erikali yaonya makondakta daladala wanaotesa wanafunzi vituoni

Dodoma. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ametoa maagizo matano kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ili kutatua changamoto za usafiri wa wanafunzi nchini.

Maagizo hayo yanatokana na malalamiko yaliyotolewa na mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam, kupitia kipande cha video akielezea adha wanayokutana nayo kwenda shule na kurudi nyumbani.

Mwanafunzi huyo anaeleza makondakta wamekuwa wakigoma kuwabeba kwa kisingizio cha kibiashara wakidai wanafunzi hawalipi nauli kamili. Bei ya wanafunzi ni Sh200.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wanalazimika kusimama barabarani kwa muda mrefu wakisubiri usafiri, wanachelewa kufika shuleni, na wakati mwingine wanashindwa kabisa kufika shuleni.

Hali hiyo inawatia hofu wanafunzi, inawachosha, na inaathiri masomo yao, pamoja na usalama wao kama watoto.

Pia, wanafunzi wanategemea daladala kama njia yao kuu ya usafiri, hivyo wanapoachwa njiani au kunyimwa huduma wanakuwa kwenye mazingira hatarishi, na kunyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu kwa usalama.

Kutokana na kadhia hiyo, leo Jumatano, Februari 4, 2026, Waziri Mbarawa amekutana na waandishi wa habari jijini Dodoma kuzungumzia malalamiko hayo na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.

Profesa Mbarawa amemsukuru mwanafunzi huyo kwa kupaza sauti kwa niaba ya wanafunzi wote nchini hususan wa mijini ambako ndiko wanatumia zaidi usafiri wa daladala.

Amesema Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kuwa ni watoa huduma za usafiri wa abiria baina ya miji, mijini na vijijini, ikiwa ni pamoja na daladala zinazotoa huduma mijini.

Amesema ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa huduma hizi zinaimarika kila wakati kupitia jukumu walilopewa LATRA kisheria. Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wote wanaokiuka taratibu na kanuni za usafiri, bila kujali nafasi zao.

Waziri huyo amesema katika kukabiliana na changamoto za usafiri wa abiria wakiwemo wanafunzi na kuboresha usafiri wa wanafunzi mijini, Serikali imeweka mipango na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma za mabasi maalumu yaendayo haraka kwa ajili ya wanafunzi, hususan katika nyakati za asubuhi na jioni, ili kuhakikisha wanafunzi wanafika shuleni na kurejea majumbani kwa usalama na kwa wakati.

Kutenga mabehewa maalumu kwa ajili ya wanafunzi kwenye treni za mijini (Dar es Salaam), hatua inayolenga kupunguza msongamano, kuongeza usalama na kutoa unafuu wa usafiri kwa wanafunzi wanaotumia treni za mijini.

Pia, kurasimisha na kusimamia utozaji wa nauli maalumu ya Shilingi 200 kwa wanafunzi katika mabasi yaendayo haraka na daladala, kwa mujibu wa taratibu na kanuni zilizowekwa. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata huduma hizi kwa gharama nafuu; na

Vilevile kutekeleza Sheria na Kanuni za Kuthibitisha Madereva na Kusajili Wahudumu (Makondakta) wa vyombo vya usafiri wa umma wa mabasi na treni.

Amesema hatua zote hizi zinalenga kutekeleza malengo ya Serikali ya kuboresha huduma za kijamii, hususan huduma za wanafunzi katika vyombo vya usafiri, ili kuwawezesha kupata elimu katika mazingira rafiki na yenye staha.

Profesa Mbarawa amesema katika kuhakikisha utekelezaji mzuri wa hatua hizi, pamoja na kujibu changamoto zilizowasilishwa na mwanafunzi Mariana, ninaagiza Latra kutekeleza yafuatayo: kuhakikisha zoezi la kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu (makondakta) kwenye mabasi linafanywa kwa kasi katika miji yote nchini, na kutoa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria kwa madereva na makondakta watakaobainika kuwanyanyasa wanafunzi;

Kuimarisha udhibiti wa nauli maalumu za wanafunzi, staha ya huduma na usalama wao kwa wakati wote.

Kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma, na watumia huduma wajue haki na wajibu wa kila mmoja.

Kuhakikisha treni za abiria, daladala zote nchini pamoja na mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani zimeandikwa namba za bure ili abiria waweze kupiga Latra.

Kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza kwenye vituo vya daladala hasa nyakati za asubuhi na jioni kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri.

Aidha, ametoa rai tena kwa wamiliki wa daladala kuwakumbusha watumishi wao kuzingatia sheria na kanuni wanapotoa huduma za usafiri kwa wanafunzi ili kujiepusha na hatua zitakazochukuliwa dhidi yao pale wanapovunja sheria husika.