Unguja. Wakati wananchi na wakazi wa nyumba za Kikwajuni Mjerumani, Mkoa wa Mjini Magharibi wakiwa bado na malalamiko kuhusu mikataba ya kuondolewa katika eneo hilo, Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), limesema litaanza kuzibomoa nyumba hizo Machi 26, 2026, kupisha utekelezaji wa mradi wa mji wa kisasa.
Wananchi hao wamesema mikataba waliyopewa na Shirika la Nyumba haina vigezo vya kutosha, licha ya baadhi yao kuitwa kwenda kusaini, wakibainisha kuwa baadaye waligundua inaweza kuwageuka kutokana na kukosa vipengele muhimu vya kisheria.
Eneo hilo lina jumla ya nyumba 150 zilizojengwa na Wajerumani wakati wa kipindi cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume na kugawiwa wananchi bila malipo. Kati ya nyumba hizo, 99 zinamilikiwa na ZHC huku 51 zikiwa ni mali binafsi.
Hata hivyo, katika mipango ya serikali ya kuendeleza miji na kujenga nyumba za kisasa kutokana na uchakavu wa nyumba hizo kupitia Shirika la Nyumba Zanzibar, eneo hilo linatarajiwa kukabidhiwa kwa mwekezaji anayetarajiwa kujenga nyumba zaidi ya 1,150.
Katika makubaliano yaliyopo kati ya ZHC na wananchi wanaoishi katika nyumba hizo, imeelezwa kuwa wananchi watapatiwa fedha za kujikimu kwa kipindi cha miaka miwili wakati mradi ukiendelea, kisha watapatiwa nyumba za kuishi katika eneo hilo baada ya mradi kukamilika. Hata hivyo, ujenzi wa mradi huo umetajwa kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja.
Akizungumza na Mwananchileo JumatanoFebruari 4, 2026, Katibu wa Kamati ya Kusimamia Uondoshwaji katika eneo hilo, Omar Nassor Suleiman amesema licha ya mradi huo kuwa na sifa za maendeleo, bado kuna masuala kadhaa ambayo hayajakaa sawa katika mikataba, hali inayozua hofu miongoni mwa wananchi.
Amesema awali kulikuwapo changamoto za wananchi kutokubaliana na mradi huo, lakini kamati ilishirikiana kwa karibu na serikali kutoa elimu kuhusu uondoshwaji huo, hatua iliyosaidia wananchi kuelewa.
Hata hivyo, amesema changamoto mpya zimeibuka katika hatua ya makubaliano ya mikataba.
Amesema kulikuwapo makundi matatu; la kwanza la wanamapinduzi ambao hawakutaka kuondoka wakihofia kupotea kwa urithi wa Mapinduzi, kundi la pili lililokataa kabisa kuachia nyumba zao na kundi la tatu lenye mtazamo wa maendeleo.
“Tulifanya kazi kubwa kuhakikisha serikali inawapa uhakika wananchi kwamba wataondolewa kwa muda na baada ya mradi kukamilika watarejeshwa. Tulifanya vikao vingi hadi tukakubaliana kuwepo kwa mikataba miwili kwa ajili ya kumlinda mwananchi; mkataba wa kuondoka na mkataba wa kurejea katika eneo husika,” amesema.
Suleiman amesema kwa sasa changamoto kubwa ipo katika suala la mkataba, akieleza kuwa awali, ZHC iliwafungisha wananchi mikataba kupitia masheha, mikataba iliyozungumzia zaidi hati ya malipo ya fidia, jambo ambalo kwao lina maana ya kupoteza haki ya ardhi.
Amesema wananchi wanataka fedha wanazopewa zitambuliwe kama posho za kujikimu katika kipindi chote cha mradi.
Ameeleza kuwa licha ya makubaliano hayo, mikataba ina upungufu unaoashiria uwezekano wa ujanja wa kuwaondosha wananchi bila kuwarejesha baada ya mradi kukamilika. Ameongeza kuwa ZHC inaonekana kutotaka kutoa mikataba ya kisheria itakayowalinda wananchi.
Amesema wananchi wanataka mkataba huo usimamiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na pia, mwekezaji ahusishwe moja kwa moja ili ajue wajibu wake wa kuwarejesha wananchi baada ya mradi kukamilika.
Aidha, wameomba suala la kodi kwa wale watakaorejeshwa liwekwe wazi katika mkataba, likiwa la kawaida na linaloendana na uwezo wa wananchi, badala ya baadaye kuwekewa kodi kubwa ikizingatiwa kuwa nyumba nyingi zitakuwa za kibiashara.
Suleiman amesema mkataba uliopo hauelezi wazi kama mwananchi atarejeshewa nyumba katika eneo husika, bali umeandika tu kuwa atapewa nyumba bila kutaja eneo.
Pia amesema mashuhuda wa mkataba huo hawajumuishi taasisi ya kiserikali wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali, bali umetajwa ZHC na wananchi pekee.
Amesema kipengele kingine kilichokosekana ni kile kinachoeleza iwapo fedha za kujikimu za miaka miwili zitaisha kabla ya ujenzi kukamilika, chanzo cha fedha za ziada kitakuwa ni nini.
“Tunataka kiwepo kifungu kinachoeleza wazi kwamba iwapo miaka miwili itaisha na ujenzi haujakamilika, mjenzi atalazimika kuendelea kutoa fedha za kujikimu hadi mradi ukamilike,” amesema.
Ameongeza kuwa mkataba haujaeleza ukubwa wa nyumba zitakazotolewa baada ya mradi kukamilika, licha ya makubaliano ya awali ya mikutano yao ya kawaida na viongozi wa shirika kwamba kila mwananchi atapatiwa nyumba yenye vyumba vinne.
Ameshauri, ikiwezekana mwekezaji ahusishwe kwenye mkataba ili kuepusha changamoto za baadaye ambapo ZHC linaweza kudai kuwa haihusiki kwa kuwa nyumba zitakuwa mali ya mwekezaji.
“Walikubaliana mikataba isianze kusainiwa hadi kamati na wananchi wote wakubaliane na kusaini kwa pamoja,” amesema.
Akizungumza na Mwananchikuhusu madai hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Habari wa ZHC, Amour Mussa Makame bila kufafanua iwapo mikataba ina kasoro, amesema wananchi wamehusishwa tangu mwanzo wa mchakato huo na vikao vingi vimefanyika, huku baadhi yao wakiwa tayari wameshasaini mikataba na kupokea fedha huku wengine wakiendele kuwekewa kwenye akaunti zao.
Amesema kwa kuzingatia makubaliano hayo, ZHC itaendelea na kazi ya kubomoa nyumba hizo Machi 26, 2026.
Amesema kati ya nyumba zilizopo eneo hilo, 99 ni mali ya ZHC huku 51 zikiwa ni za watu binafsi.
“Serikali imetumia busara kuwalipa wananchi na itawarejesha katika eneo hilo. Miundombinu ya sasa imechoka na majumba ni mabovu, hivyo kuna haja ya kujenga nyumba za kisasa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi,” amesema.
Ameeleza kuwa wengi wa wanaopinga ni wapangaji ambao wamezoea kuishi katikati ya mji, hivyo hawana imani kama kweli watarejeshwa baada ya mradi kukamilika.
Hata hivyo, amesema mpango wa serikali ni kuwarejesha wote kama ilivyokubaliwa.
“Watapewa fedha za kujikimu kwa kipindi cha miaka miwili licha ya mradi kujengwa kwa mwaka mmoja. Pia watapewa kipaumbele katika ujenzi wa nyumba za kurejea ambazo zitajengwa kwanza, na kila nyumba itakuwa na vyumba vinne,” amesema.
Amesisitiza kuwa serikali haitamdhulumu mtu yeyote, bali itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa mujibu wa makubaliano yaliyowekwa.
