Dar es Salaam. Wananchi wa Tabata, jijini Dar es Salaam bado wanaishi katika sintofahamu huku wakilazimika kuvumilia vumbi linalotoka kwenye barabara mbovu zilizopo katika mitaa yao na wakati wa mvua wakilazimika kupita katika maji na matope yaliyotuama barabarani.
Licha ya mikataba ya ujenzi wa barabara tofauti katika eneo hilo kusainiwa kwa ajili ya utekelezaji chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu Dar es Salaam awamu ya Pili (DMDP 2), hali bado tete.
Mkataba huo ulisainiwa Februari 20, 2024 lakini hadi sasa wakazi wa maeneo ya Kimanga na Migombani wanasema hawaoni dalili za mabadiliko, hali inayozidi kuathiri biashara na usafiri.
Barabara ya Tabata Kisiwani- Mawenzi ambapo baadhi ya nyumba zimeanza kuwekewa alama mbalimbali za mradi wa DMDP.
Wananchi wanalazimika kuvumilia mashimo, vumbi kali na kukosekana kwa mitaro, wakijiuliza ni lini ahadi ya uboreshaji wa barabara hizo itageuka kuwa uhalisia.
Mkataba wa ujenzi wa barabara za Tabata kwa kupitia mradi wa uboreshaji wa miundombinu Dar es Salaam (DMDP) ulisainiwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) nchini, Nathan Belete Februari 20, 2024.
Mkataba huo waliotia saini ulikuwa ni mkopo wa Sh1 trilioni kutoka benki hiyo uliolenga uboreshaji wa miundombinu Dar es Salaam awamu ya Pili (DMDP 2).
Kwa mujibu wa mkataba huo ambao utekelezaji wake ni wa miaka sita katika mwaka wa fedha 2024/25, asilimia 78 ya fedha hizo zitatekelezwa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara na masoko.
Katika Jiji la Dar es Salaam (Ilala) zinajengwa jumla ya kilomita 29.8 zikijumuisha barabara za Tabata zikiwemo barabara za Migombani kilomita 1.57, Tabata Mawenzi–Kisiwani kilomita 2.12.
Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kudai barabara za Kimanga zimeendelea kuwa mbovu na kutokuwepo kwa mitaro chanzo kikiwa kimesababisha mashimo kipindi cha mvua na vumbi wakati wa jua kali.
Akizungumza na Mwananchi Januari 30, 2026, mfanyabiashara wa nguo, Khalid Ally amesema eneo hilo limekuwa ni kero na vumbi kwa wafanyabiashara na wapo wanaofunga maduka kutokana na kutokuwepo kwa biashara.
Barabara ya Kimanga ambayo imekuwa ikilalamikiwa na watumiaji wa njia hiyo ikiwa imewekewa tope jeusi kuziba shimo lililokuwa linasumbua eneo la Savanna.
“Biashara matangazo unatamani kuweka mfano wa nguo nje lakini ukifikiria vumbi la hapa inakuwa ngumu, biashara kwetu imeshakuwa na changamoto jambo ambalo linatukatisha tamaa,” amesema Ally.
Dereva wa daladala ya Tabata Kimanga hadi Muhimbili, Salehe Nyembo amesema kwa sasa baadhi ya wamiliki wameamua kuhamisha njia za magari yao baada ya kuona barabara haiwalipi.
“Sasa hivi ukifuatilia daladala kwenye njia hii zipo chache, kwa sasa zinatumika bajaji na pikipiki. Wamiliki wengi wamebadilisha route kama gari za Tandika, Ubungo na Kinyerezi zinaendelea kupungua kwa sababu ya ubovu wa barabara,” amesema Nyembo.
Amesema ubovu huo umewapa fursa wapiga debe wakikosa pesa wanaingia mitaani kutafuta vifusi vya tofali au matope kuweka barabarani ili kupata chochote kitu kutokana na hali hiyo hata kukiwa na mashimo hakuna anayejali.
Nyembo amesema tangu walivyosikia barabara hiyo itafanyiwa marekebisho hadi kufikia mwaka 2026 hawaoni dalili zaidi ya kukwanguliwa endapo mashimo yatazidi.
Naye, Naomi Mmbando, mkazi wa Migombani amesema hali iliyopo kwa sasa ni kutokuwepo kwa mifereji ya kupitisha maji ya mvua hivyo kukosekana kwa mwelekeo sahihi wa maji hayo.
“Watu wanasema ukanda huu una maji, laiti kungekuwa na mifereji maji yangeelekea kwenye uelekeo wake lakini hakuna, mwisho wa siku yanazagaa mitaani na kwenye nyumba za watu,” amesema Naomi.
Akizungumza na Mwananchi, Februari 1, 2026 Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geoffrey Mkinga amesema katika eneo hilo kuna changamoto ya fidia kwa wale watakaopitiwa na mradi.
“Tukianza kazi bila kuwalipa fidia kutakuwa na kelele nyingi kuliko zinazungumzwa sasa hivi,” amesema.
Hali ya barabara ya Migombani -Segerea ilivyo kipindi hiki cha Februari 2026.
Amesema tayari wameshaanza kufanya maandalizi ya kulipa fidia ya maeneo hayo ili utekelezaji utakapoanza usiwe wa kusuasua kwani wanatamani kazi iendelee kufanyika na mkandarasi hajakaa tu, anaendelea na kazi zake muhimu.
Kutokana na hilo amesema kuanzia Februari 2, 2026 kutakuwa na uhakiki wa fidia na baada ya kujihakikishia kutokana na akiba iliyopo wataanza kulipa na kazi kuendelea.
Pia, Mkinga amesema changamoto nyingine ni kwamba kuna mtaa umepitishwa bomba kubwa hivyo wanaangalia namna ya kufanya ili isiwaathiri watu wa maeneo husika.
“Wito wetu ni ili kazi zisiwe zinachelewa, maana hiyo waache kuvamia maeneo ya barabara kwa kuongeza kidogo kidogo ikiwemo vibanda maana mwisho wa siku tunapotaka kufanya maendeleo watu wamejaa kwenye korido ya barabara,” amesema Mkinga.
Amesema haifai kwa watu kupunguza ukubwa wa barabara kwa kuongeza vibanda jambo ambalo si sawa, mwisho wa siku utekelezaji wa mradi unakuwa mgumu kwa sababu watu wamevamia eneo la barabara na inapotakiwa kuvunja wanaona wanaonewa.
Hivyo, amesema wanashughulika na jambo hilo kwa taratibu ili kujua kuna malalamiko ya aina gani ili maendeleo yawe baraka badala ya laana.
