotuba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla alipomwakilisha kufungua mkutano huo Unguja, Zanzibar.

Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema upatikanaji wa dawa muhimu za kuokoa maisha hususan insulini ni haki ya msingi ya binadamu.

Dk Saada amesema Mpango wa Maendeleo Endelevu wa mwaka 2050, umeweka viashiria muhimu vya utendaji ikiwa ni pamoja na kuongeza wastani wa kuishi kutoka miaka 65 mwaka 2019 hadi miaka 75.

Amesema, pia, unakusudia kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi yasiyoambukiza kutoka asilimia 4.9 hadi asilimia 2.2 ifikapo mwaka 2050.

“Ili kuyafikia malengo haya lazima tuwe na mfumo imara katika afya ikiwamo upatikanaji wa insulini zenye viwango na kwa wakati katika maeneo yote kwa jamii,” amesema.

Dk Saada amesema kuna changamoto mbalimbali zinasababisha kuwa na matatizo katika upatikanaji wa insulini katika nchi za Afrika ambazo zinafanana kwa kiasi kikubwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kisukari Tanzania (TDA), Professa Kaushik Ramaiya,  amesema tangu mwaka 2003 wanasambaza dawa za kisukari na kuwaangalia watoto wenye kisukari na kuna watoto 7,800 wanaotibiwa ugonjwa huo.

Amesema mkutano huo umelenga kujadili upatikanaji wa dawa za insulini na namna ya kuboresha matibabu ya maradhi ya kisukari.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema dawa ya insulini imekuwa ikiokoa maisha kwa zaidi ya karne moja sasa na mamilioni ya watu wanaoishi na maradhi ya kisukari hususan katika nchi zenye kipato cha kati haipatikani kwa urahisi.

Amesema kutokana na changamoto hiyo gharama, mifumo ya usambazaji na uwezo wa mifumo ya afya, vikwazo hivyo vinaendelea kuweka mzigo mkubwa usiokubalika kwa watu binafsi, familia na mifumo ya afya ya kitaifa.

Dk Mngereza amesema takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa  watu milioni 1.7 wanaishi na kisukari na takriban watu milioni 1.3 hawakuwa wamegundulika.

Kwa mujibu wa takwimu za kipindi cha mwaka 2017 hadi mwaka 2024 makadirio ya kiwango cha maambukizi yanaonesha kuanzia asilimia 3.6 mwaka 2017 hadi asilimia 9.8 mwaka 2024.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2020 zinaonesha kuwa, vifo 6,247 vinatokana na kisukari, sawa na asilimia 2.12 ya vifo vyote. Tanzania, zaidi ya watu 2.9 wanaishi na kisukari na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo ni takribani asilimia mbili ya vifo vyote katika rika zote.

Amesema ongezeko hilo ni ishara kwamba, juhudi zinahitajika kuchukuliwa zaidi na kuimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali kupitia ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.

Ofisa Mkuu wa kiufundi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, majeraha na afya ya akili kutoka Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia  Magonjwa (CDC), Dk Adelard Kakunze amesema ipo haja kuondoka kwenye nadharia na kwenda kwenye vitendo katika kudhibiti magonjwa hayo.

Amesema lazima dawa za insulini zipatikane kwa wepesi na kwa gharama nafuu ili kuokoa maisha ya wananchi wengi wanaotaabika na ugonjwa huo.

Mkutano huo wa siku tatu umewakutanisha wajumbe kutoka nchi 15 za Afrika wakiwemo wadau wa sekta ya afya washirika wa maendeleo, madaktari bingwa, watafiti, mabalozi na watu wanaoishi na maradhi ya kisukari kwa lengo la kujadiliana, kubadilisha uzoefu na kuweka dhamira ya dhati ya watu wanaoishi na maradhi hayo.