Uwajibikaji ni jambo muhimu ambalo linachochea matokeo yanayotarajiwa na linapokosekana basi matokeo yanakuwa siyo yanayotarajiwa na aghalabu mafanikio huonekana kwenye eneo husika linalohitaji kupiga hatua.
Kwenye mfumo wa uendeshaji wa Serikali, uwajibikaji ni muhimu kwa sababu unalenga kuleta matokeo chanya kwa wananchi ambao wanatarajia kupata huduma stahiki kutoka kwa viongozi na watendaji wa serikali.
Kuna mifumo tofauti ya uwajibikaji serikali ambapo katika zama hizi za kidigitali, dunia inahamishia utendaji wake katika njia za kidigitali siyo tu kurahisisha njia za mawasiliano, bali kuleta matokeo ya haraka.
Wakati akizindua kampeni za uchaguzi za Chama cha Mapinduzi (CCM), Oktoba 28, 2025, mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan aliahidi mambo mengi yatakayofanyika ndani ya siku 100 za kwanza ikiwamo kuanzisha mifumo ya kidigitali ya uwajibikaji.
Katika eneo hilo, Samia alisema wakipewa ridhaa na wananchi, wataanzisha mifumo rafiki ya uwajibikaji ambapo mawaziri, wakuu wa mikoa na watendaji wengine wa Serikali, watatoa taarifa na kujibu maswali kutoka kwa wananchi kwa njia ya kidigitali na SMS za bure.
Mgombea huyo alisisitiza kwamba hicho ndiyo kitakuwa kipimo cha mawaziri kwa kuzingatia idadi ya shida za wananchi zilizowasilishwa kwake, amejibu ngapi na ngapi amezichukulia hatua zinazotakiwa.
Katika uchaguzi huo, Samia alitangazwa mshindi, akaapishwa Novemba 3, 2025, hivyo akaunda serikali na siku chache zijazo anafikisha siku 100 za kwanza tanguaanze muhula wake wa pili madarakani.
Mwananchi limeangazia utekelezaji wa ahadi hii ya Rais Samia na kubaini kwamba Serikali imeanza utekelezaji wake kwa kuzindua mifumo hiyo itakayowawezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao moja kwa moja.
Utekelezaji Wizara ya Afya
Januari 26, 2026, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa alizindua rasmi mfumo wa “Ongea na Waziri”, jijini Arusha, hatua ya kimkakati inayolenga kuisogeza sekta ya afya karibu zaidi na wananchi, kusikiliza sauti zao na kujibu changamoto zao kwa vitendo.
Katika hafla hiyo, Mchengerwa alisema kuwa mpango wa “Ongea na Waziri” unatuma ujumbe mmoja ulio wazi kwa Watanzania wote kwamba sauti ya mwananchi si maoni ya pembeni, bali ndiyo dira ya maboresho ya huduma za afya.
“Katika sekta ya afya, haya ni mapinduzi makubwa. Tunapozungumzia afya, hatuzungumzii tu mifumo na majengo, bali tunazungumzia heshima ya binadamu, ulinzi wa maisha, na haki ya kila Mtanzania kupata huduma bora kwa wakati,” alisema Waziri huyo.
Uzinduzi wa mpango huo pia umeweka msisitizo mkubwa kwenye matumizi ya teknolojia kama chombo cha kuboresha utoaji wa huduma, si kama mtindo wa kujionyesha.
Katibu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema wizara hiyo inaendelea kutekeleza kikamilifu ahadi ya Rais Samia ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya teknolojia na mifumo ya kisasa ya mawasiliano.
Amesema wizara inatumia mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa e-Mrejesho, vituo vya mawasiliano kwa njia ya simu (call centres), pamoja na mitandao ya kijamii kama YouTube na WhatsApp ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi.
“Hatua hii inalenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za sekta ya maji, sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata majibu ya haraka kuhusu changamoto na masuala yanayowahusu,” amesema Mwajuma.
Ameongeza kuwa wizara imetoa namba za mawasiliano za viongozi na watendaji wa sekta ya maji ili kuwawezesha wananchi kutoa kero, maoni, ushauri na taarifa mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa miradi na huduma za maji.
“Taarifa zote zinazopokelewa kupitia mifumo hiyo, hufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wahusika husika ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na ufumbuzi wa changamoto zao kwa wakati,” amesema.
Amesema kwa sasa Wizara ya Maji ina mpango wa kuboresha vituo vya mawasiliano (call centres) ili viunganishwe na Kituo cha Taifa cha Mawasiliano.
“Kwa sasa Wizara inakusudia kuboresha vituo vya mawasiliano (call centers) ili viungane na kituo cha Taifa kuwezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa taarifa zinazotolewa,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema katika kutekeleza agizo la Rais la kuwasiliana moja kwa moja na wananchi, amezunguka halmashauri zote sita za mkoa huo, kufanya mikutano ya hadhara na kugawa namba za simu za watendaji wote wa serikali, ikiwemo namba yake binafsi.
Mhita amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika kupokea na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati.
“Tunakutana na wananchi na kuwapa namba hizi ili kuwapa fursa ya kuwasiliana nasi moja kwa moja, hususan wale wenye changamoto, waweze kueleza kero zao kwa urahisi,” amesema Mhita.
Ameongeza kuwa namba zake pamoja na za watendaji wengine zinapatikana kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kuhakikisha wanawafikia wananchi moja kwa moja.
“Wananchi wamekuwa wakinipigia simu au kunitumia ujumbe mfupi kueleza changamoto zao, na hilo ndilo tunalotekeleza kwa vitendo,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame amesema mkoa huo unatarajia kuzindua mfumo wa kidijitali utakaowawezesha wananchi kuwasilisha kero na masuala mbalimbali ya maendeleo moja kwa moja kwa uongozi wa mkoa, mwishoni mwa wiki hii.
“Mbali na kuzindua mfumo huo wa kidijitali, tutatoa pia taarifa ya utekelezaji wa ahadi nyingine zilizotekelezwa ndani ya siku 100 za Rais Samia tangu aingie madarakani. Taratibu za kuratibu zinaendelea ili kuwapa wananchi fursa ya kuhudhuria,” amesema.
Amesema siku 100 za Rais Samia zinatamatika Februari 13, hivyo maandalizi ya kukamilisha mfumo huo yanaendelea hadi sasa.
“Baada ya uzinduzi tutatoa maelezo ya kina, kwani mfumo huu unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumamosi. Tutautoa kwa umma na kueleza ni pakeji gani tumewaandalia wananchi pamoja na lengo la kuwasiliana nao moja kwa moja,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema mkoa huo umeweka utaratibu wa mawasiliano na wananchi kwa muda mrefu huku juhudi zikielekezwa katika kuendelea kuboresha mifumo hiyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Telack amesema mkoa ulizindua mfumo wa “Ongea na Mkuu wa Mkoa” unaowapa wananchi fursa ya kuwasilisha kero zao moja kwa moja kwa kupiga simu.
“Tulizindua mfumo wa ‘Ongea na Mkuu wa Mkoa’ ambapo kila mwananchi anapata nafasi ya kupiga simu na kueleza kero yake. Simu yangu kila mwananchi anayo, hivyo si jambo jipya bali tunaendelea kuboresha,” amesema Telack.
Mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Shukrani Sabinus ameusifu mfumo huo akisema una mchango mkubwa katika kuimarisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao, ingawa ameonyesha wasiwasi juu ya utekelezaji wake.
“Ni mfumo mzuri katika kuwasiliana na wananchi, lakini wananchi ni wengi na kila mmoja ana changamoto zake. Ni vigumu kutekelezeka ipasavyo endapo mtu mmoja ndiye anayetegemewa kumaliza shida zote,” amesema.
Ameishauri Serikali kuimarisha ugatuzi wa madaraka ili kila kiongozi awajibike moja kwa moja kwa wananchi katika maeneo yao, jambo litakalosaidia kupunguza dhana ya kumtegemea Rais au mkuu wa mkoa pekee katika kutatua changamoto za wananchi.
Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Profesa Samuel Wangwe amesema mfumo huo ni muhimu katika kupata mrejesho kwa viongozi walioko madarakani na kupima namna utendaji wao unavyowagusa wananchi.
Amesema ili kuimarisha uwajibikaji, ni lazima kuwepo na mfumo wa mrejesho unaowahusisha viongozi wa ngazi zote kuanzia ofisi ya mkuu wa mkoa, wilaya, halmashauri, tarafa hadi kata.
“Ili kuhimiza uwajibikaji, lazima kuwe na mrejesho kwa Mkuu wa Mkoa, ngazi ya wilaya, halmashauri, tarafa na kata. Ikiwa mrejesho unapelekwa kata, basi nakala yake lazima ipelekwe tarafa au ngazi ya juu zaidi,” amesema Profesa Wangwe.
Amesema utekelezaji wa mfumo huo utaleta tija kwa sababu utahamasisha viongozi kuwajibishana na kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
