KESI YA UBUNGE WA BABA LEVO: Pingamizi lingine la AG, Msimamizi latupwa

Kigoma. Mahakama imetupilia mbali pingamizi lililowekwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya maombi madogo ya waleta maombi wanaopinga matokeo ya uchaguzi jimbo hilo.

Hii ni mara ya pili kwa wawili hao kukwaa kisiki katika shauri hilo baada ya Januari 9, 2026, mahakama hiyo kulikataa ombi lao la kusimamisha usikilizaji wa shauri hilo kwa muda usio na kikomo kwa kuwa wana nia ya kukata rufaa.

Katika maombi yao namba 275 ya 2026, walalamikaji Johary Kaborou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali waliomba kupata fursa ya kukagua na kujiridhisha kuhusu nyaraka mbalimbali, zikiwamo za matokeo ya uchaguzi huo.

Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi na AG, kupitia jopo la mawakili sita wa Serikali likiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Mark Malwambo, waliwasilisha pingamizi kupinga maombi hayo wakidai hayana msingi wa kisheria.

Mbali na Wakili Malwambo, mawakili wengine wanaounda jopo hilo ni mawakili wakuu wa Serikali Vivian Method na Lesia Majala, Wakili Mwandamizi wa Serikali George Kalenda, na mawakili wa Serikali Erick Rumisha na Edwin Webiro.

Uamuzi wa kulitupa pingamizi hilo ulitolewa Februari 3, 2026 na Jaji Victoria Nongwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, ambaye amesema anakubaliana na hoja za Wakili John Seka anayewawakilisha walalamikaji.

“Nimepima na kulinganisha hoja zilizowasilishwa, nianze kwa kukubaliana na Wakili Seka kuwa katika kujibu pingamizi lililowasilishwa, si sahihi kurejea hati ya madai katika Shauri la Uchaguzi namba 28949 la mwaka 2025,” amesema Jaji na kuongeza;
“Hii ni kwa sababu maombi ya kukagua nyaraka yanajitegemea na ndiyo maana yamesajiliwa tofauti na kupewa namba ya shauri tofauti.”

“Pamoja na kusema maombi ya kukagua nyaraka yanalenga madai katika shauri hilo la uchaguzi, pingamizi la wajibu maombi wa 1 na 3 haliwezi kuamriwa kwa kufanya mlinganisho wa maelezo katika shauri hilo na maombi haya,” amesisitiza Jaji huyo.

Akirejea misimamo ya kesi ya Alli Shaban na wenzake, Jaji Nongwa amesema anakubaliana na kanuni ya sheria kuwa pingamizi lolote la awali linatokana na kuangalia nyaraka zilizowasilishwa mahakamani pekee.
“Lakini matumizi yake, kwa maoni yangu, hayaendi hadi kupekua na kuangalia nyaraka zilizopo shauri jingine. Katika maombi ya sasa, nyaraka za shauri ni wito wa faragha na kiapo cha waleta maombi vinavyounda vyaraka vya waleta maombi,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Hizo ndo nyaraka pekee ambazo mahakama na wadai wanapaswa kuzizingatia ili kuibua, kutetea na kupinga pingamizi, na si vinginevyo.”

Amesema pingamizi la awali lilipaswa kujikita katika upungufu wa maombi ya kukagua nyaraka pekee bila kwenda nje na kuangalia nyaraka zingine katika shauri lingine.

“Kutokana na mjadala hapo juu, ni wazi kuwa pingamizi la wajibu maombi wa kwanza na wa tatu halijajikita katika matakwa ya sheria kwani linaitaka mahakama kwenda kuangalia nyaraka za shauri lingine, ambalo ni Shauri la Uchaguzi 28949 la 2025,” amesema.

Hivyo, amesema anakubaliana na Wakili wa waleta maombi (Seka) kuwa pingamizi lililoletwa na wajibu maombi wa kwanza na wa tatu halina sifa ya kuwa pingamizi la kisheria. Mahakama imetupilia mbali pingamizi la awali bila gharama kutokana na mazingira ya maombi husika.

Maombi ya kukagua nyaraka

Katika maombi yao madogo, walalamikaji hao wanne wanaiomba mahakama iwapatie fursa ya kukagua na kujiridhisha kuhusu uwepo wa nakala halisi ya Fomu namba 10, ambayo ni tamko la mgombea kuheshimu Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za Mwaka 2025, iliyojazwa kikamilifu na Chipando au Baba Levo.

Wanaomba pia kukagua na kujiridhisha kuhusu uwepo wa nakala halisi za Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumiwa katika kila kituo cha uchaguzi kuidhinisha mpiga kura aliyestahiki kupiga kura katika Jimbo la Kigoma Mjini.

Pia wanaomba kupatiwa Fomu namba 13, ijulikanayo kama Fomu ya hesabu ya karatasi za kura katika vituo vyote vya Jimbo la Kigoma Mjini, na Fomu namba 20, ijulikanayo kama taarifa ya msimamizi wa kituo cha kupigia kura.

Halikadhalika, wanaomba fursa ya kupitia na kujiridhisha kuhusu Fomu namba 21B, ijulikanayo kama Fomu ya matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika kituo cha kupigia kura katika vituo vyote vya Jimbo la Kigoma Mjini.

Mbali na fomu hiyo, wanaomba kupitia Fomu namba 22B, ambayo ni Jedwali la matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika jimbo, na Fomu namba 23B, ijulikanayo kama Jedwali la matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika jimbo kwa kila chama.

Pia wanaomba kupatiwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumiwa katika kila kituo cha uchaguzi kuidhinisha mpiga kura aliyestahiki kupiga kura.

Pingamizi la AG, Msimamizi

Hata hivyo, mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na AG waliwasilisha pingamizi la awali kupinga maombi hayo.

Walieleza maombi hayo hayana msingi kisheria kwani ni kinyume na Amri ya VI Kanuni ya 7 ya Sheria ya Mwenendo wa Madai Sura ya 33 Rekebu la Mwaka 2023, ikisomwa sambamba na aya ya 10(a) na (n) ya Hati ya Shauri la Uchaguzi.

Kwa mujibu wa wajibu maombi, katika shauri hilo la uchaguzi, walalamikaji walieleza bayana kuwa wana nyaraka zote zinazohusiana na shauri hilo.

Wakili Malwambo alijenga hoja kuwa mashauri ya uchaguzi wa wabunge yanaongozwa na Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge, Tangazo la Serikali Na. 431 la Mwaka 2025, ambazo hazijaweka utaratibu wa nini kifanyike pale ambapo nyaraka zimeenda tofauti na msingi wa madai.

“Mkwamo huo unatanzuka kwa kutumia Sheria ya Mwenendo wa Madai [Sura ya 33 Rekebu la Mwaka 2023] kama ambavyo imeelekezwa kwenye kanuni ya 24 ya Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka 2025,” amesema.

Wakili aliendelea kueleza ni msimamo wa sheria kuwa pingamizi la awali lazima lijikite katika misingi ya sheria bila kuhitaji ushahidi mwingine kulithibitisha, na halitoki hewani bali kupitia nyaraka za madai na viambatanisho vyake.

Alieleza wadai wanabanwa na nyaraka zao walizoziwasilisha kortini, na kwamba maombi hayo madogo ya waleta maombi yametokana na Shauri la Uchaguzi namba 28949 la 2025 la kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini.

“Yanayosemwa kwenye maombi ya waleta maombi hayapaswi kutofautiana na yaliyosemwa kwenye shauri la msingi, na hivyo kuifanya mahakama kuzingatia nyaraka zote zilizoletwa mbele yake katika kuamua maombi,” amesema.

Wakili Malwambo alisema maombi ya kupata fursa ya kukagua, kujiridhisha na kupatiwa nakala halisi au nakala durufu ya nyaraka walizoziorodhesha, yanapishana na malalamiko shauri la uchaguzi katika aya ya 10(a).

Amesema aya hiyo inaonyesha kuwa mawakala wa ACT Wazalendo walikuwa na nyaraka zinazoombwa kukaguliwa na kupatiwa nakala halisi au durufu.

Akijibu hoja hizo, Wakili Seka, akirejea misimamo ya uamuzi wa mahakama, amesema ilikemea kitendo na mchezo wa mawakili kuleta hoja za kujadiliwa kwenye kesi ya msingi au maombi kama pingamizi la awali.

Wakili Seka amejenga hoja kuwa pingamizi hilo la awali limeletwa mapema kwani linahitaji kujadili maelezo ya shauri la msingi, yaani Shauri la Uchaguzi namba 28949 la 2025, hivyo kulifanya pingamizi hilo likose sifa ya kisheria.

Amesema kitendo cha wakili wa Serikali kurejea aya za shauri la uchaguzi pamoja na nyaraka zake kinaonyesha dhahiri kuwa hili sio pingamizi la kisheria.

Kuhusu Amri ya VI Kanuni ya 7 ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Wakili Seka alisema kuwa kifungu hicho kinalenga kulifanya shauri lililowasilishwa kuwa thabiti kwa kuweka msimamo kuwa mtu akishawasilisha maombi yake ya awali, hawezi kubadilisha madai au kuleta madai mapya kiholela.

Wakili Seka amesema maombi ya kukagua nyaraka, yaani daftari na fomu, si madai mapya, bali ni utaratibu wa kutafuta ushahidi ulioruhusiwa kisheria ili kuthibitisha madai yaliyopo kwenye hati ya shauri mama.

Amesema kitendo cha mawakili wa Serikali kurejea aya ya 10(a) na 10(n) ya hati ya madai katika Shauri la Uchaguzi namba 28949 la 2025 ni kuingia kwenye mtego wa kudhania kuwa mawakala wa ACT Wazalendo waliozuiwa kuingia na daftari la wapiga kura ndio walalamikaji katika shauri hilo.

“Kusema fomu ina kasoro na kisha kuomba kuikagua fomu halisi ni hatua za kimantiki zinazosaidiana,” amesema Wakili Seka na kusisitiza kuwa huwezi kuthibitisha makosa bila kuona nakala halisi iliyopo kwenye mamlaka.