Dar es Salaam. Mashaka, wasiwasi na woga ndio mtindo mpya wa maisha ya Watanzania wanaoishi nchini Marekani, baada ya kuimarishwa kwa hatua za udhibiti wa uhamiaji nchini humo.
Hatua hizo za Serikali ya Marekani inayoongozwa na Rais Donald Trump zimeibua mashaka sio kwa raia wanaoishi nchini bila vibali halali pekee, bali hata wenye vibali wanahofia.
Hofu hizo, kwa mujibu wa raia hao wanaoishi katika Taifa hilo, zinatokana na kile wanachosema, maofisa uhamiaji na wale wa forodha, wamekuwa wakiwasimamisha mara kwa mara kuwahoji na kuwataka waoneshe vibali vyao.
Februari 2025, ubalozi wa Tanzania nchini Marekani ulithibitisha Watanzania 24 wanashikiliwa katika vituo vya uhamiaji nchini humo.
Ingawa wengi waliamini kinachotokea ni hatua za mpito, hatimaye hali ikaendelea na mwaka mmoja baadaye, matumaini ya furaha na amani kwa Watanzania wanaoishi huko yakapotea.
Katika majimbo kadhaa, maofisa wa uhamiaji wamekuwa wakifanya operesheni za wazi, wakikamata watu wanaodhaniwa kuishi Marekani bila vibali halali.
Kutoka oparesheni chache za maofisa wa uhamiaji katika majimbo mbalimbali nchini humo, sasa imekuwa kawaida kushuhudia makundi ya maofisa hao wakipita huku na kule kuwasaka wahamiaji wa Marekani wasio na vibali halali.
Kwa Watanzania wengi wanaoishi Marekani, hali hiyo imewalazimisha kuishi kwa tahadhari ya kudumu. Baadhi wameacha kutumia mitandao ya kijamii. Kurasa zao zimekuwa kimya, wakihofu kubainika na kukamatwa.
“Najihisi kama wanaweza kunifuatilia kupitia mtandao. Ninaishi New York na tumeshuhudia misako mingi,” amesema mmoja wa Watanzania aliyeishi Marekani kwa zaidi ya miaka 10.
Katika Jiji la New York, eneo maarufu la Canal Street limekuwa uwanja wa mapambano kati ya waandamanaji na maofisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE).
Machafuko kama hayo yameshuhudiwa pia katika majimbo mengine kadhaa, huku kukaribia kwa uchaguzi wa katikati ya muhula kukiifanya operesheni hiyo kuwa suala la kisiasa linalotarajiwa kuathiri uamuzi wa wapiga kura.
Minnesota kitovu cha oparesheni
Kati ya majimbo yote, Minnesota limejitokeza zaidi katika vichwa vya habari. Mwaka 2026, watu wawili waliotambulika kama Watanzania walikamatwa katika jimbo hilo na kuhamishiwa kwenye kambi ya wahamiaji wasio na nyaraka katika jimbo la Texas, hatua ya mwisho kabla ya kurejeshwa nchini.
Kwa mujibu wa Mtanzania anayeishi Minnesota, Ndaga Mwakabuta, ingawa jimbo hilo halina jamii kubwa ya Watanzania, limekuwa miongoni mwa maeneo yenye operesheni kali zaidi za ICE dhidi ya wahamiaji wasio na vibali.
Tukio la kuuawa kwa Renee Good wakati wa makabiliano na maofisa wa ICE wiki moja baada ya sikukuu ya mwaka mpya lilidhihirisha ukubwa na ukali wa operesheni hizo.
Katika tukio lingine, Alex Pretti, muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) mwenye umri wa miaka 37, aliuawa kwa kupigwa risasi na mawakala wa Serikali alipokuwa akipinga utekelezaji wa sera za uhamiaji.
Minnesota, jimbo lililopo Kaskazini mwa Marekani karibu na mpaka wa Canada, ndilo nyumbani kwa Mwakabuta kwa miongo kadhaa.
Yeye ni miongoni mwa Watanzania waliohamia Marekani kihalali na kuanzisha familia. Hata hivyo, hilo halijamfanya awe nje ya mashaka.
“Nimeshawahi kusimamishwa mara kadhaa. Naonyesha nyaraka zangu, wanazikagua, halafu wanaondoka,” amesema.
Ameeleza polisi wa majimbo wana mamlaka ya kumuomba mkazi atoe kitambulisho, huku maofisa wa uhamiaji wa shirikisho kama ICE wakiwa na haki ya kumkaribia mtu hadharani na kuomba nyaraka.
Hata hivyo, raia ana haki ya kukaa kimya na kuomba wakili na ICE hairuhusiwi kuingia katika nyumba binafsi bila kibali cha mahakama.
Atlanta nako hali si shwari, Mtanzania aliyeolewa na raia wa Marekani, amechagua kuishi kwa siri kwa miaka mingi. Akiwa na watoto wawili waliozaliwa Marekani, amejitenga na mikusanyiko ya Watanzania, matukio ya kijamii, hata makundi ya WhatsApp.
Kwa wengi kama yeye, kuachana na utambulisho wa zamani na kujinasibisha kikamilifu na maisha ya Marekani ni mkakati wa kujilinda hasa wakati masoko ya wahamiaji, wafanyabiashara wadogo na matukio ya kijamii yamekuwa yakilengwa katika misako.
Hofu imewafanya baadhi ya wahamiaji kubeba pasi zao za Marekani kila wanapotoka, kutokana na matukio ya wahamiaji halali, wakiwamo Waafrika kukamatwa kimakosa.
California, Minnesota na Chicago, Illinois ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na misako na maandamano. Baadhi ya waliokamatwa wamelalamikia kubaguliwa kwa rangi zao wakati wa kukamatwa.
Katika Jimbo la Washington, Mtanzania mmoja amesema hutegemea mitandao ya kijamii, hasa Reddit, kufuatilia maeneo ambayo maofisa wa ICE wameonekana.
Amesema kumekuwa na taarifa zinazochapisha barabara wanazopita maofisa hao wa uhamiaji, namba za magari yao na taarifa nyingine zozote zinazosaidia kuwaepuka.
“Huu ndio ulikuwa mwaka niliopanga kumleta binti yangu kutoka Dar es Salaam, lakini kwa sasa haiwezekani,” amesema.
Kwa mujibu wa Mwakabuta, hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa jamii za wahamiaji. Baadhi ya Watanzania wasio na nyaraka kamili wamehama kutoka jimbo moja kwenda jingine kwa hofu ya kukamatwa, huku wengine wakiondoka kabisa Minnesota. ICE sasa imepanua msako kutoka mitaani hadi kwenye anuani wanazodai kuwa na taarifa zake.
Oparesheni hizo, zimeshuhudia zikiwafuata hata wanafunzi wenye visa halali ili kuthibitisha usajili wao vyuoni na kuhakiki kama bado wanahudhuria masomo.
“Mmoja wa Watanzania aliyekuwa kwenye mchakato wa kupata Greencard alifuatwa hadi kazini. Walihakiki taarifa zake zote,” amesema Mwakabuta, akiongeza baadhi ya maofisa huonekana kuwa na malengo ya idadi ya watu wa kukamata.
Watanzania wengi waliopo Marekani wana nyaraka halali na wameishi huko kwa muda mrefu. Hata hivyo, mashambulizi ya Septemba 11 yalibadilisha mfumo wa uthibitishaji na ajira, yakifanya safari ya uraia kuwa ndefu na ngumu zaidi.
Minnesota, ambayo awali ilirahisisha upatikanaji wa leseni za udereva na huduma za kifedha bila kujali hali ya uhamiaji, sasa imebadilisha mwelekeo wake.
Baadhi ya Watanzania wameacha kazi zinazohitaji kuwepo ofisini, wengine wamechagua kufanya kazi kwa mtandao, huku baadhi wakibaki nyumbani. Milango ikiwa imefungwa, wakisubiri hali itulie, ingawa bado mambo yanaendelea kuonekana magumu, hasa ikizingatiwa utawala wa Rais Donald Trump unatarajiwa kumalizika Januari 20, 2029.
Huko Houston, Texas, ambako kuna idadi kubwa ya Watanzania, misako imeongezeka tangu 2024. Mwishoni mwa 2025, zaidi ya watu 1,500 walikamatwa. Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rice waliunda ramani ya ICE kufuatilia shughuli za utekelezaji wa sheria.
Georgia nako, jumuiya ya Watanzania imewahimiza walio katika hatari kuhakikisha wanawasiliana mara kwa mara na kupanga masuala ya kifedha endapo watakamatwa ghafla.
Minnesota, Kanisa la Minnesota Swahili Christian Congregation, limeanzisha huduma za ushauri nasaha na namba ya dharura kusaidia jamii ya Waafrika Mashariki.
Watanzania wameelekezwa kuepuka maeneo yenye operesheni nyingi za ICE, ikiwamo Portland Avenue, Kusini mwa Minneapolis, karibu na eneo alikouawa Renee Good.
Kwa Watanzania waliokuwa na ndoto ya kusoma, kuhamia au kuungana na familia zao Marekani, matumaini hayo kwa sasa yanaonekana kufifia.
“Ndoto hiyo kwa sasa haipo,” amesema Mwakabuta, akiwashauri Watanzania kuangalia maeneo mbadala ya Kwenda Canada, ambayo bado yana sera rafiki kwa wahamiaji.
Idadi ya Watanzania waliorejeshwa nchini haijulikani, hasa kwa kuwa baadhi ya waliokaa zaidi ya muda wa visa walichagua kuchukua uraia wa nchi nyingine ili kuomba hifadhi ya kisiasa.
Kwa sasa, jumuiya za Watanzania Marekani zimewahimiza wanachama wake kuwa macho, kuwasiliana mara kwa mara, na kuhakikisha familia zao zinafahamu walipo iwapo watakumbwa na mkasa wa kukamatwa au kurejeshwa nyumbani.
