ACT yatoa msimamo, ZEC ikitangaza kuteketeza nyaraka za uchaguzi

Unguja. Wakati Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikiidhinisha kazi ya kuteketeza nyaraka zote zilizotumika katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025, chama cha ACT-Wazalendo kimesema huo ni mpango wa kuendelea kuchelewesha haki na kuteketeza ushahidi.

Hilo linatokana na chama hicho kufungua kesi za uchaguzi katika majimbo 25 ya uwakilishi, kikipinga matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 29, 2025.

ACT-Wazalendo kinasema kuharibu ushahidi kwa jambo lililopo mahakamani ni kosa la jinai.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, Februari 3, 2026, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, amesema uamuzi wa kuteketeza nyaraka hizo umefikiwa baada ya kukamilika kwa muda wa siku 90 tangu kumalizika kwa uchaguzi bila kupokea zuio lolote la mahakama linalozuia utekelezaji huo.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha tume kilichofanyika Februari 2, 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unakamilika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo, kwa mujibu wa tume hiyo.

Hata hivyo, Jaji Kazi amesema hatua hiyo inafanyika kwa kuzingatia kifungu cha 98(3) cha Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018.

β€œKifungu hiki kinaitaka ZEC kuharibu nyaraka zote zinazohusiana na uchaguzi mkuu baada ya kupita siku 90 tangu kukamilika kwa uchaguzi husika,” amesema Jaji Kazi.

Kwa mujibu wa Jaji Kazi, kabla ya kuidhinisha utekelezaji wa kazi hiyo, tume ilijiridhisha kuwa hakuna amri yoyote ya mahakama inayozuia utekelezaji wa hatua hiyo, hali iliyoiwezesha kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria baada ya kukamilika kwa muda uliopangwa.

Hivyo, amewataka wadau wote wa uchaguzi kushirikiana katika utekelezaji wa kazi hiyo ili kuhakikisha inafanyika kwa mafanikio, uwazi na kwa kuzingatia kikamilifu misingi ya kisheria na taratibu zilizowekwa.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Ismail Jussa, amesema ZEC imeamua kujificha kwenye kifungu hicho huku ikijua ni kosa la jinai kuharibu ushahidi wakati kuna shauri la kisheria linaloendelea mahakamani.

Akizungumza leo, Jumatano Januari 4, 2026, na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho eneo la Vuga, Zanzibar, amesema chama hicho kilifungua kesi 25 ambazo ziko mahakamani na kwamba nyaraka hizo ni muhimu kwa ushahidi, hivyo hazipaswi kuteketezwa kwani huenda zikahitajika mahakamani.

β€œKwa tume ya uchaguzi ambayo yenyewe imetumia nyaraka hizo katika utetezi wake na inafahamu kuwa nyaraka hizo kwa vyovyote iwavyo zitahitajika katika mashauri yaliyopo mahakamani, kutumia kifungu kilichotajwa hapo juu ili kuziteketeza ni kutumia sheria kwa nia ovu na ni kuharibu ushahidi kwa makusudi,” amesema Jussa, na kuongeza;

β€œZEC inafahamu fika, kwa sababu ni sehemu ya wadaiwa kwenye mashauri yetu yaliyoko mahakamani, kuteketeza nyaraka hizi sasa siyo utaratibu wa kisheria, ni uhujumu wa ushahidi.”

Kutokana na hali hiyo, Jussa amesema chama hakitakaa kimya wakati haki za wananchi wa Zanzibar na demokrasia vikiendelea kuchanwa na kutupwa, huku kikitaka mambo matatu yatekelezwe.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kusimamishwa mara moja amri ya uteketezaji wa nyaraka hizo hadi mashauri yote yaliyopo mahakamani yatakapomalizika.

β€œMsajili wa mahakama kuu anapaswa ashughulikie maombi yetu ya ukaguzi wa nyaraka kwa haraka, na tunatoa wito kwa mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha nyaraka zote za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinatunzwa chini ya ulinzi madhubuti ili kuzuia upotevu,” amesema Jussa.

Akifafanua kuhusu madai ya ACT-Wazalendo, Jaji Kazi amesema hakuna walichofanya kinyume na sheria.

Amesema hadi sasa hawajapokea zuio lolote la mahakama linalowataka wasiteketeze nyaraka hizo kwa mujibu wa sheria.

Jaji Kazi amesema kosa la ACT-Wazalendo ni kutokwenda mahakamani kuomba zuio la kuteketezwa kwa nyaraka hizo, kama sheria inavyoelekeza, kabla ya kufungua kesi.

Amesema kifungu cha 98(3) kinaelekeza kuteketezwa kwa nyaraka hizo isipokuwa kama itaelekezwa vinginevyo na mahakama kutokana na kesi za uchaguzi.

β€œWao walijisahau kuomba zuio la mahakama, kwa hiyo siku 90 ziliisha Januari 29, na jana tulikaa kikao cha ZEC na wanasheria wetu wakatuhakikishia kuwa hakuna zuio lolote, hivyo kikao kikaamua kuendelea kutekeleza matakwa ya sheria,” amesema jaji huyo.

Ameongeza, β€œHakuna uovu wowote tuliofanya wala sheria iliyokiukwa. Kama tusingefanya hivi, basi sisi ndiyo tungekuwa tunakwenda kinyume na sheria.”