Wabunge waibua kilio miradi kutokamilika, rushwa ikitajwa

Dodoma. Hofu, rushwa na utitiri wa miradi vimetajwa kuwa kikwazo cha kukwamisha miradi mingi nchini huku Serikali ikielezwa kuwa, kwenye utekelezaji wake wahusika hawaongei lugha moja.

Mambo hayo yameibuliwa na wabunge leo Jumanne Februari 3, 2026 wakati  wakichangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 na ya mwaka 2026/27.

Julai 17, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Dira 2050 akielekeza kukamilika kuandika mpango elekezi wa muda mrefu, kukamilika kuandika mpango wa nne wa maendeleo wa miaka 25 na kukamilika kuandika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/27.

Mpango huo unaojadiliwa, uliwasilishwa bungeni jana Jumatatu, Februari 2, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo akiwasilisha bugeni mpango elekezi wa maendeleo wa muda mrefu 2026/2027 – 2050/2051, mpango wa nne wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano 2026/2027 – 2030/2031 na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2026/2027, jijini Dodma Februari 2, 2026.

Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku maarufu Msukuma amesema Tanzania ni hodari katika kupanga isipokuwa haina mikakati ya kusimamia utekelezaji na mara nyingi unapofika wakati wa utekelezaji wahusika hawatembei pamoja.

Msukuma amesema kwenye utekelezaji kila mtu anakuwa kivyake huku akilaumu namna ambavyo makandarasi wazawa wanavyotembea na vidonge mifukoni, kutokana na kuugua vidonda vya tumbo kwa sababu ya mawazo ya madeni na misukosuko wanayoipitia.

“Mara nyingi tunapanga vizuri, lakini ikifika kwenye utekelezaji tunatawanyika kila mtu sehemu yake, yaani kusimamia mipango hatuwezi, lakini Serikali haiongei na kuimba wimbo mmoja, lazima tuwe na ufuatiliaji wa miradi ya awali kabla ya kuanza mipango mingine,” amesema Msukuma.

Msukuma ameitaka Serikali kusimamia kile inachokipanga ili iweze kwenda vizuri huku akisisitiza suala la kuwajali makandarasi wazawa ambao kwa mujibu wa maelezo yake wanaishi kwa shida kubwa ukilinganisha na wageni ambao mikataba yao inawalinda bali wazawa wanaishia kujikomba maofisini.

Kilio kingine cha Msukuma ni utekelezaji wa ujenzi wa barabara kutoka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam akisema kuna matuta mengi yanayofanya wasafiri wasiwe kwenye hali nzuri na kuhoji waliosanifu walitoka wapi.

Kwenye mpango huo, amesifia kipengele kinachotaja nafasi za wenyeviti wa bodi kwamba watapatikana kwa ushindani huku akipendekeza suala la umri kwa wajumbe hao litazamwe ili nafasi ziwafikie wenye nguvu badala ya kutoa kwa watu ambao umri unawataka wapumzike.

Ameiomba Serikali katika mipango yake kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambao kwa maelezo yake, amesema ni muda mrefu ujenzi wake ulianza lakini hakuna kinachoendelea.

Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema kutokuwepo kwa tathmini ya mara kwa mara kunasababisha miradi mingi kushindwa kuleta tija kwa wananchi badala yake kila wakati kunabaki na maneno.

Sanga amesema utitiri wa miradi kwenye mipango unasababisha kuwepo na mianya ya rushwa ndani ya miradi ambayo ametaja kuwa inatokana na eneo la kusaini mikataba.

“Rushwa imeshamiri maeneo mengi, eneo mojawapo ni katika kusaini mikataba lakini mifumo ya ukusanyaji mapato bado ni utitiri, nashauri tuwe na mfumo mmoja ambao unadhibiti utoroshaji wa fedha kama tulivyoona maeneo mengine ikiwamo pale Hospitali ya Tumbi (Kibaha),” amesema Sanga.

Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe  ametilia shaka juu ya kutokuwepo kwa mpango wa matengenezo jambo alilosema kuna wakati litakuja kusababisha mipango yote kutokuwa kwenye malengo.

Mafuwe amesema ili mipango hiyo iweze kukamilika na kuwa ya kudumu, ni lazima Serikali ikubali kutenga fedha katika mpango wa matengenezo kwa kuwa, miradi inayotekelezwa haijawekewa kinga ya namna gani inaweza kufanyiwa matengenezo kwa haraka.

Wabunge wengine ambao waligusia hoja hiyo ni Abdallah Chikota (Nanyamba) ambaye alidai tabia ya kuanzisha miradi mipya wakati baadhi ya miradi iliyopo bado haijakamilika jambo alilosema linasababisha kupoteza fedha za umma na kuwanyima wananchi matokeo ya maendeleo yaliyokusudiwa.

Mwingine alikuwa Mbunge wa Ludewa (CCM), Joseph Kamonga ambaye hoja yake iliungana na Chikota huku akieleza tathmini na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ni jambo la msingi kabla ya kuanzisha miradi mingine.

Kamonga amesisitiza kuanzishwa kwa taasisi maalumu ya kufanya tathmini na ukaguzi wa miradi ili fedha za Serikali zitumike kwa uwazi na ufanisi, huku akisisitiza kuondoa utamaduni wa kuanzisha miradi mipya kabla ya kumaliza ile iliyopo.

Mapema asubuhi akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Ester Matiko, Naibu Waziri wa Maji, Mathew Kundo amesema Serikali inapunguza utitiri wa kuanzisha miradi mipya kwa lengo la kukamilisha iliyopo kwanza.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo amehoji ni kwa namna gani Serikali itasaidia kuanzisha mradi mpya utakaowezesha wananchi wa Tarime Mjini waweze kupata maji ya kutosheleza ambacho ni kilio chao.