Jela miezi 14 kwa kumuua mtoto wake bila kukusudia

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Musoma imemhukumu Saguda Sanga kifungo cha miezi 14 jela baada ya kumkuta na hatia ya kumuua bila kukusudia mtoto wake, Baraka Saguda aliyekuwa na umri wa miezi tisa.

Mauaji hayo yanadaiwa kutokea Novemba 23, 2024 katika Kijiji cha Mwibagi, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, kwa kumpiga kichwani baada ya kumsukuma, kufuatia vurugu zilizotokea nyumbani baina yake na mkewe kwa madai kuwa amedanganya anaumwa.

Ilidaiwa akiwa anampiga mkewe kwa kutumia kipande cha kuni, alimpiga pia teke na kusababisha mtoto aliyekuwa amebebwa na mama yake kuangukia kwenye kreti ya soda iliyokuwa imehifadhiwa chumbani.

Ilidaiwa wakati mkewe akijaribu kumsaidia mtoto wao, mshtakiwa huyo alimsukuma mwanamke huyo.

Hata hivyo, Saguda alikiri kusababisha kifo cha mtoto wake bila kukusudia, kutokana na kukiri kwake, alitiwa hatiani na mahakama kwa kosa la kuua bila kukusudia kinyume na vifungu vya 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu.

Hukumu hiyo ilitolewa Februari 2, 2026 na Jaji Kamazima Kafanabo aliyesema licha ya mshtakiwa kutokusudia kumuua mwanawe, mazingira ya tukio hilo yanaonyesha vitendo vya ukatili wa nyumbani usiokubalika katika jamii.

Baada ya tukio hilo, Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa aliondoka nyumbani saa saba mchana hadi saa 11 jioni bila kumsaidia mtoto wala kutoa taarifa kwa mamlaka husika na aliporudi, mwanawe alikuwa ameshafariki dunia.

Ilidaiwa baada ya kugundua kifo cha mtoto wake, mshtakiwa aliomba familia kuficha ukweli na kudai mtoto amekufa kwa degedege, jambo lililoelezwa kuwa lilionyesha kutojutia kosa.

Upande wa Jamhuri, uliomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine dhidi ya vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kuendeleza vurugu za nyumbani na kuwa kitendo cha mshtakiwa kilikuwa cha uzembe na kilihusisha unyanyasaji wa familia, huku akimuua mtoto mchanga asiye na hatia.

Upande wa utetezi, mawakili waliomba mshtakiwa apewe adhabu ndogo au kuachiliwa huru wakidai ni kosa lake la kwanza, amekiri kosa mapema na ameokoa muda na rasilimali za Mahakama.
Walieleza kuwa mshtakiwa ana wake wawili na watoto tisa wanaomtegemea na tayari amekaa mahabusu zaidi ya miezi 14 tangu Novemba 2024, muda ambao unapaswa kuzingatiwa kama sehemu ya adhabu.

Katika hukumu yake, Mahakama ilisema adhabu ya kuua bila kukusudia inaweza kufikia kifungo cha maisha, lakini si ya lazima na Mahakama inaweza kuamua adhabu kulingana na mazingira ya kesi.

Jaji Kafanabo amesema kumbukumbu za mahakama zinaonyesha mshtakiwa alimshambulia mama wa marehemu mgonjwa mara mbili siku hiyo na mtoto alipodondoka kwenye kreti ya soda, hakuonyesha kujutia, kwa kuwa hakujaribu kumsaidia marehemu wala mkewe baada ya shambulio hilo.

Amesema kwa kuzingatia ukweli uliopo, ni wazi kwamba mshtakiwa alimshambulia marehemu kwa kumpiga mateke na kwamba, nia yake haikuwa kumuua mwanawe bali kumpiga mkewe hata hivyo, tukio zima linaonyesha ukatili usiokubalika kwa watu wa karibu wa familia yake, ambao hauwezi kuvumiliwa.

“Mahakama hii, baada ya kuzingatia mambo yanayozidisha na kupunguza uzito yaliyoainishwa hapo juu, inaweka jambo hili katika kundi la mauaji ya bila kukusudia ya kiwango cha kati na mwa mujibu wa hali ya kesi hii, Mahakama hii ina maoni kwamba muda wa kifungo ungekuwa miaka mitano.

Hata hivyo, Mahakama inaona kwamba mshtakiwa alikiri hatia ya taarifa hiyo siku ya kwanza aliposomewa Mahakamani. Mahakama inaona kwamba kukiri hatia huku kumeokoa muda mwingi kwa pande zote mbili na Mahakama, hivyo adhabu inapunguzwa na Saguda anahukumiwa kifungo cha miezi 14,” amehitimisha Jaji.