Dodoma. Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, amewataka wabunge wenzake kuchangia mapendekezo ya mpango wa Serikali kwa uwazi na bila kificho, akisisitiza kuwa wabunge wanalindwa na sheria wanapotekeleza majukumu yao ya kikatiba.
Waitara amesema hana tatizo kutamka wazi mbele ya Bunge kuwa katika jimbo lake kuna watu watatu waliopotea na hadi sasa haijulikani walipo.
Ameeleza kuwa kusema ukweli hadharani si kosa, mradi kunafanywa kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Februari 3, 2026, wakati akichangia mapendekezo ya mpango wa Serikali bungeni.
Amesema alishangazwa na taarifa alizozisikia hivi karibuni kuwa baadhi ya wabunge walichangia hoja bungeni kisha ikadaiwa kuwa wanapaswa kuhojiwa kwa kauli zao.
“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi ni mbunge kwa kipindi cha tatu. Nimezisoma kanuni za Bunge, kanuni za maadili pamoja na Katiba ya nchi, na ninafahamu ninachokisema. Nikikosea, nipo tayari kuitwa Kamati ya Maadili au sehemu nyingine zinazohusika, lakini kusema wazi siyo dhambi,” amesema Waitara.
Bila kuwataja wahusika, amewataka wote wanaohusika kuruhusu Bunge lifanye kazi yake kwa uhuru, akionya kuwa masuala nyeti hayawezi kujadiliwa kwa kificho au kwa kauli zisizo wazi.
Mbunge huyo amesema ni muhimu Bunge likatunge sheria kali dhidi ya watu wanaokiuka misingi ya utawala bora.
Ameongeza kuwa wabunge wanapogusa masuala ya utawala bora, wanapaswa kuwa wazi na kwamba majibu ya Serikali yanayotolewa yahusishe uwazi na yawasilishwe hadharani ili wananchi waelewe kinachoendelea.
“Humu ndani tuliorudi ni takribani asilimia 30 pekee, hao asilimia 70 wako wapi? Ninyi mlioingia humu tambueni kuwa kikulacho kinguoni mwako. Fanyeni kazi ya wananchi iliyowaleta,” amesisitiza.
Kwa upande wa jimbo lake, Waitara amesema hana wasiwasi kwa wananchi anaowaongoza kwa sababu wanamfahamu vyema na anabaki kuwa yuleyule wa siku zote.
Kuhusu mpango wa Serikali, amesema Tanzania haijawahi kukosa mipango, akibainisha kuwa ipo mingi iliyopo kwenye makabati, lakini changamoto kubwa imekuwa ni utekelezaji.
Ameeleza kuwa ni wakati sasa wa kuhakikisha mambo yanayopangwa yanazingatiwa kwa umakini ili mipango isiendelee kubaki kwenye makaratasi bila kutekelezwa.
