FYATU MFYATUZI: Kama miwaya inakula umeme kwa nini umeme usiile miwaya?

Juzi, nilishangaa nusura nife. Si kuna eti utafiti uliofanywa kubaini kwanini umeme unatumika haraka hata kama vifaa vyote vimezimwa! Uliona wapi zaidi ya kwa mafyatu tu? Hapa bado hujasukuti juu ya kuisha muda wa matumizi ya bando la simu.

Kweli bando linaisha au linaishishwa ili kuwafyatua mafyatu waliokataa kufyatuka wakafyatua hadi wanafyatuliwa na kila jizi na zwazwa? Hamuoni wachukuaji wakiitwa wawekezaji wawekezao hila za kuwafyatua mafyatua? Ufyatuzi huu haukuanza jana wala juzi. Jikumbushe skandali ya mikataba ya kampuni jizi la Ipielo enzi za ruxa wakati jamaa wa Msonga akiwa waziri wa nishati.

Kama haitoshi, jikumbushe kashfa ya NBC na ABSA na shemejize Ben. Pia, jikumbushe kashfa mama za Escrew, Kagoda, Mwanakaya Memetuka na nk. wakati wa jamaa wa Msonga. Ukitoka hapo, njoo wakati wa Jiwe ni ile kashfa ya Chatolite ingawa haikupigiwa upatu tokana na kumuogopa mwamba. Kwani, Chatolite ina tofauti gani na Gbadolite ya Kukungbenduwazambanga?

Japo ya kale hayanuki, wakati mwingine hunuka. Bila kujua ya kale, inakuwa vigumu kujua ya leo yapo kwa sababu gani. Turejee ufyatuaji wa kizwazwa. Sijawahi kuelewa mfano kusikia eti miwaya inaweza kusababisha bili za umeme kupanda.

Kwanini haisababishi kushuka? Nilishangaa kusikia eti miwaya isiyopaswa kubeba umeme ilibeba umeme. Kwani, umeme ni maji? Maana, hata kama miwaya ilibeba bila kutumika, umeme ungebaki pale pale. Kwani, kazi ya miwaya ni nini? Hata ukichukua hiyo miwaya ukauganisha kwenye mti, bado bili ya umeme haitaongezeka vingenevyo kuna uchawi.

Hivi miwaya kweli inakula umeme au tunafyatuliwa sababu ya uzwazwa au kukosa ufyatukaji wa kuwafyatua wanaotufyatua? Kesho, bili za maji zitaongezeka. Tutaambiwa sababu ya ni aina ya mabomba yaliyotumika. Hebu tujiuize kifyatu. Nani anamilki mitandao ya miwaya inayoingiza umeme kwenye mbavu zetu za mbwa?

Hamjasikia mafyatu wakilalamika. Mabomba hayatoi maji lakini bili zinakuja. Huenda hata taa nazo zikizimwa zinaendela kula umeme tu au umeme unakula taa. Da! Mmejua kutufyatua!

Hii ni dharau na roho mbaya sina mfano. Mmetuletea miluku kutubana ilhali sirkal haiitumii. Hamkutosheka! Sasa mnasingizia hata miwaya! Tutajuaje kama kesho, hatutaambiwa kuwa hata matone ya mvua yakigusa miwaya au kunguru kutua juu yake vinapaisha bili? Nimekumbuka. Ndiyo maana juzi nilimuta mghoshi Machungi akiwa na manati anawinda kunguru wasitue kwenye nyaya ili wasimuongezee bili.

Hakuna kitu huniumiza nikatamani nifyatuke na kufyatua kama namna kila tapeli tena zwazwa, awe wa ndani au nje, anavyoifyatua Fyatuliand. Yaani, mashirika mengi tunayoita ya kiwekezaji ni ya kichukuaji. Kama yanawekeza, basi ni kwa wale walioyawekeza yakawekea njuluku kwenye akaunti zao fichi. Wanachota toka kwa mafyatu na kutajirika na kuondoka na kutuachia umaskini.

Daima, nawaza kifyatu. Mfano, inakuwaje mafyatu wanene wanatumia njuluku za mafyatu kapuku kujenga miradi halafu wanaita wachukuaji, sorry, wawekezaji waiendeshe? Inakuwaje lisrikal lijiingize kwenye biashara hii ya kichawa, sorry, kichaa? Au ni kwa vile wanene waneemeka kwa kuwafyatua mafyatu waliogoma kufyatuka wakafyatua hadi wanafyatuliwa na kila atakaye kuwafyatua?

Sitashangaa kwenda kituo cha wese nikajaziwa hewa na kuambiwa kuwa tatizo ni aina ya mkweche ninaoendesha. Sijui itakuwaje na Bi Mkubwa akianza kunifyatua njuluku akisingizia mkoba anamoziweka.

Hebu tuwe serious kidogo. Inawezekana kweli bando likaisha au kuisha muda wa matumizi wakati siyo bidhaa inayoisha? Inawekezekanaje bili kupanda bila umeme kutumika? Baya zaidi, mijizi inapanga tarehe ya kuisha bando kana kwamba ni chakula au inajua unvyotumia. Tunamfyatua nani na kwanini yarabi au tumeishiwa ubunifu wa kutengeza njuluku? Bando ni data.

Siyo chakula wala dawa ifikie mwisho wa matumizi yake. Hapa Ukanadani sijawahi kusikia kitu hiki. Ukitaka kuwafyatua mafyatu wa hapa kizwazwa kama hivi, wanakufyatua, kukutoa kwenye ulaji na kukufungulia mashtaka.

Kama hatutazuia ujambazi huu, anaweza kutokea munene akashirikiana na makampuni ya kutengeneza bidhaa kama baiskeli, magari, hata nguo na kuambiwa kuwa nazo zina mwisho wa matumizi ili kuwalazimisha mafyatu kununua bidhaa hizi. Kama bando linakuwa na mwisho wa kutumika, mbona simu hazina? Chondechonde mswambie mafyatu kuwa na watumiaji wa simu nao wana mwisho wao wa matumizi.

Mkimaliza, mtawafyatua mafyatu. Mtadai kuwa na runinga zao zina mwisho wa matumizi! Yote fanyeni. Msijetwambia kuwa hata njuluku tulizo nazo zinaexpire. Kama vyote vinaexpire, natamani waanze hawa wanaotufyatua na kutuchezea shere kana kwamba sisi ni hamnazo kwa sababu tumegoma kufyatuka na kuwafyatua ili kuwaachisha kutufyatua tena kizwazwa.

Natamani niandamane. Hata hivyo, naongopa ndata wasinigenzii, wasiojulikana wasiniteke, kunipoteza na kuninyotoa roho. Naonya. Ukija kuniteka, nakuteka, nakupoteza, na kukudedisha kwa vile nisipofanya hivyo, nitafanyiwa. Hii huitwa self-defense kisheria.

Nionye. Asitokea fyatu yoyote akadai kuwa na Bi Mkubwa wangu amefikia mwisho wa matumizi. Kama hiyo inawezekana, basi kamwambia Bi Mkubwa wenu anayewaruhusu mfyatue vitu vya hovyo na kizwazwa kama hivi. Nimesemaje? Kumbe niko Mirembe!!