Bodi ya Mfuko wa Barabara kutumia zaidi ya Sh983 bilioni huduma za barabara

Dodoma. Jumla ya Sh983.9 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kufadhili miradi ya matengenezo ya barabara nchini.

Fedha hizo zimetengwa kwa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) na zitakwenda kwenye matengenezo ya barabara kwa asilimia 100 ya mahitaji ya fedha za matengenezo ili kuzilinda zisiharibike.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Rashid Kalimbaga, ametoa kauli hiyo leo, Jumatano, Februari 4, 2026, akisema vipaumbele vya matengenezo ya barabara huwa vinafanywa na wakala wa barabara husika.

Kalimbaga amesema jukumu la RFB ni kutoa fedha za matengenezo ya barabara na kufuatilia matumizi yake, ili kuhakikisha kama matengenezo yanafanyika kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa.

Kalimbaga alitamka kuwa kati ya miaka ya fedha 2019/20 na 2024/25, mapato ya bodi yameongezeka kutoka Sh841.5 bilioni hadi Sh1.2 trilioni, ambalo ni sawa na ongezeko la Sh382 bilioni, sawa na asilimia 45.

“Ongezeko la mapato limesababishwa na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ufanisi wa bandari, lakini pia uwepo wa amani na utulivu nchini na katika nchi za jirani zinazotumia bandari zetu,” ameeleza.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, vyanzo vya mapato ya Mfuko wa Barabara ni pamoja na tozo ya mafuta (fuel levy), tozo ya magari (transit charges), na tozo ya kuzidisha uzito wa magari (overloading charges).

Amesema tozo ya mafuta huchangia zaidi ya asilimia 97 ya mapato ya mfuko, ambapo Sh263 hutozwa kwa kila lita ya petroli na dizeli.

Vilevile, amesema bodi inaendelea kufanya tafiti kwa lengo la kuongeza vyanzo vya mapato ya mfuko ili kuimarisha uwezo wake na ufuatiliaji wa makusanyo ya mfuko kutoka kwenye vyanzo vilivyopo.