Ahadi ya Sh200 bilioni zitaakisi fursa au changamoto kwa wafanyabiashara wadogo?

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikijiandaa kutangaza utaratibu wa namna wafanyabiashara wadogo watakavyonufaika na Sh200 bilioni zilizoahidiwa kutolewa ndani ya siku 100 na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, walengwa na wadau mbalimbali wameibua hofu na mapendekezo kuhusu namna bora ya utekelezaji wa mpango huo.

Miongoni mwa hoja zinazojitokeza ni ugumu wa upatikanaji wa mikopo, urasimu katika usajili wa wafanyabiashara wadogo, pamoja na matumizi ya sera, kanuni na sheria ambazo kwa nyakati zilizopita zimeonekana kukwama katika utekelezaji.

Wadau wanasema ni muhimu Serikali ijifunze kutokana na uzoefu wa mipango ya awali ili fedha hizo ziwafikie walengwa halisi.

Ahadi ya utoaji wa Sh200 bilioni ilitolewa na Rais Samia alipokuwa akiomba ridhaa ya wananchi kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka jana.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa kabla ya kuanza kwa utoaji wa mikopo hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ameiambia Mwananchi leo, Jumatano Februari 4, 2026, kuwa utaratibu wa utoaji wake utatangazwa siku chache zijazo kupitia mkutano na waandishi wa habari.

“Siku chache zijazo, kutafanyika mkutano wa waandishi wa habari kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha ili kutoa maelezo ya kina kuhusu namna fedha hizi zitakavyotolewa,” amesema Nanauka.

Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, kutoa taarifa kwa umma kuhusu fursa hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa Januari 30, 2026, Dk Gwajima aliwahamasisha wafanyabiashara wadogo kuchangamkia mikopo ya Serikali yenye masharti nafuu na riba ya asilimia saba kwa mwaka, inayotolewa kupitia benki ya NMB ambayo imeingia makubaliano na Serikali kusimamia mikopo hiyo.

Mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo ndogo wenye mauzo ghafi yasiyozidi Sh4 milioni kwa mwaka, wakiwamo mama na baba lishe, machinga, waendesha bodaboda wa magurudumu mawili, matatu na guta, pamoja na makundi mengine yanayotambuliwa na kusajiliwa na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali nchini.

Ili mfanyabiashara anufaike na mikopo hiyo, anatakiwa awe ametambuliwa na kusajiliwa katika Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Wafanyabiashara Wadogo (WBN-MIS) kupitia ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri husika.

Aidha, mwombaji anatakiwa awe raia wa Tanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18, awe na biashara inayotambuliwa katika eneo lake, pamoja na kuwa na Kitambulisho cha Taifa (Nida) au namba ya kitambulisho hicho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utaratibu wa kuomba mikopo ni wazi na rafiki. Mwombaji mwenye kitambulisho cha kidijitali au namba ya Nida anatakiwa kwenda katika tawi la benki ya NMB, kujaza fomu ya maombi na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika.

Maombi hufanyiwa uhakiki na uchambuzi kwa mujibu wa taratibu za benki, na waombaji wanaokidhi vigezo huingiziwa fedha kwenye akaunti zao kulingana na aina ya mikopo waliyoomba.

Mikopo hiyo itarejeshwa ndani ya miezi mitatu hadi 24, kulingana na aina ya biashara. Riba ni asilimia saba kwa mwaka na mkopo umewekewa bima dhidi ya kifo na ulemavu wa kudumu kwa mkopaji, kwa lengo la kumlinda mfanyabiashara na familia yake.

Baadhi ya wafanyabiashara wadogo, wakiwamo machinga, mama lishe na waendesha bodaboda, wamesema licha ya kutambua umuhimu wa mpango huo katika kuwawezesha kiuchumi, bado changamoto ya kutambuliwa na kuingizwa kwenye mifumo rasmi ni kikwazo kikubwa.

Mfanyabiashara mdogo wa Kariakoo, Rashid Mohamed, amesema wengi wao hawana elimu ya kutosha kuhusu mifumo ya kifedha na urasimishaji, hali inayowafanya kuogopa kusajiliwa kwa kuhofia kodi, tozo na masharti magumu ya mikopo.

“Serikali inasema kuna Sh200 bilioni za mitaji, lakini sisi tunajiuliza tutazipataje ikiwa hatuelewi hata mfumo wenyewe unafanyaje kazi,” amehoji.

Kwa upande wake, Eva Patrick, mama lishe wa eneo la Buguruni, amesema mikopo mingi huwa na nia njema, lakini utekelezaji wake hauzingatii mazingira halisi ya kazi za wafanyabiashara wadogo.

Amesema wengi wao hawana utaratibu wa kutunza kumbukumbu rasmi za mauzo, jambo linalowafanya waonekane hawakidhi vigezo vya kupewa mikopo.

“Tunaweza kunufaika na mikopo hii, lakini masharti yakizidi ugumu, tutabaki pale pale na kuendelea kukopa vikoba au mikopo ya riba kubwa,” amesema.

Naye dereva wa bodaboda, Hamad Ngonyani, amesema kuingizwa kwenye mifumo rasmi kuna faida ya kupata mitaji na bima, lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa taarifa sahihi kwa walengwa.

“Wengi wetu hatujui hata tuanzie wapi. Kama taarifa hizi hazitafika vizuri chini, haitatofautiana na mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri ambayo imekuwa ikiwafikia wachache,” amesema.

Akizungumzia suala hilo, mdau wa biashara, Profesa Haji Semboja, amesema kila awamu ya uongozi inakuja na mikakati ya kuwawezesha vijana na wafanyabiashara wadogo, lakini mingi imekwama kutokana na changamoto za utekelezaji.

Ameshauri Serikali ijifunze kutokana na mipango iliyopita kwa kutumia mifumo iliyopo tayari ikiwemo sera, sheria, kanuni na taasisi, badala ya kuanzisha mifumo mipya.

“Tusitafute vitu vipya wakati tuna mifumo inayofanya kazi. Mara nyingi fedha hizi zimekuwa zikiishia kwa wasiostahili. Ni muhimu kuhakikisha fedha hizi zinawafikia walengwa halisi ili kuepuka kurudia makosa ya nyuma,” amesema Profesa Semboja.