Mustakabali wa ODM bila Odinga, kikipitia nyakati ngumu

Nairobi, Kenya. Miezi mitatu imepita tangu kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga alipofariki dunia, Oktoba 15, 2025 na kuacha ombwe kubwa ndani ya chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM).

Katika nyakati zake za furaha, marehemu Odinga alikuwa na mtindo wake wa kuzungumza jukwaani hususani vitendawili, jambo ambalo liliongeza hamasa ya wananchi kumsikiliza wakati huku akichanganya mzaha na ukweli ndani yake.

Tangu amefariki dunia, chama chake kimekuwa katika harakati za kutaka kujaza pengo lake huku kaka yake, Oburu Odinga akikaimu nafasi ya kiongozi wa chama cha ODM huku kukiwa na maoni mseto kuhusu ushawishi wake ndani ya chama hicho.

Odinga alikuwa si tu mwanasiasa, bali taasisi ya kisiasa iliyozaa imani, matumaini na maono ya Kenya mpya kwa wanasiasa na kizazi chipukizi kilichotamani mageuzi.

Sasa taifa hilo la Afrika Mashariki, linaingia katika kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 bila uwepo wa ‘Baba’ hali inayofungua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa siasa za upinzani na ushawishi wa mirengo mikuu ya kisiasa.

Raila alikuwa nguzo ya siasa za upinzani tangu miaka ya 1990, akipigania mfumo wa vyama vingi, haki za raia na uwajibikaji wa Serikali.

Aliwahi kufungwa, kuumizwa na kudai kupokonywa ushindi mara kadhaa, lakini alibaki mstari wa mbele katika harakati za mageuzi.

Wafuasi wake walimwona kama shujaa wa ukombozi wa kisiasa na kumpa jina ‘Baba’ huku wapinzani wake wakimchukulia kama mpinzani asiyechoka.

Odinga kupitia ODM, alishiriki chaguzi kadhaa ambazo alishiriki sambamba na wagombea wengine, ambapo licha ya nguvu kubwa aliyekuwa nayo, yeye binafsi na muungano wa kisiasa, lakini alishindwa kwenye chaguzi hizo.

Hata hivyo, hata baada ya kushindwa katika chaguzi, chini ya Raila, ODM ilishikiliwa kwa nguvu, pembe zake zikivutwa karibu kwa utepe mwembamba. Baada ya kifo chake, utepe huo unaonekana kukatika.

Sasa kuna mchanganyiko ndani ya ODM, taa zimezimwa na mapazia yamevutwa kwa nguvu. Kuna kimbunga kinachozunguka ndani ya ODM. Ni kama msimu wa mwisho wenye giza.

Wakati huohuo, mandhari ya siasa inazidi kuwa ya kukata tamaa na isiyo na huruma, moshi mweusi, mchafu na unaosonga koo. Tai wanazunguka, kila mmoja akitafuta fungu la chama.

Uwanja wa nguvu, mtu aliyeshikilia ODM pamoja, hayupo tena. Raila alisimamisha mpangilio katika vurugu za siasa za vyama nchini Kenya, kwa busara, uzito wa haiba na nidhamu ya hali ya juu.

Sasa kilichobaki ni kumbukumbu na kusambaratika kwa sura ya kumbukumbu hizo ni tupu na za kuumiza moyo.

ODM sasa ipo njia panda, ikikabiliwa na kitendawili kama kinachozikumba harakati, jamhuri au himaya zozote baada ya kifo cha kiongozi wake. Katika fasihi, Shakespeare aliangazia migogoro ya urithi wa madaraka, mvutano wa kizazi na machafuko yanayofuata baada ya kuanguka kwa mhimili wa umoja.

Kifo cha Odinga kinafanana na cha Shakespeare: utaratibu wa zamani unasambaratika, vijana wanapigania madaraka na himaya inatetemeka na kupasuka.

Shakespeare katika kitabu chake cha Henry IV, ndiyo alitoa mwangwi unaofanana na hali ya ODM kwa sasa. Tamthilia hiyo inaakisi Roma baada ya kifo cha Kaizari Augustus mwaka 14 BK wakati himaya hiyo ilipoingia katika kipindi cha wasiwasi kwa sababu zinazofanana na hali ya ODM.

Kwanza, baada ya Augustus, wasomi wa zamani wa jamhuri, walinzi wa ulimwengu uliokuwa unafifia waliwaangalia kwa shaka vijana waaminifu wa himaya. Augustus alikuwa amejenga mfumo ulioshikamana pamoja na haiba ya mtawala mkuu (na ndani ya ODM, hata baada ya kifo, kivuli cha Raila bado ni kikubwa).

Hali hiyo hiyo inajirudia ODM. Kuna mgawanyiko ulio wazi: wasomi wa zamani dhidi ya vijana waaminifu, kukiwa na mpasuko unaoonekana kati ya kundi la zamani linaloongozwa na Oburu Odinga na vijana waaminifu akiwemo Babu Owino, Edwin Sifuna, Winnie Odinga na wengine.

Katika Roma ya kale, vijana waliokuwa chini ya kivuli cha Augustus waliamini kuwa mustakabali ulikuwa wao.

Ndani ya ODM, vijana waliokuwa chini ya kivuli cha Raila, pia wanaamini mustakabali ni wao na wamekataa wito wa kuondoka chamani.

Pili, baada ya kifo cha Augustus, Tiberius mrithi aliyesitasita, aliingia kuziba pengo. Hakuwa kipenzi cha watu, lakini aliisimamia himaya kwa ustahimilivu mkubwa. Ndani ya ODM, baada ya kifo cha Raila, Oburu aliingia.

Ingawa baadhi wanasema alikuwa mshauri wake mkuu, tofauti na Raila mwenye mvuto mkubwa, Oburu huenda si kipenzi cha watu. Roma ilinusurika kwa sababu Tiberius, kama Henry IV, alielewa kwamba wakati mwingine tendo kubwa zaidi la uongozi ni kuzuia kusambaratika na hiyo ndiyo inapaswa kuwa maelezo ya kazi ya Oburu.

Katika tamthilia ya King Lear ya Shakespeare, tunapata mwangwi wa kihistoria wa Roma baada ya kifo cha Constantine Mkuu, wakati vita kati ya ndugu vilipozuka. Constantine alipokufa mwaka 337 BK, aliacha watoto watatu, mdogo mwenye tamaa na asiye tayari kugawana madaraka. Himaya iligawanywa kati yao kwa lengo la kudumisha amani.

Badala yake, hatua hiyo iliibua uhasama mkali. Majenerali na wasimamizi wakongwe walijaribu kuwazuia watawala vijana, lakini wana wa Constantine walikuwa wameazimia kuchonga hatima yao wenyewe.

Matokeo yake kulitokea vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ikiwa ODM haitakuwa makini, vita vya kisiasa vya ndani vitaibuka na watakaopoteza zaidi watakuwa chama chenyewe na wanachama wake.

ODM sasa imesimama katika nafasi ile ile iliyoachwa na Augustus, Constantine na King Lear. Suala siyo kama makundi yatatokea, tayari yapo.

Suala ni kama ODM itachagua njia ya Tiberius aliyeshikilia kitovu au njia ya watoto wa Constantine wa Roma (na watoto wa King Lear wa Shakespeare), waliyoipasua himaya vipande vipande.

ODM kimejikuta katika mvutano wa ndani kuhusu mwelekeo wake ujao huku Naibu Kiongozi wa Chama, Godfrey Osotsi, na Kiongozi wa mpito, Oburu, wakikinzana angalau kwa maneno kuhusu namna ODM inavyopaswa kushirikiana na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto.

Osotsi ameibuka kuwa mkosoaji mkuu wa mtindo wa uongozi wa Oburu, akionya kile anachokitaja kuwa ni msimamo mgumu unaopuuza sauti za viongozi wakongwe wa chama.

“Sina tatizo na kiongozi wetu Oburu Odinga, lakini ni muhimu asikilize pia maoni ya viongozi wengine wa chama. Hata Raila Odinga alikuwa akisikiliza kila sauti ndani ya ODM,” anasema Osotsi akinukuliwa na Dawan Africa, akirejea urithi wa marehemu Odinga wa uongozi shirikishi.

Zaidi ya mtindo wa uongozi, Osotsi ameonya juu ya hatari za kimkakati.

Anaitaka ODM isiwe na pupa ya kuingia kwenye muungano na UDA, akisema makubaliano ya haraka yanaweza kukigharimu chama.

“Tusiwe na haraka ya kujiunga na UDA ya Rais Ruto. Ruto anaweza kutuacha njiani na kuunda muungano mwingine na kambi tofauti,” anaonya, akidai kuwa kuna juhudi za makusudi za wapambe wa UDA kuingia na kuathiri ODM.

Hata hivyo, Oburu hajachukua kauli hizo kwa mzaha. Akizungumza katika hafla ya uwezeshaji vijana ya Nyota mjini Kisumu,  iliyohudhuriwa pia na Rais Ruto, Oburu alitetea kwa nguvu mkakati wa mazungumzo wa chama.

Alisisitiza kuwa ODM haifuatilii vyeo wala nafasi serikalini, bali masuala yanayogusa maisha ya wananchi wa kawaida.

“Naomba niwe wazi kabisa…ODM haifuati kazi ya mtu yeyote. Nafasi yako kama Makamu wa Rais iko salama. Tunachojadili ni kinachowanufaisha wananchi wetu,” alisema, akijibu madai kuwa chama kinataka kuingia serikalini au kudhoofisha viongozi kama Naibu Rais wa Kenya, Kithure Kindiki.

Kwa mujibu wa Oburu, mazungumzo hayo ni ya vitendo na ya kuangalia mbele. Akiwa na chini ya miaka miwili kuelekea Uchaguzi Mkuu, alisema ODM haiwezi kuacha fursa zipite bila maandalizi.

Lengo, alisisitiza, ni kuhakikisha wafuasi wa chama wananufaika moja kwa moja na ODM inapata ushawishi mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa katika serikali ya mwafaka mpana.

Katika hatua inayoongeza msisimko wa kisiasa, Rais Ruto ameashiria kuwa yuko tayari kwa mazungumzo, diplomasia na maridhiano.

Kamati Kuu ya Uongozi ya UDA (NEC) imempa jukumu la kuongoza mazungumzo na ODM, ikisisitiza siasa shirikishi na mshikamano wa kitaifa.

Ruto ameyataja mazungumzo hayo kama fursa ya ushindi wa pande zote, bila kuhatarisha nafasi au utambulisho wa kisiasa.

“Kuna nafasi ya kila Mkenya. Si lazima mmoja apoteze ili mwingine apate,” alisema, akijitokeza kama kiongozi anayetafuta umoja wakati mvutano wa kisiasa unaongezeka.

Kwa sasa, uwanja wa siasa umewekwa kwa mchezo wa hatari kubwa. Ndani ya ODM, chama kinakabiliwa na jukumu gumu la kusawazisha wito wa ushirikishwaji na tahadhari unaotolewa na viongozi kama Osotsi, dhidi ya maono ya kimkakati na msimamo thabiti unaoendelezwa na Oburu.

Nje ya chama, mkono wa wazi wa Rais Ruto unatoa fursa pamoja na hatari nafasi ya ushirikiano, lakini pia mtihani wa umoja na uthabiti wa ODM.

Kinachowekwa mezani si muungano pekee. ODM iko katika wakati wa uamuzi, je, itaweza kucheza kwa ustadi mchezo wa kuunganisha mshikamano wa ndani, utambulisho wa chama na diplomasia ya kitaifa? Au migawanyiko ya ndani na muungano wa pupa na UDA vitapunguza urithi wake na nguvu yake ya kujadiliana?

Kadiri pazia la siasa linavyoendelea kufunguka, jambo moja ni dhahiri:

siasa za Kenya hazichoshi kamwe, na hatua zitakazochukuliwa na ODM sasa zinaweza kuweka mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Mchezo umeanza, wachezaji wako wazi, na dau ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote.