Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini kushirikiana kwa karibu na madiwani katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani, akisema hatua hiyo ni msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri.
Itunda ametoa agizo hilo leo Jumatano, Januari 4, 2026, alipokuwa akifungua kikao cha robo ya pili cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, kilichojadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema mapato ya ndani ndiyo nguzo muhimu ya halmashauri kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa watendaji na madiwani kushirikiana kikamilifu ili kuongeza makusanyo hayo.
“Endeleeni kushirikiana na waheshimiwa madiwani katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani, kwa kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kila halmashauri unategemea kwa kiasi kikubwa makusanyo ya ndani,” amesema Itunda.
Amesema Serikali imewekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati mkoani Mbeya na maeneo ya jirani, ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma mkoani Songwe, ambapo zaidi ya Sh bilioni 185 zimetolewa.
Kwa mujibu wa Itunda, kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa za kiuchumi, kuimarisha biashara na kuunganisha mataifa mbalimbali kupitia Barabara Kuu ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia (TANZAM).
Amesema sambamba na mradi huo, Serikali inatekeleza pia mradi wa kimkakati wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira.
“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mbeya. Tayari ujenzi wa barabara ya njia nne eneo la Uyole umeanza, lami ikimwagwa, jambo linaloonyesha dhamira ya Serikali katika kuboresha miundombinu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Itunda amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, Erica Yegella, kwa kufanikisha ukusanyaji wa asilimia 100 ya mapato ya ndani, akieleza kuwa ni mafanikio makubwa kwa halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vijijini, Erica Yegella akitoa taarifa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani. Picha na Hawa Mathias
“Nitumie fursa hii kumpongeza dada yangu Mkurugenzi Erica kwa kufanya vizuri katika makusanyo ya mapato ya ndani, jambo litakalowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati,” amesema.
Amesisitiza kuwa ni wakati sasa kwa watendaji na madiwani kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuongeza ufanisi na kufikia hatua kubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini, Erica Yegella, amesema siri ya mafanikio katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ni ushirikiano mzuri baina ya uongozi, watumishi na madiwani.
“Tutaendelea kushirikiana kikamilifu bila vikwazo katika kukusanya mapato ya ndani, sambamba na kusimamia utekelezaji wa miradi katika sekta za elimu, afya, barabara na vipaumbele tulivyoviainisha,” amesema Yegella.
Naye Diwani wa Utengule Usongwe, Aida Haule, amesema madiwani wataendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani na Serikali Kuu ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inazingatiwa.
“Tutasimamia kwa karibu matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali au zinazokusanywa ndani ya halmashauri ili miradi inayotekelezwa iendane na kiwango cha fedha kilichotengwa,” amesema.
Aida, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, amesema katika kutekeleza majukumu yake atahakikisha anafikika kwa wananchi na kushirikiana na uongozi uliopo kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.