Petroli bei juu, dizeli na mafuta ya taa kicheko

Dares Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto vinavyotumia petroli wataendelea kuugulia maumivu ya ongezeko la bei katika mafuta katika mwezi Februari 2026 huku watumiaji wa dizeli na mafuta ya taa kicheko.

Hiyo ni baada ya petroli kuendelea kupanda kwa mujibu wa bei kikomo zilizotolewa na  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( Ewura) zitakazotumika kuanzia leo Februari 4, 2026.

Ongezeko la bei ya petroli nchini inashuhudiwa wakati ambao bei kikomo kwa Februari 2026 za mafuta hayo katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 6.41, asilimia 0.50 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 1.70 kwa mafuta ya taa.

Licha ya bei ya mafuta kupungua kwenye soko la dunia katika mwezi husika gharama za kuagiza mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 1.88 kwa mafuta ya petroli na asilimia 1.65 kwa mafuta ya taa na kupungua kwa wastani wa asilimia 5.10 kwa mafuta ya dizeli.

Katika bandari ya Tanga zimepungua kwa asilimia 1.62 kwa petroli na dizeli na katika bandari ya Mtwara zimepungua kwa asilimia 9.24 kwa mafuta ya petroli na hakuna mabadiliko kwenye mafuta ya dizeli.

Gharama za mafuta (FOB) na gharama za uagizaji (Premiums) zinalipwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani. Kwa bei za mwezi Februari 2026, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umeongezeka kwa asilimia 1.86.

Kufuatia hilo sasa watumiaji wa mafuta yatakayopita katika Bandari ya Dar es Salaam watanunua lita moja kwa Sh2,788 kutoka Sh2,778 iliyotumika Januari 2026, petroli watanunua kwa Sh2,701 ikiwa ni pungufu kutoka Sh2,726 iliyotumika mwezi uliopita.

Kwa watumiaji wa mafuta ya taa, watanunua kwa Sh2,746 kwa lita ikiwa ni pungufu kutoka Sh2,763.

Kwa watumiaji wa mafuta yanayopitia bandari ya Dar es Salaam lita moja watanunua kwa Sh2,849 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2,839 iliyotumika Januari mwaka huu, dizeli watanunua kwa Sh2,762 ikiwa ni pungufu kutoka Sh2,787 iliyokuwapo mwezi uliotangulia.

Wale wa mafuta ya taa watatumia Sh3,807 kupata lita moja ya ikiwa ni pungufu kutoka Sh2,854 waliyokuwa wakitumia mwezi jana.

Upande wa Mtwara na mikoa Jirani inayotegemea bandari ya kusini, watatumia Sh2,881 kupata lita moja ya mafuta ya petroli iliyo ongezeka kutoka Sh2,870 waliyokuwa wakiitumia mwezi uliotangulia.

Kwa upande wa dizeli ni kicheko kwani sasa watatumia Sh2,794 kupata lita moja ikiwa ni chini kutoka Sh2,818 waliyotumia mwezi uliopita na mafuta ya taa wakitumia Sh2,838 iliyoshuka kutoka Sh2,856.

Kufuatia hilo, Ewura imewataka wafanyabiashara kuuza mafuta kwa bei zinatajwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekiuka agizo hilo.

“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani,” imeelezwa.

Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

“Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita,” imeelezwa.

Stakabadhi hizo zitatumika kama ushahidi kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokezamalalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa. Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli.